IESE-Barcelona:Shule ya Biashara ya tabaka ya juu | Habari za Ulimwengu | DW | 06.11.2006
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

IESE-Barcelona:Shule ya Biashara ya tabaka ya juu

Kwa mujibu wa majarida mashuhuri ya kiuchumi kama “Wall Street Journal” au “Economist”,Taasisi ya wasomi wa tabaka ya juu iliyo Barcelona nchini Hispania-kwa ufupi IESE-ni mojawapo ya shule ya biashara iliyo bora kabisa duniani.

Barani Ulaya,shule ya biashara ya Barcelona ipo katika kundi moja na Shule ya Biashara ya London au Taasisi ya Kimataifa ya Uendeshaji wa Biashara mjini Lausanne.Maprofesa wa shule hiyo ya biashara wanatoka kila pembe ya dunia na husomesha sehemu mbali mbali za ulimwengu.Iwe Shule ya Biashara ya Harvard au kwenye Chuo Kikuu cha Stanford au hata katika Shule ya Kimataifa ya Biashara ya Ulaya nchini China.Wanafunzi huonyesha vipaji vyao na hamu ya kutaka kupata mafanikio.Kimsingi,Kingereza ni lugha inayotumiwa katika masomo yanayotolewa kwenye vyumba vya kisasa kabisa vya shule hiyo ya Barcelona,lakini masomo mengine hufundishwa pia kwa lugha ya Kihispania.Masomo hutolewa kwa kutumia mifano halisi.Profesa Marc Sachon wa shule ya biashara ya Barcelona-IESE anaeleza hivi:

“Tunatoa mafunzo ya uendeshaji wa biashara kwa Kingereza na vile vile kwa lugha ya Hispania.Na katika makundi hayo mawili kuna tabaka mbali mbali:yaani tabaka ya kati,ya juu kidogo na ya juu zaidi.Halafu kuna mipango miwili tofauti: Katika mpango mmoja,yeyote anaetaka anaweza kujiandikisha na wa pili ni kwa ajili ya makampuni kama vile Boeing,Henkel na kadhalika.”

Masomo yanayotolewa katika makundi madogo yanachangamsha.Daima kuna masuala yanayohusika na vitendo.Maprofesa wa shule ya Barcelona-IESE husomesha kwa kutumia mifano halisi.Kila siku mifano halisi mbali mbali huchunguzwa na kila mwanafunzi mmoja na hushauriana pia na wenzake.Baadae ndio profesa huijadili kesi hiyo pamoja na wanafunzi kutafuta njia ya kutenzua tatizo linalochunguzwa siku hiyo.

Kwa maoni ya mwanafunzi Madhur Srivastava anaetoka New Delhi nchini India,utaratibu wa kujifunza ni tofauti kabisa na mtu hujifunza zaidi katika shule hiyo.Hata msomi Dr.Edward Mungai kutoka Kenya anamuunga mkono.Anasema,mtu anapojishughulisha kuchambua kesi fulani,bila shaka utaratibu huo baadae pia utakuwa na manufaa katika maamuzi ya kibiashara.Hayo yote huvutia sana.

Edward Mungai atakapomaliza masomo yake,anataka kurejea Nairobi.Anasema,huu ni mwaka wake wa nne na anahitaji mwaka mmoja mwingine kuhitimisha masomo na kupata shahada yake.Halafu anataka kurudi Kenya kufanya kazi kama profesa katika shule ya uchumi mjini Nairobi.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com