1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gharika zinatokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi

9 Agosti 2021

IPCC imetahadharisha kuwa viongozi duniani watashindwa kutekeleza ahadi zao za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi hadi pale watakapofanya uamuzi wa haraka wa kupunguza pakubwa uzalishaji wa gesi chafu.

https://p.dw.com/p/3ykDR
Türkei verheerende Waldbrände
Picha: YASIN AKGUL/AFP

Ripoti ya jopo la wataalamu wa mabadiliko ya tabia nchi IPCC imetahadharisha kuwa viongozi duniani watashindwa kutekeleza ahadi zao za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi hadi pale watakapofanya uamuzi wa haraka wa kupunguza pakubwa uzalishaji wa gesi chafu.

IPCC imesema matukio ya moto, ukame na mvua kubwa katika sehemu mbalimbali duniani yametokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Soma zaidi: Maelfu wazikimbia nyumba zao kuepuka moto wa msituni Ugiriki

Uchafuzi unaotokana na gesi ya kaboni umepanda kwa kiwango kikubwa duniani kinachotishia kuvuruga mpango wa kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabia nchi, wa kuweka viwango vya joto ulimwengu kusalia nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Celsius kufikia mwishoni mwa karne hii, na kwamba kiwango hicho kitaongezeka ndani ya kipindi cha miaka 15 ijayo.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti iliyoidhinishwa na wajumbe kutoka nchi 195 na kuchapishwa leo Jumatatu na jopo la wataalamu wa mabadiliko ya tabia nchi IPCC.

Viwango vya joto duniani vimeongezeka kwa karibu nyuzi joto 1.1 katika kipimo cha Celsius.

Utafiti huo, unatokea katika wakati ambapo joto kali na mvua kubwa vinashuhudiwa katika mataifa mbalimbali duniani. Hali hiyo ya hewa inachora picha kamili ya jinsi dunia ilivyoathirika na mabadiliko ya tabia nchi.

WS Indien Überschwemmung in Allahabad
Picha: Sanjay Kanojia/Getty Images/AFP

"Hii ndio hali halisi ilivyo,” amesema Valerie Masson-Delmotte, mmoja wa wenyekiti wa jopo la watalaamu wa mabadiliko ya tabia nchi waliyoiandaa ripoti hiyo.

Kwa kuchoma mafuta na kutoa gesi chafu hewani, viwango vya joto duniani vimeongezeka kwa karibu nyuzi joto 1.1 katika kipimo cha Celsius.

Kwa mujibu wa ripoti ya IPCC, hali hiyo imechangia kwa kiasi kubwa kuongezeka kwa mvuke na mvua kubwa. Pia vimbunga na upepo mkali vimeongezeka katika sehemu mbalimbali duniani kote.

Katika baadhi ya sehemu duniani, viwango vya ukame vimeongezeka na kufikia kiwango cha kutisha.

Tangu ripoti ya mwisho ya IPCC ya mwaka 2014, wanasayansi wamebaini kuwa athari za mabadiliko ya tabia nchi zimechangia kwa kiasi kikubwa moto, mafuriko na hata vimbunga vinavyoshuhudiwa katika sehemu tofauti tofauti duniani.

Wasayansi wanasema kuwa, suluhu ya haya yote ni rahisi-kuacha kuchoma mafuta na kutoa gesi chafu hewani lakini serikali, wafanyibiashara na hata watu wa kawaida wanashindwa kufanya hivyo ilhali wengine wanaofanya, wanajikokota.

Kwa mujibu wa shirika la utafiti la Ujerumani la Climate Action Tracker, licha ya nchi kadhaa zilizojiunga kwenye mkataba wa Paris wa kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, kutangaza kuahidi kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa, viongozi hao wanaonekana kwenda kinyume na ahadi walizotoa na badala yake wanafuata sera ambazo zinatishia kuongeza kiwango cha joto hadi nyuzi joto 3.