Ikulu ya White House yautaja uchunguzi wa ung′atuzi kuwa kinyume cha sheria. | NRS-Import | DW | 09.10.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

NRS-Import

Ikulu ya White House yautaja uchunguzi wa ung'atuzi kuwa kinyume cha sheria.

Ikulu ya White house imetangaza kusimamisha ushirikiano na kile ilichokitaja kuwa uchunguzi unaofanywa kinyume cha sheria unaotekelezwa na wabunge wa chama cha Democratic ili kumng'atua mamlakani rais Donald Trump.

Mawakili wa rais Donald Trump hapo jana walituma barua ndefu kwa wabunge na kusema wazi kwamba ikulu ya White House haitashiriki katika uchunguzi huo ambao wiki iliyopita ulipigwa jeki kwa kutolewa kwa malalamishi ya mfichua siri kwamba Trump alitafuta usaidizi wa kisiasa kutoka Ukraine.

Wakili wa White House Pat Cipollone ameandika kuwa,  kwa kuzingatia uchunguzi huo unakosa msingi halali wa kikatiba, usawa ama pia suala muhimu la ulinzi katika harakati hiyo, Ikulu hiyo haiwezi kutarajiwa kushiriki katika uchunguzi huo. Kulingana na afisa mmoja mkuu, hii inamaanisha kuwa hakuna mashahidi wa ziada watakaoruhusiwa kufika mbele ya bunge ama kuzingatia matakwa ya nyaraka hizo.

Ikulu ya White House inapinga kuwa bunge hilo halijapiga kura kuanzisha uchunguzi wa kumng'atua mamlakani rais Donald Trump. Pia imedai kuwa haki ya Trump inakiukwa. Hata hivyo mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu ujasusi Adam Schiff ameandika ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter katika kujibu na kusema hatua ya Trump ya kukataa kushiriki katika uchunguzi huo inaashiria kuwa , '' Rais ni mkuu kuliko sheria.''

Gordon Sondland

Gordon Sondland, balozi wa Marekani katika Umoja wa Ulaya.

Barua hiyo imetolewa siku moja ambapo Trump ameimarisha vita vyake dhidi ya bunge la nchi hiyo kwa kumzuia Balozi wa  Marekani katika Umoja wa Ulaya Gordon Sondland kutoa ushahidi faraghani kuhusiana na shughuli za rais huyo na Ukraine. Adam Schiff ameitaja hatua hiyo ya kumzuia balozi Sondland kuongeza, ''ushahidi muhimu'' kuwa kizuizi kwa bunge hatua inayotekelezwa na rais Trump na waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo Mike Pompeo ambayo itaimarisha kesi ya chama cha democratic.

Spika wa bunge la Marekani Nancy Pelosi amesisitiza kuwa bunge limezingatia sheria kuangazia utendakazi wa rais na serikali yake chini ya katiba hata kwa kukosekana kwa  kura rasmi ya uchunguzi wa Kumng'atua rais mamlakani. Katika taarifa hapo jana usiku, spika huyo amesema kuwa rais sheria ni kuu kuliko rais na kwamba atawajibikia makosa yake.

Katiba ya nchi hiyo inasema kuwa bunge lina mamlaka ya kumng'atua rais mamlakani na kwamba bunge la seneti lina uwezo wa kipekee wa hatua ya kuandaa kesi ya ung'atuzi. Katiba inasema kuwa rais anaweza Kung'atuliwa kwa makosa ya uhaini, hongo ama uhalifu mwingine wowote mkubwa, iwapo kutakuwa na uungwaji mkono wa thuluthi mbili za kura kutoka kwa bunge la seneti. Lakini pia inatoa mwelekeo zaidi mbali na hayo kulingana na kesi hiyo.