1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yakataa matakwa ya Trump kuhusu nyuklia

Iddi Ssessanga
13 Januari 2018

Iran imesema makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 hayawezi kujadiliwa tena, baada ya rais wa Marekani Donald Trump kutishia kuiondoa Marekani ikiwa "kosoro zilizomo" hazijatafutiwa ufumbuzi.

https://p.dw.com/p/2qo1q
Iran Atomwissenschaftler
Picha: picture alliance/dpa/epa

"Makubaliano ya nyuklia ni mkataba unaotambuliwa kimataifa na uliokamilika na hayajadiliwi," ilisema wizara ya mambo ya kigeni mjini Tehran siku ya Jumamosi, na kuongeza kuwa iran kamwe haitokubali mabadiliko yoyote kwenye mkataba huo au kutwikwa majukumu mapya.

Makubaliano hayo ya mwaka 2015, maarufu kama Mpango Mpana wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), ulisainiwa na Marekani chini y autawala uliopita wa Rais Barack Obama pamona na Iran, China, Urusi, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.

Unalenga kuhakikisha kuwa Iran inatumia uwezo wake wa kinyuklia kwa njia za amani, huku ukiizuwia kutengeneza silaha za nyuklia. Kwa kukubali kutekeleza mkataba huo, Iran iliondolewa vikwazo vya kiuchumi.

USA Trump erhöht den Druck auf den Iran
Rais Donald Trump ametishia kuiondoa Marekani kwenye makubaliano ya nyuklia ya Iran.Picha: picture alliance/dpa/AP/E. Vucci

Nafasi ya mwisho

Lakini Trump, ambaye anapaswa kuidhinisha uendelezwaji wa mkataba huo kila baada ya siku 90 na kuidhinisha usitishwaji wa baadhi ya vikwazo kila baada ya siku 120 na 180, ameukosoa vikali mkataba huo.

Akitangaza  uamuzi Ijumaa wa kuendeleza usitishwaji wa baadhi ya vikwazo vinavyohusiana na mauzo ya mafuta na mfumo wake wa benki, Trump alisema alikuwa akichukuwa hatua hiyo ili kupata makubaliano ya washirika wa Marekani barani Ulaya kushughulikia kasoro hizo.

Alisema makubaliano hayo yaliipa Iran mambo "mengi sana kwa kutoa kidogo sana," na kutaka makubaliano mapya ambayo yataweka vikwazo vipya dhidi ya Iran ikiwa itatengeneza au kujaribisha makombora ya masafa marefu, kuzuwia ukaguzi au kupiga hatua kuelekea kuunda silaha za nyuklia.

"Hii ndiyo nafasi ya mwisho," alisema Trump. "Bila kuwepo mkataba wa aina hiyo, Marekani haitasitisha tena vikwazo ili kubakia katika mkataba wa nyuklia."

Ujerumani, Urusi zatoa kauli

Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema katika taarifa kuwa "itaendelea kushinikiza utekelezaji kamili wa makubaliano ya nyuklia," na kuongeza kuwa serikali mjini Berlin itakutana na washirika wake wa Ulaya ili kuamua kwa pamoja namna ya kushughulikia msimamo wa Trump.

Sergey Ryabkov
Naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Ryabkov.Picha: AP

Urusi imesema Marekani itakuwa inafanya kosa kubwa kwa kujiondoa kwenye mkataba huo, na kuongeza kwamba Moscow itapigana kuhakikisha mkataba huo unaendelea kuheshimiwa. Naibu waziri wa mambo ya nje Sergei Ryabkov, alikosoa matamshi ya rais Trump, na kusema inavyoonekana uamuzi wa ndani kujiondoa kwenye makubaliano hayo unakaribia kufanywa au unaendelea kufanywa.

"Hili linaweza kuwa mmoja ya makosa makubwa zaidi ya kidiplomasia ya Marekani, kosa kubwa kabisaa katika sera ya Marekani," alisema. Ryabkov alisema Moscow lazima kuungana na Ulaya na China, na kufanya kazi kubwa ili kuulinda mpango huo wa sasa, huku akilalamikia kile alichosema ni jaribio la Marekani kutumia mabavu.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae, afpe.

Mhariri: Sylvia Mwehozi