1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IAEA yamchagua kiongozi mpya.El Baradei amaliza muhula wake wa 3

Thelma Mwadzaya26 Machi 2009

Wanachama 35 wa baraza la uongozi wa Shirika la Atomiki IAEA wanapiga kura hii leo kumchagua mrithi wa kiongozi anayeondoka Mohamed El Baradei.Kimsingi muhula wake wa tatu unakamilika mwishoni mwa mwezi Novemba

https://p.dw.com/p/HJrj
Kiongozi anayeondoka wa IAEA Mohamed El BaradeiPicha: picture-alliance/ dpa


Shirika la IAEA lililo na makao yake makuu mjini Vienna nchini Austria lina jumla ya wafanyakazi 2200 kutoka mataifa 90.

Mpaka sasa wagombea wawili wametangaza azma yao ya kutaka kuwania wadhifa huo.Yukiya Amano aliye na umri wa miaka 62 ni mwakilishi wa Japan na balozi katika Shirika la IAEA.Abdul Minty aliye na umri wa miaka 62 aliyepia naibu mkurugenzi mkuu wa Idara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini amekuwa akishikilia nafasi ya mjumbe wa Afrika Kusini katika shirika hilo tangu mwaka 1995.


Amano anaripotiwa kuwa na ushawishi mkubwa japo ushindi wake si wa moja kwa moja. Mrithi wa El Baradei anatarajiwa kuanza kutekeleza majukumu yake ifikapo mwishoni mwa mwezi Novemba.

Mohamed El Baradei alianza kutambulika mwaka 2002 pale uchunguzi uliofanyika nchini Iraq aliousimamia ulipotoa maelezo yaliyotofautiana na kauli za uongozi wa rais wa zamani wa Marekani George W Bush zilizosisitiza kuwa Iraq ina mradi wa kutengeza silaha za nuklia. Hali hiyo ilizua sintofahamu.

Shirika la Kimataifa la Atomiki IAEA lilizinduliwa mwaka 1957 kutokana na msukumo wa Marekani.Sababu ya msingi ya hatua hiyo ilikuwa ueneaji wa silaha za nuklia kote ulimwenguni. Majukumu yake yana hadhi maalum na yanajumuisha masuala ya sayansi na teknolojia katika mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa. Mamlaka ya IAEA inahusika na udhibiti wa matumizi ya nuklia kwa ajili ya nishati vilevile uratibu wa ushirikiano wa kimataifa pamoja na matumizi ya kijeshi ya teknlojia ya nuklia. Kadhalika shirika la IAEA linahusika na usimamizi wa utekelezaji wa makubaliano ya mwaka 1970 ya kuzuia ueneaji wa matumizi ya nuklia hususan kuunga mkono juhudi za matumizi salama ya nishati.

Hasahasa Shirika la IAEA limeandaa miradi maalum iliyo na lengo la kuimarisha viwanda vya nuklia pamoja na kuhakikisha kuwa nchi wanachama wanatimiza vigezo vya kimataifa vilivyowekwa.Moja ya majukumu hayo ni kuzuia matumizi mabaya ya bidhaa za nuklia kwa mfano kuzisambaza bila ya idhini. Mbali na hilo IAEA linasimamia matumizi ya bidhaa za nuklia katika vivanda kama ilivyoafikiwa na nchi wanachama.Hii ndiyo njia pekee itakayohakikisha kuwa vifaa vinavyotumiwa kutengezea nishati ya nuklia viko salama.


Shirika hilo lililo na makao makuu mjini Vienna nchini Austria linawajibika kulitaarifu Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu shughuli zake na inapohitajika kuliarifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa endapo kunatokea kitisho cha aina yoyote.Baraza la uongozi la Shirika la IAEA linawajibika kukutana mara tano kwa mwaka.Baraza lake kuu hukutana mara moja kwa mwaka na linawaleta pamoja wawakilishi kutoka nchi 144 wanachama.

Mwandishi:Sonila Sands ZPR / Mwadzaya

Mhariri:Saumu Mwasimba