1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CCM yamuidhinisha Hussein Mwinyi kuwania urais Zanzibar

10 Julai 2020

Halmashauri Kuu ya chama tawala nchini Tanzania, CCM imemchagua waziri wa Ulinzi wa muda mrefu nchini humo Hussein Ali Mwinyi kuwa mgombea wake wa kiti cha urais wa visiwa vya Zanzibar.

https://p.dw.com/p/3f7sr
Tansania Sansibar| Hussein Ali Mwinyi
Hussein Ali MwinyiPicha: DW/Said Khamis

Gazeti la kila siku la The Citizen limearifu kuwa Dkt Mwinyi ameibuka mshindi baada ya kupata asilimia 78 ya kura za wajumbe wa kikao cha Halmshauri Kuu na kuwapiku makada wengine watatu wa chama hicho akiwemo waziri kiongozi wa zamani wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Shamsi Vuai Nahodha.

Wakati wa kikao hicho kilichofanyika mjini Dodoma na kuongozwa na mwenyekiti Chama cha Mapinduzi ambaye pia ni rais wa sasa wa Tanzania, John Magufuli, Mwinyi alipata kura 129, huku Nahodha akiambulia kura 19 na mgombea mwingine asiyefahamika sana Khalid Mohamed naye alipata kura 19.

Hussein Mwinyi ambaye ni mtoto wa rais wa zamani wa Tanzania na wa visiwa vya Zanzibar Ali Hassan Mwinyi ametoa wito wa kuwepo mshikamano chamani kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba ambao kihistoria upande wa Zanzibar huandamwa na upinzani mkali pamoja na vurugu.

Walioshindwa waahidi kumuunga mkono 

Wagombea wengine walioshindwa wametoa aahdi ya kuunganisha nguvu ili kumwezesha Mwinyi kuchaguliwa kuwa rais awamu ya nane ya visiwa vya Zanzibar

Tansania Bashiru Ali (L) und Präsident John Pombe Magufuli
Picha: State House Tanzania

Katika hatua nyingine kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM pia kimemuidhinisha rais John Magufuli kuwa wa kiti cha urais wa Tanzania na jina lake litapelekwa mbele ya mkutano mkuu wa chama unaofanyika kwa siku mbili kuanzia kesho Jumamosi.

Rais Magufuli ambaye anawania muhula wa pili madarakani amekuwa mwanachama pekee wa CCM aliyechukua fomu za kuwania kiti cha urais mwaka 2020.

Katika hatua nyingine, na kama inavyotazamwa na wengi kama njia ya kusaka umoja kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, chama hicho leo kimemsamehe aliyekuwa katibu wake mkuu, Abdulrahman Kinana aliyekuwa amepewa adhabu kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu.

Kinana amealikwa kuhudhuria mkutano huo unaanza kesho na kumalizika siku ya Jumapili,

Chama hicho kimeendelea kumfungia milango, mwanasiasa wake, Bernard Membe aliyekuwa waziri wa mambo ya kigeni katika serikali iliyopita. Hata hivyo, Membe ameachana na chama hicho na sasa amekuwa katika majadiliano na chama kimoja cha upinzani kwa shabaha ya kuwania urais.

Hadi sasa bado haijafahamika mara moja kama katika uchaguzi mwa mwaka huu upinzani utafanikiwa kuweka mgombea mmoja au la.

Wanasiasa kadhaa wa chama kikuu cha upinzani Chadema wameshaji tokeza kuchukua fomu za kuwania urais.