1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya waliojeruhiwa Jerusalem kufuatia vurugu yapita 300

John Juma
10 Mei 2021

Makabiliano kati ya vikosi vya usalama vya Israel na Wapalestina mjini Jerusalem yameendelea huku idadi ya waliojeruhiwa ikipindukia watu 300.

https://p.dw.com/p/3tCv0
TABLEAU | Israel Jerusalem | Spannungen & Gewalt
Picha: Ahmad Gharabli/AFP/Getty Images

Shirika la Hilal Nyekundu la Palestina limesema zaidi ya Wapalestina 305 wamejeruhiwa, wakiwemo 228 waliopelekwa hospitalini. Saba miongoni mwa waliojeruhiwa wako katika hali mbaya/mahututi.

Polisi ya Israel imesema maafisa wake 21 pia wamejeruhiwa wakiwemo watatu ambao wamelazwa hospitalini. Kulingana na maafisa wa huduma za dharura za afya wa Israel, raia saba wa Israel pia wamejeruhiwa.

Maafisa wa polisi wa Israel walifyatua gesi ya kutoa machozi, risasi za mipira na mabomu ya kushtua dhidi ya Wapalestina waliowarushia mawe katika eneo la tatu kwa utakatifu miongoni mwa Waislamu lakini ambalo linakumbwa na machafuko mjini Jerusalem.

Machafuko hayo yakiwa ya hivi karibuni zaidi kuhusu misururu ya makabiliano yanayotishia kutanuka na kuwa mabaya zaidi.

Hali ikiendelea kuwa tete Jerusalem, zaidi ya mabomu kumi ya gesi za kutoa machozi mapoja na maguruneti yalirushwa ndani ya msikiti wa Al-Aqsa, ambalo ni miongoni mwa maeneo takatifu zaidi kwa Waislamu. Hayo ni kulingana na mpiga picha mmoja wa shirika la habari la Associated Press aliyeko katika eneo la mkasa.

Moshi ulionekana ukitanda mbele ya msikiti huo huku mawe na vitu vingine vikitapakaa kila mahali.

Jumuiya ya kimataifa imetoa wito wa kurejeshwa utulivu Jerusalem, mnamo wakati vurugu hizo zinatishia kutanuka na kuwa mbaya zaidi.
Jumuiya ya kimataifa imetoa wito wa kurejeshwa utulivu Jerusalem, mnamo wakati vurugu hizo zinatishia kutanuka na kuwa mbaya zaidi.Picha: Mahmoud Illean/AP Photo/picture alliance

Mvutano wa kudhibiti wilaya ya Sheikh Jarrah

Makabiliano hayo ndiyo ya hivi karibuni baada ya wiki kadhaa za mivutano kati ya Wapalestina na vikosi vya usalama vya Israel katika Mji wa Kale wa Jerusalem ambao ni kitovu cha mzozo.

Kumekuwa na makabiliano ya karibu kila usiku eneo hilo tangu mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Katiku siku za hivi karibuni, vurugu zilichochewa na mpango wa kuwaondoa makumi ya Wapalestina kutoka wilaya ya Sheikh Jarrah mashariki mwa Jerusalem, ambako walowezi wa Kiyahudi wamekuwa wakipambana na Wapalestina kisheria wakitaka kuchukua sehemu hiyo.

Taharuki ilitarajiwa kutanda zaidi leo Jumatatu mnamo wakati Israel inaadhimisha siku waliyokamata na kuchukua udhibiti wa mji wa Jerusalem mnamo mwaka 1967 baada ya vita vilivyodumu kwa siku sita. Siku yenyewe huita ‘Siku ya Jerusalem'.

Jeshi la Israel laahirisha luteka kushughulikia ghasia

Jeshi la Israel limeahirisha luteka yake kubwa zaidi katika miaka 30 ili kuelekeza nguvu katika kutuliza vurugu zaidi zinazoweza kutokea Jerusalem.
Jeshi la Israel limeahirisha luteka yake kubwa zaidi katika miaka 30 ili kuelekeza nguvu katika kutuliza vurugu zaidi zinazoweza kutokea Jerusalem.Picha: Said Khatib/AFP/Getty Images

Jeshi la Israel limesema linaahirisha luteka yake kubwa iliyopaswa kuanza leo ili kushughulikia uwezekano wa kutokea machafuko zaidi mjini Jerusalem.

Kupitia taarifa, mkuu wa majeshi ya Israel Luteni Jenerali Aviv Kohavi amesema wameahirisha luteka hiyo ambayo ni kubwa zaidi kuwahi fanyika katika miaka 30 iliyopita na badala yake wanaelekeza nguvu zao zote kukabili vurugu zitakazotokea.

Israel pia imekuwa ikiongeza walinda usalama wake katika eneo la makaazi ya Wayahudi ya Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza ambako wanamgambo wamekuwa wakirusha makombora kuelekea kusini mwa Israel tangu Jumapili.

Jumuiya ya kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa, kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis wametaka utulivu kurejeshwa Jerusalem.

Hayo yakijiri, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linajiandaa kufanya kikao cha dharura leo kujadili hali ya machafuko yanayozidi kuongezeka. Hayo ni kulingana na gazeti la Times la Israel ambalo limewanukuu wanadiplomasia.

(APE,RTRE,DPAE)