1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Pakistan: "Mzozo nchini Iran Ungezusha balaa"

Tatu Karema
17 Januari 2020

Waziri mkuu wa Pakistani Imran Khan amesema nchi yake inafanya juhudi kusuluhisha mizozo katika ukanda wa mashariki na kukosoa jumuiya ya kimataifa  kutojitolea kikamilifu kuhusiana na mzozo wa Kashmir.

https://p.dw.com/p/3WLQk
DW-Chefredakteurin Ines Pohl im Exklusivinterview mit Imran Khan
Picha: DW

Waziri mkuu Khan amesema Pakistan inajaribu kusawazisha uhusiano wake na Marekani na China ambapo China inataka kuwekeza nchini Pakistan suala ambalo litaleta mgongano na Marekani na pia kwamba taifa lake linashiriki katika mpaka wa pamoja na mataifa yanayoghubikwa na mizozo kama Afghanistan na Iran, Khan anaelezea jinsi anavyomudu kayafanya hayo yote.

Imran Khan: ''Nilijiunga na siasa kwasababu nilihisi kwamba Pakistan ina uwezo mkubwa. Wakati nilipokuwa ninakuwa, Pakistan ilikuwa na uchumi uliokuwa ukiimarika kwa kasi ya juu zaidi barani Asia na kutumika kama mfano wa maendeleo katika miaka ya 60. Lakini tukapoteza njia. Lengo langu la kuingia katika siasa lilikuwa kudumisha uwezo huo''.

Kiongozi huyo ameongeza kwamba ni kweli wanaishi katika eneo gumu lenye mizozo na inawapasa kuwa makini kuweka wizani katika uhusiano wao na majirani. Kwa mfano Saudi Arabia ni moja wa washirika wakubwa zaidi wa Pakistan na taifa hilo limekuwa likijitolea pakubwa katika masuala ya Pakistan na wakati huo huo, kuna Iran, ambayo wakati wote wamedumisha uhusiano mwema.

Hivyo basi mzozo wa kijeshi kati ya Saudi Arabia na Iran utakuwa na athari kwa Pakistan. Khan amesema kuwa wanajaribu kila wawezalo kuhakikisha kuwa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili hausambaratiki na kwamba ni eneo ambalo haliwezi kustahimili kuwa na mzozo mwingine .

Khan ameendelea kusema kuwa kwa upande mwingine kuna Afghanistan ambapo Pakistan inajaribu kile iwezavyo kuleta amani nchini humo. Afghanistan ni taifa ambalo limekuwa na misukosuko mingi na kuathirika sana katika muda wa miaka 40 iliyopita. Khan anasema kuwa wanaomba kundi la Taliban, Marekani na serikali ya Afghanistan zipate amani.

Screenshot Exklusivinterview mit Imran Khan
Waziri mkuu wa Pakistani Imran Khan

Mhariri mkuu wa DW Ines Pohl alitaka kufahamu jukumu la serikali ya Pakistan katika kutuliza hali ya taharuki iliyotanda katika eneo la Kashmiri na inayozidi kuwa mbaya ambapo India na Pakistan zilikaribia kuingia katika vita huku waziri mkuu wa India Narendra Modi akiliondolea hadhi maalum eneo la Kashmir linalomilikiwa na India mwezi Agosti mwaka jana.

Imran Khan alikuwa na haya ya kusema : ''Mimi nilikuwa kiongozi wa kwanza kuionya dunia kuhusu kile kilichokuwa kikiendelea nchini India. India imetekwa na mantiki ya itikadi kali inayojulikana kama "Hindutva." Ni mantiki ya kundi la Rashtriya Swayamsevak Sangh (RSS).  Kundi hilo ni shirika la kisiasa lililoundwa mwaka 1925, na kuchochewa na wanazi wa Ujerumani  huku waanzilishi wake wakiamini ukuu wa ubaguzi. Na kama mantiki hiyo ya wanazi ilivyojengwa kutokana na chuki dhidi ya walio wachache, kundi la RSS pia limejikita katika chuki dhidi ya waislamu na makundi ya walio wachache ikiwa ni pamoja na wakristo.''

Khan aliendelea kusema kuwa ni mkasa kwa  India na majirani wake kwamba taifa hilo limetekwa na kundi hilo la RSS shirika ambalo pia lilimuuwa Mahatma Gandhi. Alisikitika kuwa India, taifa lililojihami kinyuklia linatawaliwa na watu aliowaita wenye itikadi kali na pia kuzingirwa kwa Kashmir  kwa takriban miezi mitano sasa.

Kuhusu iwapo yuko tayari kuzungumza na waziri mkuu Modi kuhusu masuala haya, Khan amesema kuwa baada ya kuwa waziri mkuu, alifanya juhudi za kuzungumza na serikali ya India na waziri mkuu Modi. Amesema kuwa katika hotuba yake ya kwanza kama waziri mkuu alisema kuwa iwapo India ingechukuwa hatua moja mbele, wangechukuwa hatua mbili kuifuata na kutatua tofauti zao, lakini akaja kufahamu baadaye kwamba India haikujitolea katika ombi lake.

Kuhusiana na uhuru wa watu wa Kashmir kama Khan alivyotetea mwaka jana katika Umoja wa Mataifa iwapo jamii ya kimataifa itazingatia zaidi matakwa ya Khan iwapo maandamano katika eneo la Kashmir linalosimamiwa na Pakistan pia yataruhusiwa, Khan amesema kuwa hilo ni la watu wa Kashmir kuamua wanachokitaka na kwamba Pakistan iko tayari kwa kura ya maamuzi kwa hivyo Kashmir inapaswa kuamua iwapo inataka kusalia na Pakistan ama kuwa huru.