1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afisa wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) amesema leo.

23 Novemba 2017

Ukuaji wa chumi wa Zimbabwe ni wa kusuasa kutokana na matumizi makubwa yanayofanywa na serikali, usimamizi duni wa fedha za kigeni na mabadiliko yasiyo na tija. IMF imesema leo.

https://p.dw.com/p/2o9A7
Kombobild Mnangagwa (l) Mugabe (r)
Kushoto ni Emmerson Mnangagwa na kulia ni Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe.Picha: AP

Zimbabwe ilikuwa ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye uchumi unaotia matumaini lakini ukaporomoka kwa miongo mingi.

Inaelezwa kuwa hayo yalitokea baada ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Robert Mugabe, kutekeleza sera ambazo zilijumuisha kukamatwa kwa Wazungu waliokuwa wakimiliki mashamba makubwa ya biashara, jambo lililosababisha kupaa kwa bei ya bidhaa kwa kiwango cha juu.

Mugabe alijiuzulu juzi baada ya kupata shinikizo kutoka kwa jeshi la nchi hiyo, chama tawala ZANU-PF, na idadi kubwa ya wananchi, ikiwa ni baada ya kukaa madarakani kwa karibu miongo minne.

Kiongozi mpya wa ZANU-PF, Emmerson Mnangagwa, anatarajiwa kuapishwa kesho kuwa rais wa nchi hiyo.

Simbabwe Protest in Harare, Forderung Rücktritt Robert Mugabe
Wananchi walioandamana kushinikiza Mugabe ajiuzuluPicha: Reuters/M. Hutchings

Zimbabwe haijapata mikopo kutoka kwa wakopeshaji wa kimataifa tangu mwaka 1999 baada ya kushindwa kulipa madeni yake huku ikiwa na deni la nje la zaidi ya randi 1.75 billioni.

"Hali ya uchumi  bado ni ngumu Zimbabwe," anasema Afisa wa juu wa Shirika la Fedha la Kimataifa, (IMF) Gene Leon katika taarifa yake ya jana, akiongeza kuwa hatua za haraka ni muhimu katika "kupunguza kwa kiwango endelevu na kushirikiana na jumuiya za kimataifa kupata msaada wa kifedha unaohitajika."

Mchumi huyo wa IMF anasema Zimbabwe haina budi kutatua kwanza deni la Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya.

"Zimbabwe haina budi kuwa tayari kuwekeza katika sera za uchumi wa juu na mageuzi ya kimiundo," anasema.

Mwandishi: Florence Majani/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef