Ipi tafauti ya Lowassa, Magufuli kwa mpigakura wa kawaida? | Tanzania Yaamua 2015 | DW | 01.10.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Tanzania Yaamua 2015

Ipi tafauti ya Lowassa, Magufuli kwa mpigakura wa kawaida?

Watanzania wanaingia kipindi cha lala salama cha kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, huku tofauti kubwa zaidi ya mawazo ikiwa kati ya wateuliwa wawili walio mstari wa mbele kuwania urais.

Wapigakura katika moja ya chaguzi.

Wapigakura katika moja ya chaguzi.

Wakati John Pombe Magufuli anatetea rikodi ya zaidi ya miaka 50 na sera za chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM), mpinzani wake mkubwa ambaye ni mshika bendera wa chama cha upinzani cha CHADEMA chini ya mwamvuli wa umoja wa upinzani (UKAWA), Edward Ngoyai Lowassa, anasisitiza kuwa ni "wakati wa kuweka mtazamo mpya kwa taifa hilo kubwa la Afrika Mashariki.

Wakati fulani, Magufuli alionekana kujikwaa kwa makusudi kwa kutumia alama ya chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA ya M4C (Movement for Change) ili kusukuma mbele kampeni yake.

Umati wa watu wenye furaha na vikundi vya wasanii hujitokeza kupata ujumbe wa uchaguzi mahali popote wawania hao wawili wa urais wanakokwenda. Kwa kifupi, Magufuli anatoa ahadi za “kusafisha nyumba” na Lowassa anaahidi kuwatoa mamilioni ya watu katika umaskini na kutoa elimu bila malipo kuanzia chekechea mpaka chuo kikuu.

Tafauti kwenye muonekano

Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya CHADEMA chini ya UKAWA, Edward Lowassa.

Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya CHADEMA chini ya UKAWA, Edward Lowassa.

Muonekano wao ndio jambo kubwa linaloleta tofauti katika uchaguzi wa mwaka huu. Lowassa, ambaye alianza kuonekana kuwavutia watu wengi kwa nafasi ya urais kabla ya kufarakana na CCM, ameendelea hadi sasa kufanya hivyo, kwani umaarufu wake kwa nchi nzima haukufifia na Watanzania wengi wanaelekea kumkubali kwamba ndiye mtu awezaye kuleta mabadiliko yanayotakiwa nchini.

Kwa upande wake, Magufuli anasaidiwa kwa kiasi fulani kujulikana kupitia vyombo vya habari kama mtendaji wa maamuzi ya serikali akiwa waziri katika wizara mbalimbali alizowahi kuziongoza, ingawa wakosoaji wa mambo wanadai kwamba naye si msafi kama anavyotangazwa.

Wanatoa sababu kuwa lengo la CCM kumtangaza ni kupoteza hisia mbaya kuhusu mteuliwa wake kwa kumuonyesha kuwa ni mzoefu na ni chaguo linalopendelewa na wengi.

Vyama vidogo 'vyafunikwa' na mafuriko ya UKAWA, CCM

Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, John Magufuli.

Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, John Magufuli.

Kwa upande wao, vyama vidogo vilivyo katika kinyang'anyiro cha urais vinakabiliwa na kazi ngumumno. Vyengine mikutano yao - ikilinganishwa na ile ya Lowassa au Magufuli - ni kama mikusanyiko tu ya kawaida kandokando ya barabara, sokoni na vituo vya mabasi ambayo haikuhitaji maandalizi ya viwanja wala kuiombea sehemu kubwa.

Licha ya kutokuwa na matumaini makubwa, wateuliwa wa vyama hivyo wanaendelea kupaza sauti zao kuhusu mambo kadhaa yanayowagusa wananchi na kueleza nini wangelifanya wakipewa ridhaa. Mambo hayo ni pamoja na kuboresha miundombinu maeneo ya vijijini, kufufua na kujenga viwanda vya kusindika mazao ya kilimo na kuimarisha uadilifu na uwazi katika utumishi wa umma.

Kwa ujumla, Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi na kuzitaja zote katika muda mfupi wa kampeni za uchaguzi ni jambo lisilowezekana, lakini ni jambo la faraja kuwa wagombea wote wanaonekana kuwa makini kuhusu mateso na matarajio ya wananchi, ingawa hofu ya wapigakura iko pale pale kwamba ahadi za kampeni huenda zisitimizwe. Awamu zilizopita za utawala wa nchi zinakumbukwa kwa ahadi ambazo hazikutekelezwa na visingizio vya kushindwa kuzitekeleza.

Nafasi ya vijana kwenye uchaguzi

Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Anna Mghirwa.

Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Anna Mghirwa.

Mbali ya maoni hasi, ambayo huenda yakawa na athari kwa mgombea mmoja au mwingine, ni sehemu ndogo ya wapiga kura vijana, ambao ndio wengi, wanaotilia maanani maoni hayo.

Mgombea anayewavutia lazima aongee kwa ufasaha kuhusu masuala yanayowahusu katika maisha yao ya leo – ajira ambazo zitawaletea hali bora ya maisha, ustawi wa kiuchumi na kijamii – na siyo historia ya uhuru wa taifa.

Vijana ndio wadau wakubwa katika uchaguzi huu na hiyo inaeleza wazi sababu yao kuwa lengo la vyama vyote vya siasa katika kampeni zinazoendelea sasa. Kutokana na wingi wao kitakwimu, vijana wanatarajiwa kupiga kura kwa idadi kubwa kuliko ilivyokuwa katika chaguzi zote zilizopita Tanzania.

Bila kujali kiwango chao cha elimu, hali ya ajira, makazi yao yalipo kama ni vijijini au mijini, vijana wanaelekea kuwa wameshafanya uamuzi wa uchaguzi wao wakielewa kuwa huyo watakayemchagua, watakuwa wamempa madaraka ya kuwaongoza kuelekea wanakokutaka.

Licha ya vikundi fulani vinavyojitegemea kufanya tafiti za maoni kuhusu wagombea urais, matokeo yao hayakuwa na lolote la kushangaza, zaidi ya kuongeza mashaka na wakosoaji wametahadharisha kuwa tafiti hizo, zikiwa na nafasi kubwa ya makosa, zinaweza kuashiria mchezo wa rafu siku ya uchaguzi.

Mwandishi: Anaclet Rwegayura/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com