1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yaruhusu uchunguzi Afghanistan

Lilian Mtono
5 Machi 2020

Majaji katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC ya mjini The Hague, wameamua hii leo kufanyika uchunguzi wa madai dhidi ya udhalimu uliofanywa wakati wa vita nchini Afghanistan.

https://p.dw.com/p/3Yv1b
Niederlande Chefanklägerin beim Internationalen Strafgerichtshof in Den Haag | Fatou Bensouda
Picha: Getty Images/AFP/E. Plevier

Maamuzi hayo pia yanajumuisha kuangazia uwezekano wa uhalifu mbaya kabisa uliofanywa na wanajeshi wa Marekani. Uamuzi huu unapindua ule uliofikiwa awali.

Jaji Piotr Hofmanski miongoni mwa jopo la majaji, amesema kwenye uamuzi huo kwamba "Katika mazingira kama haya na kwa faida ya usimamizi wa shughuli na mfumo wa kimahakama na majaji wa rufaa wanaona inafaa kurekebisha uamuzi huo na kuidhinisha uchunguzi kwa msingi wa matokeo ya hapo awali kwenye kesi ya awali."

Ni jaji Piotr Hofmanski wa mahakama ya ICC wakati walipokuwa wakitoa maamuzi hayo hii leo.

Huo ni uamuzi wa kwanza kutolewa na majaji wa mahakama hiyo unaomruhusu mwendesha mashitaka wa ICC kuwachunguza wanajeshi wa Marekani. Washington kwa muda mrefu imekuwa ikipingana vikali na uamuzi huo wa kimahakama na kukataa katakata kutoa ushirikiano. Afghanistan pia inapinga uamuzi huo.

Mwaka 2018, aliyekuwa mshauri wa masuala ya usalama nchini Marekani, John Bolton alisema mahakama hiyo iliyoanzishwa mwaka 2002 kuchunguza uhalifu mbaya kabisa unaotokea kote ulimwenguni inatishia uhuru wa Marekani pamoja na maslahi ya kiusalama ya taifa hilo".

Afghanistan 2017 | Operation Resolute Support | US-Armee
Wanajeshi wa Marekani waliokuwa nchini Afghanistan, kama picha ilivyochukuliwa mwaka 2017. Picha: picture-alliance/AP Photo/Operation Resolute Support Headquarters/Sgt. Justin T. Updegraff

Ingawa uchunguzi huo sasa umeruhusiwa, bado inasubiriwa kuona iwapo mtuhumiwa yoyote ambaye kwa namna moja ama nyingine ametajwa na mwendesha mashitaka kuhusika na madai hayo atapanda kizimbani. 

Makundi ya haki za binadamu yasifu uamuzi huo.

Makundi ya haki za binadamu yamesifu uamuzi huo wa ICC. Mkurugenzi wa masuala ya haki za kimataifa kwenye shirika la kimataifa la haki za binaadamu la Human Rights Watch Param-Preet Singh amesema uamuzi huo wa kuruhusu uchunguzi wa uhalifu mbaya nchini Afghanistan licha ya shinikizo kubwa dhidi ya uhuru wa mahakama unathibitisha jukumu muhimu la mahakama kwa wahanga, wakati milango mingine ya haki ikiwa imefungwa."

Soma zaidi: Sasa ICC yaiandama Marekani

Uamuzi huo uliotolewa siku chache baada ya Marekani kukubali kuwaondoa wanajeshi wake katika mzozo wa Afghanistan uliodumu kwa muda mrefu, kufuatia kutiliana saini makubaliano ya amani kati yake na Taliban, unabatilisha uamuzi wa awali wa mahakama ya chini na kufungua njia kwa mwendesha mashitaka mkuu Fatou Bensouda kuanzisha uchunguzi kamili, licha ya upinzani huo wa Marekani.

Afghanistan ni mwanachama wa mahakama hiyo ya mjini The Hague. Marekani si mwanachama wa ICC na tayari rais Donald Trump amewawekea vikwazo vya kusafiri na vinginevyo watumishi wa ICC mwaka mmoja uliopita.

Jopo la majaji waliosikiliza hoja za awali mwaka jana, walikataa ombi la Bensouda la kuanzisha uchunguzi alilolitoa mwezi Novemba 2017. Kwenye ombi hilo alisema kuna taarifa kwamba wanajeshi wa Marekani na idara za kijasusi waliwatesa watu, kuwatendea ukatili dhidi ya utu wao, kuwabaka na ukatili wa kijinsia dhidi ya wafungwa waliohusishwa na mzozo huo nchini Afghanistan na maeneo mengine, hasa kati ya mwaka 2003-2004.

Mashirika: AFPE, APE