1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran na Israel

8 Julai 2008

Iran endapo ikihujumiwa na Israel,italipiza kisasi kwa kuripua Tel Aviv na manuwari za Marekani katika Ghuba.

https://p.dw.com/p/EYcU

Iran imeonya jana kwamba itairipua Israel na manuwari za kimarekani zinazoegesha katika Ghuba kama jibu lake la kwanza kwa hujuma yoyote ile itakayofanywa katika vinu vyake vya mradi wa nuklia.

Mji wa tel Aviv na kundi la manuwari za kimarekani katika ghuba zitakua shabaha ya kwanza itakayoripuliwa na kuashwa moto katika jibu kali la Iran-alisema Ali Shirazi,msaidizi wa Kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.

►◄

Marekani na mshirika wake wa chanda na pete katika Mashariki ya Kati-Israel ,hazikuondoa kabisa uwezekano wa kuhujumu zana za kinuklia za Iran,ambazo kambi ya nchi za magharibi inahofia zinalenga kuunda silaha za kinuklia.

Karibuni hivi wasi wasi umeibuka kuwa shambulio dhidi ya Iran lakaribia kufanyika.Hii ilitokana na mazowezi ya kijeshi yaliofanywa nchini Ugiriki ambayo yalioonekana kimsingi ni kujiandaa kuhujumu vinu vya nuklia vya Iran.

Msemaji wa Imam mkuu wa Iran, Ali Shirazi amesema "utawala wa wayahudi unawashinikiza viongozi wa Ikulu ya Marekani (White House) kupanga njama ya kijeshi kuihujumu Iran .Kwahivyo, Iran italipiza kisasi ikiwa upumbavu kama huo utafanyika."-alisema Shirazi.

Haikufahamika wazi lakini, iwapo Shirazi akukusudia hapo Tel Aviv kama ni mji tu au dola la Israel ambalo Jamhuri ya kiislamu ya Iran, halilitambui.

Iran mara kwa mara, ikionya kujibisha pigo kali uchokozi wowote kwake ,lakini onyo kali kama hili alilotoa jana Ali shirazi halikuwa la kawaida.

Taarifa ya Shirazi imetoka wakati walinzi wa kimapinduzi-wanajeshi wa Iran- wameanza duru mpya ya mazowezi kujinoa na kuwa tayari kwa zahama yoyote huku mvutano ukizidi juu ya mradi wa kinuklia wa Iran.

Luteka iliopewa jina "Mtume III" (Great Prophet III) ikiingiza vikosi vya wanamaji na vya makombora vya jeshi la walinzi wa mapinduzi-revolutionary Guarads lengo lake ni kukuza uweto wa kupigana wa vikosi hivyo.

Walinzi wa mapinduzi ndio wenye jukumu la makombora makali kabisa ya masafa marefu ya Iran pamoja na yale ya "Shahab 3" ambayo yaweza kuifikia Israel na kambi za Marekani ziliopo Ghuba la uajemi.

Juu ya hivyo, juhudi za kibalozi pia zinasonga mbele kuepusha balaa kama hilo.Iran imeitikia mkono ilionyoshewa na dola kuu ili kuumaliza msukosuko huu wa kinuklia. Wajumbe wa kibalozi wamo kuchambua hivi sasa kile kinachoonekana kama "jibu la kutatanisha " kutoka Teheran.

Mjumbe wa Umoja wa Ulaya anaehusika na siasa za nje,Javier Solana atafunga safari ya Iran kwa mazungumzo juu ya mradi huo wa kinuklia-kwa muujibu alivyoarifu Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa,kandoni mwa mkutano wa dola kuu 8-tajiri huko Japan.

Mwenyekiti huyo wa sasa wa Umoja wa Ulaya, hakutaja lini Bw.Solana atafunga safari hiyo ya Iran.

Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad, aliarifu juzi tu jumatatu kwamba, Iran kamwe haitaacha kurutubisha madini yake ya uranium-shughuli ambayo anadai, inalenga kuipatia Iran nishati ya umeme.

Dola kuu zimejitolea kuipa Iran teknolojia ya kisasa mradi tu isimamishe mradi huo.Iran haioneshi kuregeza kamba au kuitikia hodi hodi hizo mlangoni mwake.

Mjumbe wake mjini London amearifu kwamba dola kuu zinapoteza wakati wao kwa kuishikilia Iran iachane na mradi wake. Haitafanya hivyo.