1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

India yachukua msimamo mkali dhidi ya Pakistan

Thelma Mwadzaya4 Desemba 2008

Nchi ya India imeonya kuwa itatumia mbinu zote ili kukabiliana na nchi jirani ya Pakistan kufuatia mashambulio ya mabomu yaliyotokea mjini Mumbai wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/G8vM
Bendera za nchi jirani za Pakistan na India


Kwa upande mwingine Marekani inaishinikiza Pakistan kutoa ushirikiano kamili katika uchunguzi wa mashambulio hayo unaoendelea.Akizungumza katika mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari Waziri wa mambo ya kigeni wa India Pranab Mukherjee alisisitiza kuwa nchi yake itafanya kila iwezalo kujilinda.

''Serikali ya India itafanya kila iwezalo ili kulinda mipaka yake na haki ya raia wake kuwa na maisha ya amani kwa kutumia mbinu zote.Tunataraji kupata ushirikiano kamili wa jamii ya kimataifa katika vita dhidi ya ugaidi.''


Mashambulio hayo ya mabomu yaliyotiokea kwenye makao makuu ya kibiashara mjini Mumbai yalitokea wiki iliyopita na kudumu kwa kipindi cha saa sitini.Jumla ya wapiganaji 10 waliowasili mjini humo kwa mahori walihusika na kushambulia hoteli mbili za kifahari za Taj Mahal na Oberoi vilevile kituo cha Kiyahudi.

Mpiganaji mmoja pekee aliyesalimika ndiye aliyekamatwa na maafisa wa usalama wa India.Alikiri kuwa raia wa Pakistan na mwanachama wa kundi la kiislamu la Lashkar-e-Taiba lililo na makao yake kwenye eneo la mpaka wa India na Pakistan.

Takriban watu 180 waliuawa katika shambulio hilo na wengine yapata 300 kujeruhiwa.Pakistan kwa upande wake imekanusha kuhusika na mashambulio hayo na imependekeza kuundwa kwa tume ya pamoja ya uchunguzi.