Human Rights Watch yataka Sudan iwajibishwe | Matukio ya Afrika | DW | 23.09.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Human Rights Watch yataka Sudan iwajibishwe

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema baraza la kutetea haki za binadamu la Umoja wa mataifa linapaswa kuiwajibisha Sudan kuhusu vifo vya mamia ya waandamanaji waliouawa na askari

Askari waliwafyatulia risasi mamia ya waandamanaji waliokuwa wakifanya maandamano ya amani tarehe 23 mwezi Septemba mwaka jana kufuatia hotuba iliyokuwa imetolewa na Rais Omar al Bashir ya kusitisha ruzuku ya mafuta.

Baraza la kutetea haki za binadamu la Umoja wa Mataifa litafanya kikao hii leo kuijadili Sudan mjini Geneva na inatarajiwa kutangaza azimio kuhusu hali nchini humo baadaye wiki hii.

Uchunguzi huru na wazi unahitajika

Shirika la Human Rights Watch linataka baraza hilo la umoja wa Mataifa kulaani mauaji ya waandamanaji na madhila mengine yaliyofanywa Sudan na kuishinikiza serikali kuruhusu uchunguzi huru na wa wazi kuhusu kisa hicho cha mwaka jana ili kutoa fursa kwa waliohusika kufunguliwa mashitaka.

Afisa wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch Philippe Dam

Afisa wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch Philippe Dam

Afisa wa shirika la Human Rights Philippe Adam amesema iwapo Sudan itachelewesha uchunguzi,basi baraza la kutetea haki za binadamu linapaswa kuhimiza asasi ya kimataifa kama Umoja wa Afrika kuingilia kati.

Katika utafiti uliofanywa mapema mwaka huu,Human Rights Watch walipata ushahidi kuwa maafisa wa usalama waliuawa kiasi ya watu 170 kwa kuwapiga risasi wakiwemo watoto,kuwajeruhi,kuwakamata na kuwazuia mamia ya wengine.

Maafisa waliwazuia waandamanaji kadhaa,wanaharakati wa kisiasa na wanahabari kwa muda mrefu bila ya kuwafungulia mashitaka au kuruhusu kuwakilishwa na mawakili au kutembelewa na jamaa zao. Human Rights Watch iligundua kuwa baadhi ya waliokuwa wakizuiwa waliteswa.

Serikali ya Sudan imekanusha kuhusika

Maafisa wa serikali ya Sudan wamekuwa mara kwa mara wakikanusha idadi kamili ya waliouawa katika maandamano hayo na kupuuzilia mbali madai kuwa serikali ilihusika. Ahadi za kuendeshs auchunguzi huru ambao utawekwa wazi kwa umma pia hazijatimizwa.

Waandamanaji mjini Khartoum wakipinga hatua ya serikali kuondoa ruzuku ya mafuta

Waandamanaji mjini Khartoum wakipinga hatua ya serikali kuondoa ruzuku ya mafuta

Ripoti kutoka kwa ofisi ya mwendesha mkuu wa mashitaka Mashood Baderin katika jimbo la Khartoum iliyotumwa kwa wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa walioko Sudan mwezi Juni mwaka huu inaeleza kuwa watu 85 waliuawa lakini waliowafyatulia risasi hawajaweza kutambulika kutokana na ukosefu wa ushahidi.

Katika ripoti nyingine iliyotolewa tarehe nne mwezi huu, Baderin alisema ripoti ya serikali haitoi thibitisho lolote kuwa uchunguzi wa kina na huru ulifanywa na kuongeza kutokana na idadi kubwa ya watu waliopoteza maisha yao na haja ya kuwepo uwajibikaji, kuna haja kisheria kuwepo kwa uchunguzi huru kuhusu mauaji hayo na madhila mengine.

Maandamano hayo ya mwaka jana yalioanza mwezi Septemba hadi Okotoba,kwa kiasi kikubwa yalikuwa ya amani licha ya vijana katika siku za mwanzo kuchoma mali yakiwemo majengo ya serikali na magari. Serikali ilijibu kwa kutumia nguvu kupita kiasi na kuwakandamiza wanahabari kusudi wasiripoti kuhusu maandamano hayo kwa kuwakamata,kuwazuia na kufunga baadhi ya vituo.

Mwandishi:Caro Robi/Hrw.org/africa/sudan

Mhariri: Gakuba Daniel