1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IMF yatabiri anguko uchumi Mashariki ya Kati

Lilian Mtono
28 Oktoba 2019

Ripoti iliyochapishwa na Shirika la fedha ulimwenguni IMF imesema sintofahamu ya kisiasa na bei za mafuta zinazobadilika badilika Mashariki ya Kati kwa pamoja vinazuia ukuaji wa uchumi katika ukanda huo mwaka huu. 

https://p.dw.com/p/3S36J
Saudi-Arabien Drohnenangriffe
Picha: AFP

Ripoti hiyo ya kikanda iliyochapishwa hii leo inaonyesha makadirio ya ukuaji wa uchumi kwenye ukanda wa Mashariki ya Kati kufikia asilimia 0.5 tu kwa mwaka huu wa 2019, ikilinganishwa na asilimia 1.6 ya mwaka 2018.

Kulingana na ripoti hiyo, kuongezeka kwa shughuli kwenye sekta za mafuta na gesi kunatarajiwa kuimarika hadi asilimia 2.7 ya ukuaji ifikapo mwaka 2020, ingawa takwimu hizo ni za chini sana ikilinganishwa na makadirio ya awali.

Ukanda huo unajikongoja kutokana na vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, lakini pia shambulizi dhidi ya mitambo mikubwa zaidi ya uzalishaji wa mafuta duniani mwezi uliopita nchini Saudi Arabia, ambayo ilisababisha kupanda kwa kwa kiasi kikubwa kwa bei ya mafuta tangu vita vya Ghuba vya mwaka 1991. Tangu wakati huo, ukanda huo uliendelea kuwa imara.

IMF imesema, bei za mafuta zimeongezeka kutoka dola 55 kwa pipa hadi dola 75 tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Libanon Beirut Proteste
Picha: picture-alliance/Zuma/ Le Pictorium/B. Tarabey

Aidha, ripoti hiyo kwa upande mwingine imesema inayapitia mapendekezo ya mageuzi ya dharura yaliyotangazwa na serikali ya Lebanon wiki iliyopita, huku likisisitiza kwamba mageuzi hayo yanatakiwa kutekelezwa mara moja kufuatia viwango vikubwa vya madeni  vinavyolielemea taifa hilo pamoja na upungufu wa fedha.

Lebanon imekumbwa na maandamano ya takriban siku kumi ya kupinga ufisadi unaofanywa na wanasiasa nchini humo pmoja na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Iran nako hali yatabiriwa kuwa tete.

Wiki iliyopita serikali ilitangaza hatua kadhaa zilizolenga kuwatuliza waandamanaji kwa upande mmoja lakini pia kuwashawishi wafadhili wa kimataifa kwamba itapunguza nakisi katika bajeti yake ya mwaka ujao. 

Mkurugenzi wa IMF eneo la Mashariki ya Kati na Asia ya Kati Jihad Azour ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa Lebanon ni mojawapo ya nchi zenye viwango vya juu zaidi vya deni la serikali, kama sehemu ya uzalishaji wa kiuchumi, huku utabiri ukionyesha nakisi kufikia kufikia asilimia 9.8 ya pato la ndani la taifa kwa mwaka huu na asilimia 11.5 mwaka ujao.

Azour amesema, mapendekezo hayo yanatakiwa kutekelezwa mara moja ili kurejesha utulivu wa uchumi nchini humo na uaminifu pamoja na kuchochea ukuaji lakini pia kutoa suluhu kwenye masuala yaliyoibuliwa na waandamanaji. 

Ripoti hiyo imeigusia pia Iran, na kusema itahitaji pipa moja ya mafuta kuuzwa kwa dola 194.6 ili kuisawazisha bajeti yake ya mwaka ujao. Kulingana na IMF, Iran inayokabiliwa na vikwazo vya Marekani inatarajiwa kukumbwa na nakisi ya asilimia 4.5 mwaka huu, na 5.1 kwa mwaka ujao.

Kulingana na Azour, uchumi wa Iran unatarajiwa kuanguka kwa asilimia 9.5 mwaka huu, tofauti na makadirio ya awali ya asilimia 6, huku pato la ndani likabakia palepale kwa mwaka ujao.