Human Rights Watch yataka Sudan ikomeshe kamatakamata | Matukio ya Afrika | DW | 01.03.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

SUDAN

Human Rights Watch yataka Sudan ikomeshe kamatakamata

Shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch linasema kikosi maalum cha jeshi nchini Sudan kinawakamata raia kinyume cha sheria na hakuna hatua zilizochukuliwa na serikali ya mpito kulinda haki za mahabusu hao.

Ripoti iliyotolewa leo (Jumatatu, Machi 1) na shirika hilo inasema licha ya kikosi hicho kiitwacho RSF kutokuwa na mamlaka ya kisheria kukamata na kuweka watu kizuizini, kimekuwa kikiwashikilia mahabusu na kuwazuwia kutokuonana na jamaa au wanasheria wao katika mazingira yanayoashiria kuwafanya watu hao wasionekane tena.

Human Rights Watch imeitaka serikali ya Sudan kuchukuwa hatua za haraka kukizuwia kikosi hicho kufanya matendo hayo yaliyo kinyume na sheria na pia kuhakikisha raia wote waliowekwa mahabusu wanaachiliwa haraka.

"Serikali ya mpito ya Sudan lazima ikidhibiti kikosi cha RSF, ambacho kinajitwalia madaraka yasiyokuwa yake kisheria. Haikubaliki kabisa kwa jeshi kuwashikilia raia mahabusu badala ya kuwakabidhisha kwa mamlaka za kiraia ama kuwaachia huru kama hilo haliwezekani." Alisema mkurugenzi wa shirika hilo kwa eneo la Pembe ya Afrikam Laetitia Bader, alipotowa ripoti hiyo jijini Nairobi.

Human Rights Watch imesajili matukio kadhaa ya kukamatwa raia katika mwaka 2020 na kikosi hicho ambacho kinafahamika kwa kuhusika kwake na ukatili dhidi ya raia wa jimbo la Darfur na maeneo mengine yenye mizozo.

Sudan Soldaten RSF

Kikosi cha s Rapid Support Forces (RSF) nchini Sudan kinatuhumiwa kwa kuwakamata watu ovyo na kuwaweka mahabusu kinyume cha sheria.

Yanayowakumba mahabusu mikononi mwa RSF

Baina ya mwezi Septembe 2020 na Februari 2021, shirika hilo liliwahoji mahabusu wanne wa zamani, wanafamilia wawili na mwanasheria mmoja juu ya kadhia hizo, ambapo mahabusu hao wa zamani walisema kwamba maafisa wa kikosi hicho waliwashikilia kwa kipindi cha baina ya wiki moja hadi mwezi mzima bila ya kuwaruhusu kuwasiliana na jamaa ama wanasheria wao. Wawili kati yao waliadhibiwa vikali na kikosi cha RSF.

Kwenye ripoti hiyo, Human Rights Watch inaitaka serikali ya Sudan kuchunguza matukio ya kukamatwa watu ovyo, kufungiwa ndani bila kuruhusiwa kuwasiliana na jamaa zao, kupotezwa, na mateso mengine wawapo vizuizini, likiwemo la kifo cha mmoja wa mahabusu hao. 

Kwa mujibu wa katiba ya mpito ya Sudan, kikosi cha RSF kimewekwa kwenye kundi la majeshi ya kawaida, lakini kinafahamika kwamba ndicho kilichoongoza operesheni ya ukandamizaji dhidi ya maandamano ya amani ya tarehe 3 Juni 2019 katika viunga vya miji ya Khartoum, Bahri na Omdurman, ambayo ilipelekea vifo vya watu 120 na mamia ya wengine kujeruhiwa.

Licha ya kuwa na sifa hiyo mbaya, bado serikali ya mpito ya Sudan imeendelea kuwatumia maafisa wa kikosi hicho kudhibiti watu kwenye mikusanyiko mikubwa na pia kwa ajili ya operesheni za kusimamia usalama.