IOC yatetea adhabu yake dhidi ya Urusi | Michezo | DW | 15.11.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Doha, Qatar

IOC yatetea adhabu yake dhidi ya Urusi

Rais wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki - IOC Thomas Bach ametetea namna alivyoshughulikia tuhuma za matumizi ya dawa za kusisimua misuli dhidi ya Urusi.

Rais huyo amepinga ukosoaji uliotolewa kwenye michezo ya Olimpiki iliyofanyika Rio de Jeneiro, Brazill kwa kusema hakuna mji ambao ungeweza kushinda zabuni ya kuandaa michezo hiyo mwaka 2024 kama si mpango wake wa kurejelewa kwa "Agenda ya Olimpiki ya 2020".

Mbele ya mkutano mkuu wa jumuiya ya kamati za kitaifa za Olimpiki Jumanne hii, Bach alionekana kukabiliana na tuhuma mbaya zilizotolewa kuhusu mwenendo kwenye michezo ya Olimpiki, tuhuma za matumizi ya dawa za kusisimua misuli, changamoto zilizojitokeza wakati wa maandalizi ya Rio na wasiwasi kuhusu gharama za kuandaa mashindano.   

Bach amesema, michezo ya Rio ilikuwa na mafanikio makubwa, akizingatia idadi iliyovunja rekodi ya watazamaji kupitia runinga na mitandao ya kijamii, ingawa hakusema chochote kuhusu viti vilivyosalia wazi na mapungufu ndani ya taasisi hiyo ambayo pia yalivuruga mashindano hayo. 

Alienda mbali zaidi kwa kukingia kifua hatua ya kamati ya kimataifa ya mashindano hayo ya kuifungia Urusi kushiriki kwenye mashindano hayo, akisema amepata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa viongozi wengi wa dunia kuhusu hatua hiyo. Taasisi ya kimataifa ya kupambana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli ilitaka Urusi kufungiwa kufuatia ripoti ya kiuchunguzi iliyoonyesha uhusika wa serikali ya Urusi.

Ripoti ya mwisho kuhusu matumizi ya dawa hizo inatarajiwa kutolewa mwezi ujao na itaangazia madai dhidi ya Urusi na udanganyifu  uliofanywa kwenye sampuli za wanamichezo katika michezo ya kipindi cha baridi iliyofanyika Sochi, mwaka 2014. Makamishna wawili wa OIC wanaweza kukumbwa na tuhuma hizo. 

Hatua zinazoweza kuchukuliwa ni pamoja na kuwekewa vikwazo kwa Urusi kushiriki michezo ya kipindi cha baridi mwaka 2018, huko Pyeongchang, Korea Kusini.

Mwandishi: Lilian Mtono/ APE.
Mhariri: Daniel Gakuba