1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huu si wakati wa kupigia debe sera za chama

P.Martin - (DPA)10 Machi 2009

Athari za mzozo wa fedha,mvutano katika chama cha Kansela Merkel na shida za familia masikini na watoto wao ni mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo siku ya Jumanne.

https://p.dw.com/p/H92B

Tukianza na gazeti la PFORZHEIMER ZEITUNG linasema:

"Mtu asishangazwe na onyo lililotolewa na shirika la kuwahifadhi watoto kuwa wazazi wanapokabiliwa na wakati mgumu ni dhahiri kuwa watoto pia hupata shida.Hilo si jipya lakini ni bora kukumbushwa.Kwani katika midahalo ya hivi sasa watoto wanatumiwa kama njia mojawapo ya kufufua uchumi- familia hulipwa Euro 100 kwa kila mtoto.Hiyo hudhihirisha vipi wanasiasa wanashindwa kuelewa matatizo yanayokabiliwa na familia masikini."

Na gazeti la HAMBURGER ABENDBLATT likiendelea na mada hiyo linasema:

"Wazazi na watoto hunufaika zaidi kwa pato linalotokana na ajira kuliko misaada inayotolewa na serikali.Kwa hivyo kilicho muhimu na kinachohitajiwa zaidi ni miradi ya kuzalisha nafasi za kazi badala ya kuzindua mifumo mipya ya misaada mara kwa mara."

Mzozo wa fedha na uchumi ukiendelea kuutikisa ulimwengu mzima, gazeti la WETZLARER NEUE ZEITUNG limeandika:

"Ukweli kuwa hata makampuni madogo na ya wastani sasa yataathirika vibaya kutokana na mzozo wa fedha wala usizushe wasiwasi mkubwa.Kwani mifumo ya makampuni kama hayo ni tofauti kabisa-kampuni moja likiathirika haimaanishi kuwa makampuni mengine pia yatafuata mkondo huo huo.Kwa sehemu kubwa,makampuni madogo na ya wastani yataweza kustahmili kipindi hiki kigumu kuliko baadhi ya makampuni makubwa."

Mada nyingine inayoendelea kuchomoza katika magazeti ya Ujerumani inahusika na Kansela Angela Merkel anaetuhumiwa na wanachama wa ngazi ya juu katika chama chake cha CDU kuwa hana msimamo baina na kumuonya kuwa anapoteza umaarufu wake miongoni mwa wapiga kura.Lakini gazeti la FRÄNKISCHER TAG linasema:

"Kwa hivi sasa maelfu ya watu wakikabiliwa na kitisho cha kupoteza nafasi zao za ajira,chama cha CDU kinapaswa kutafuta njia ya kuokoa nafasi hizo za kazi badala ya kuzingatia maslahi ya chama."

Kwa maoni ya gazeti la LANDESZEITUNG LÜNEBURG, mvutano huo umezushwa na hofu za kukimbiwa na wapiga kura katika uchaguzi ujao. Likiendelea linaeleza hivi:

"Wengi wa Wajerumani wanahisi kuwa si kiongozi tu bali hata wanasiasa hawatekelezi wajibu wao ipasavyo.Huu si wakati wa kutanguliza sera za chama katika kupitisha maamuzi muhimu ya kisiasa.Badala yake viongozi wanapaswa kuwajibika katika kuamua kile kilicho sahihi au la."