1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yagusa siasa za Kenya

7 Aprili 2011

Wakati Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, ikiangalia uwezekano wa mashtaka dhidi ya wanasiasa sita wa Kenya wanaoshukiwa kushiriki machafuko ya 2007, tayari serikali ya mseto nchini humo imegawika juu ya hatua hii.

https://p.dw.com/p/10pGA
Rais Mwai Kibaki wa Kenya akila kiapo mwaka 2007
Rais Mwai Kibaki wa Kenya akila kiapo mwaka 2007Picha: AP

Umesalia mwaka mmoja tu kabla ya uchaguzi mkuu wa Kenya. Uchunguzi unfanyawa leo The Hague dhidi ya washukiwa wa machafuko ya uchaguzi mkuu uliopita, wengi wao ni wanasiasa kwenye serikali ya sasa. Bila ya shaka sura ya kisiasa nchini Kenya itabadilika.

Watu sita ambao huenda wakapanda kizimbani, ni pamoja na wanasiasa watatu wa ngazi ya juu katika baraza la Mawaziri la Rais Mwai Kibaki: katibu mkuu kiongozi, Balozi Francis Muthaura, waziri wa fedha Uhuru Kenyatta, na aliyekuwa waziri wa viwanda, Henry Kosgey.

Mchakato uliowafikisha wanasiasa hawa ICC umeiacha serikali ya mseto wa vyama vya PNU-ODM ikiwa imepata pigo vibaya kwa mgawanyiko.

PNU na kesi za The Hague

Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga wakiweka saini makubaliano ya kuunda serikali ya pamoja
Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga wakiweka saini makubaliano ya kuunda serikali ya pamojaPicha: picture-alliance/ dpa

Upande wa PNU, unaoongozwa na Rais Mwai Kibaki, unapinga kesi hizi kwa msingi kwamba watuhumiwa wamepatikana kibaguzi.

"Msimamo wetu ni kwamba, mashitaka haya hayafanyiki kwa waliohusika wenyewe, bali tunaona sheria ya kuchukuwa wale wasiohusika na kuacha waliohusika." Anasema mnadhimu wa PNU bungeni, Johnston Muthama.

Kwa msingi huu, hata baada ya kuwa mwanzoni alisema kwamba serikali yake ingelishirikiana kikamilifu na ICC, Rais Kibaki alimtuma pia makamo wake, Kalonzo Musyoka, katika mwezi Machi, kufanya ziara jijini New York na Addis Ababa, kutafuta uungwaji mkono wa kimataifa ili kuzuia mchakato wa kisheria wa ICC. Hoja ya PNU ni kuwa kupelekwa kwa kesi hizi ICC, kutachochea vurugu zaidi.

Upande wa ODM

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Fedha wa Kenya, Uhuru Kenyatta
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Fedha wa Kenya, Uhuru KenyattaPicha: AP

Hata hivyo, madai haya yanapingwa na baadhi ya wanaharakati wa haki za binaadamu na sheria, kama Dokta Ekuru Oukot, ambaye ni mwanasheria wa katiba nchini Kenya.

“Sidhani ikiwa Wakenya ni wapumbavu kiasi hicho. Watu hawa sita hawawezi kutumika kama hoja ya kwamba eti nchi itaporomoka wakishitakiwa. Sioni hivyo. Badala yake nikiongea na watu mitaani wanasema waache waende, kwababu tunajaribu kujenga utawala wa sheria." Anasema Dkt. Oukot.

Sehemu kubwa ya wajumbe wa ODM wanataka kesi hizi zifanyike. Mwezi uliopita, wabunge wa chama hicho kutoka Bonde la Ufa, ambako sehemu kubwa ya mauaji ilifanyika, walitishia kuitisha kura ya maoni kuzuia uchaguzi wa mwakani, ikiwa kesi hazikuendeshwa sasa huko The Hague.

Lakini wenyewe washukiwa, wanasema hawakufanya kosa lolote na hakuna litakalowapata. Mmoja wao, Uhuru Kenyatta, anasema kwamba anakwenda The Hague kusafisha jina lake na hakuna kitakachobadilika.

“Sifikiri kuwa hili litakuwa na athari kubwa. Tunaendelea kufanya kazi hapa, kazi itaendelea, Kenya itaendelea, uchumi utaendelea. Kwa upande anagu, halina athari yoyote ile." Anasema Uhuru Kenyatta.

Mapema mwezi uliopita, Ocampo, mwendeshaji mashtaka wa mahakama hiyo yaThe Hague alitaka baadhi ya washukiwa wavuliwe vyeo vyao ili kupisha uchunguzi; akiwataja Balozi Muthaira, ambaye Idara ya Usalama ya Kenya iko chini yake, na naibu waziri mkuu, Uhuru Kenyatta, lakini hadi leo kesi zinaanza, hakuna aliyejiuzulu.

Ingawa Ocampo anajiamini hakuna litakalouzuwia mchakato huu wa kisheria unaoanza leo, lakini hali halisi nchini Kenya ni tafauti. Siasa za ukabila zinaonekana kugongana na siasa za ICC, na matokeo yake yanaweza yasiwe mazuri kwa siasa za kustahamiliana, haki na upatanisho.

Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Othman Miraji