1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IAAF yasema ripoti hiyo haikuwa na chochote kipya

17 Agosti 2015

Shirikisho la kimataifa la riadha – IAAF lilizuia kuchapishwa ripoti ambayo ilionyesha kuwa zaidi ya thuluthi ya wanariadha maarufu duniani walikiri kutumia mbinu za kuongeza nguvu mwilini

https://p.dw.com/p/1GGrH
Rais anayeondoka wa IAAF Lamine Diack
Rais anayeondoka wa IAAF Lamine DiackPicha: picture-alliance/empics

Waandishi wa ripoti hiyo wameliambia gazeti la Uingereza la Sunday Times kuwa IAAF ilizuia uchapishaji wa utafiti huo uliofanywa miaka minne iliyopita. Hata hivyo IAAF ilijibu kwa kusema kuwa hakuna chochote kipya kuhusu ufichuzi huo.

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Tuebingen nchini Ujerumani walizungumza na wanariadha mahiri katika mashindano ya dunia ya 2011 mjini Daegu, Korea Kusini na kusema katika utafiti wao kuwa kati ya asilimia 29 na 34 ya washindani 1,800 katika mashindano hayo walikuwa wamekiuka sheria za kupambana na dawa za kuongeza nguvu mwilini katika kipindi cha miezi 12 iliyotangulia. IAAF imesema haikuwahi kuzuia uchapishwaji wa ripoti hiyo, ikiongeza hata hivyo kuwa ilikuwa na mashaka kuhusiana na ufafanuzi wa matokeo yaliyotolewa na kikundi cha utafiti kama ilivyothibitishwa na watalaamu wa ngazi ya juu katika sayansi ya kijamii ambao waliitathmini ripoti hiyo kufuatia ombi la Ia IAAF.

Rais wa IAAF Lamine Diack anakamilisha uongozi wake na nafasi yake kuchukuliwa na bingwa wa zamani wa mbio za wastani Sebastian Coe au bingwa wa zamani wa Olimpiki wa kuruka kwa mlingoti Sergey Bubka kupitia uchaguzi utakaofanyika wiki hii kabla ya kuanza mashindano ya Beijing.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga