1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Imeripotiwa kwamba mahabusu waliotekwa nyara huko Yemen wameuwawa

Miraji Othman15 Juni 2009

Maiti za mahabusu waliotekwa nyara Yemen zimepatikana

https://p.dw.com/p/IAFz
Gari la jeshi la usalama la Yemen likipiga doria katika mji mkuu, SanaaPicha: AP


Saba kati ya mahabusu tisa walio raia wa kigeni, akiwemo mtoto, leo walipatikana wamekufa huko kaskazini mwa Yemen. Hii ni kwa mujibu wa afisa wa usalama. Alisema walizipata maiti za watu hao waliotekwa nyara, na kwamba waliuliwa. Wawili kati ya watoto wawili waliotekwa nyara na kikundi hicho inaripotiwa walipatikana wakiwa hai.

Maiti hizo zilipatikana na mtoto wa kiongozi wa kikabila huko Noshour, mashariki ya eneo la milima la mkoa wa Saada ambako watu hao tisa walitekwa nyara. Wakuu wa huko Yemen waliwatuhumu waasi wa madhehebu ya Kishia ya Zaidi katika mkoa wa Saada kwamba waliwakamata Wajerumani saba, mmoja wao akiwa ni daktari, mhandisi wa Kiengereza na mwalimu wa kike anayetokea Korea Kusini. Waasi hao waliikana tuhuma hiyo.

Watu hao tisa, wakiwemo watoto watatu wa na wauguzi wawili wa kike wa Kijerumani, ni wa kutoka kikundi cha kimataifa kinachotoa misaada, na walikuwa wakifanya kazi kwa miaka 35 sasa katika hospitali ilioko katika mkoa wa Saada unaopakana na Saudi Arabia. Mmoja wa wauguzi hao aliolewa na mmoja wa Wajerumani waliotekwa nyara.

Hakuna mtu aliyedai dhamana ya kuwateka nyara watu hao. Hiki ni kisa cha mwishoni katika mlolongo wa vitendo vya utekaji nyara dhidi ya raia wa kigeni katika nchi hiyo ilio moja ya nchi maskini kabisa duniani. Ikiwa mauaji hayo yamefanywa na majeshi ya kikabila, hiyo itakuwa ni mara ya kwanza kwa mahabusi wa kike kuuliwa. Hata hivyo, wanawake wawili wa Kibelgiji waliuliwa mwaka 2008 na watu waliokuwa na silaha katika mashambulio ya ghafla ambapo wakuu wa serekali waliulaumu mtandao wa al-Qaida.

Mjini Berlin, Kansela Angela Merkel alisema hakuweza kuhakikisha juu ya ripoti ya vifo vya mahabusu hao, wakiwemo Wajerumani watatu, wanaosemakana walipigwa risasi. Alisema wanasonga mbele kuzichunguza habari hizo. Wizara ya mambo ya kigeni ya Korea Kusini ilisema hawana habari juu ya tukeo hilo na ilikuwa inaichunguza ripoti hiyo.

Afisa wa Yemen alisema jana kwamba kikundi hicho kilitekwa nyara na kikundi cha waasi wa kutoka kabila la Huthi la madhehebu ya Zaidi ambacho kimekuwa kikipigana dhidi ya serekali ya Sanaa tangu mwaka 2004. Kuuliwa watu hao kumefanyika siku moja baada ya wakuu huko Yemen kumkamata mtu anayetajika kuwa mfadhili mkubwa kutoka mtandao wa al-Qaida katika Yemen na Saudi Arabia.

Lakini msemaji wa waasi hao alisema tuhuma hizo hazina msingi na akasema utekaji nyara huo umefanyika katika eneo linalodhibitiwa na majeshi ya usalama katika mji wa Saada.

Pia watu waliokuwa na bunduki alhamisi iliopita waliwakamata kama mahabusu raia wa kigeni 28 walio wafanya kazi wa shughuli za tiba, wakiwemo Waarabu , kutoka hospitali ya Amran, kaskazini ya Sanaa, na kuwaachia huru siku ya ijumaa baada ya kufanyika upatanishi baina ya makabila. Pia watu wa kabila Huthi walilauamiwa kwa kisa hicho.

Raia wa kigeni mara nyingi hutekwa nyara huko Yemen na watu wa makabila kama njia ya kupata matakwa yao kutoka upande wa serekali kuu kuhusu mizozo yao ya kienyeji. Zaidi ya raia wa kigeni 200 wametekwa nyara mnamo miaka 15 iliopita. Wote waliachiwa huru bila ya kudhuriwa, isipokuwa Waengereza watatu na M-Australia mmoja waliokamatwa na watu wenye siasa kali za Kiislamu hapo mwaka 1998, na waliuliwa pale majeshi ya usalama yalipoyashambulia maficho yao.


Mwandishi: Miraji Othman

Mhariri : Josephat Charo