1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yaamuru wanajeshi watoto Congo walipwe dola 10 milioni

Florence Majani15 Desemba 2017

Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita, (ICC)  imetoa uamuzi kwa wanajeshi watoto wa zamani, kulipwa fidia ya kihistoria ya dola milioni 10 baada ya kuingizwa katika makundi ya wapiganaji ya Congo. 

https://p.dw.com/p/2pRi1
Niederlande Kongo Menschenrechte Urteil Thomas Lubanga
Mbabe wa Kivita, Thomas Lubanga, akiwa katika mahakama ya ICC Agosti 2011.Picha: dapd

Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita, (ICC)  imetoa uamuzi kwa wanajeshi watoto wa zamani, kulipwa fidia ya kihistoria ya dola milioni 10, kutokana na mazingira ya kikatili waliyopitia baada ya kuingizwa katika makundi ya wapiganaji ya Congo. 

Mbabe wa Vita Thomas Lubanga, alifungwa miaka 14 jela baada ya kukutwa na hatia mwaka 2012 na mahakama hiyo ya ICC kwa kuwaingiza vijana wadogo wa kike  kwa wa kiume, katika kikosi cha wanamgambo kinachofahamika kama Umoja wa Wazalendo wa Congo,(UPC). Ni katika eneo la Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Majaji wamesema Lubanga  pia anastahili kulipa fidia hiyo kutokana na madai ya  waathirika 425 waliotambuliwa na mahakama na ambao wakati wa uhalifu huo, kati ya mwaka 2002 na 2003, wote walikuwa na umri wa chini ya miaka 15.

Lakini walisisitiza kuwa, mamia au hata maelfu ya waathirika watakaoongezwa, waliathirika katika mikono ya wanamgambo wa Lubanga. Kila mhanga katika wahanga hao 425,  atalipwa kiasi cha dola 8000 kila mmoja,  kutoka katika jumla ya dola 3.4 milioni. Alisisitiza Jaji Marc Perrin de Brichambaut.

Kadhalika majaji hao waliamuru dola 6.6 milioni za ziada, kuwasaidia wengine ambao watajitokeza. Fidia hiyo ni ya pamoja, hivyo, itatumika katika miradi kuwasaidia wahanga hao.

Hata hivyo swali lililoibuka ni  hili,  ni kwa  namna gani thamani ya utoto uliopotea katika ukungu wa vurugu, kumwagika kwa damu na machafuko, itakokotolewa? Muda umepita na waathirika walio wengi wapo katika miaka ya 30 na wana watoto wao.

´´Unakokotoa vipi ujana uliopotea? Kipi kina thamani? Milioni, nusu milioni, euro elfu tano au euro elfu moja? Wakili Luc Walleyn, aliiiuliza katika mahakama, ya The Hague, katika shauri hilo, mwaka 2016.

Kongo 2003 Rebellen UPC
Mmoja wa wanajeshi wa watoto aliyekuwa amejiunga na UPC. Picha ya Maktaba mwaka 2003.Picha: AP

Walikuwepo wanajeshi watoto wa kike

Pamoja na mambo mengine, wasichana wengi waliolazimishwa kuingia katika jeshi, waligeuka watumwa wa kingono na wakarudi nyumbani wakiwa na watoto. Fidia hiyo,  ambayo ni sawa na euro 8.5 milioni, itasimimiwa na mfuko wa waathirika, ambao tayari umeshatenga euro milioni moja, katika kesi ya Lubanga.

Imeanzisha mpango wa miaka mitatu, kwa ajili ya miradi ya kuwasaidia wahanga hao wa vita,  ikiwamo, kiafya, matibabu ya kisaikolojia, elimu na mafunzo ya ufundi.

Taasisi isiyo ya kiserikali, ya Wanajeshi watoto wa Kimataifa, ambayo inafanya kazi ya kuzuia watoto wasitumike katika migogoro, imesema kuwa wasichana waliohojiwa nchini Congo, wameelezea madhila ikiwamo ukiwa na kutishiwa kifo.

Hata hivyo, Lubanda ambaye anatumikia kifungo chake Congo, anaweza kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo. Mwanasheria wake, Jean-Marie, Biju-Duval, alisisitiza katika shauri la Oktoba 2016 kuwa mteja wake hatakiwi kulipa chochote.

Lubanga ni mtu wa tatu, ambaye Mahakama ya ICC imeamua alipe fidia. Machi mwaka huu, majaji waliamuru dola 250 zilipwe kwa kila muathirika kati ya  waathirika 297 wa vita katika kesi dhidi ya mbabe wa vita, Germain Katanga.

 Mwandishi: Florence Majani(AFP)

Mhariri: Saumu Yusuf