1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hukumu dhidi ya Oscar Pistorius yasomwa

11 Septemba 2014

Oscar Pistorius, mwanariadha wa Afrika kusini anayekimbia kwa miguu ya bandia, anakabiliwa na hukumu leo(11.09.2014), wakati jaji ameanza kusoma hukumu ya kesi ya mauaji, ambayo inaweza kumpeleka jela kwa miaka 25.

https://p.dw.com/p/1DAJu
Südafrika Mordprozess Oscar Pistorius Gericht in Pretoria 11.09.2014
Jaji Thokozile Masipa akisoma mapitio ya kesi ya PistoriaPicha: picture-alliance/K. Ludbrook

Katika hali ya kumbukumbu ya jinsi Afrika kusini ilivyobadilika katika muda wa miaka 20 iliyopita tangu kung'olewa kwa utawala wa kibaguzi, hatima ya Pistorius , mzungu ambaye pia ni tajiri akitokea katika jamii yenye mafanikio, iko mikononi mwa mwanamke mwenye asili ya Afrika mwenye umri wa miaka 66 kutoka Soweto, Jaji Thokozile Masipa.

Mwanariadha huyo nyota aliwasili mahakamani katikati ya mji mkuu Pritoria akivalia suti yake nyeusi na shati jeupe. Alikuwa amezungukwa na kundi la walinzi wake na polisi ambao walimsindikiza akipita kundi la waandishi habari pamoja na kamera za televisheni.

Südafrika Mordprozess Oscar Pistorius Gericht in Pretoria 11.09.2014
Oscar Pistorius kizimbaniPicha: Reuters/K. Ludbrook

Jee , Pistorius aliuwa kwa kukusudia?

Wakati jaji Thokozile Masipa akianza kusoma mapitio ya kesi hiyo iliyochukua siku 41 na mashtaka ya mauaji na mengine matatu madogo, ambayo hayahusiani na makosa yanayohusiana na silaha, Pistorius ambaye alionekana mtulivu alijiinamia kizimbani , akibubujikwa na machozi.

Masipa analazimika kufanya mapitio ya kurasa 4,000 za nyaraka kutoka siku 41 za kesi hiyo , ikiwa na maana kwamba hukumu ya mwisho huenda ikacheleweshwa hadi kesho Ijumaa.

Südafrika Gericht Verhandlung Oscar Pistorius
Oscar Pistorius akiwa kizimbani amejiinamiaPicha: Reuters

Akisoma mapitio hayo ya kesi leo, jaji Thokozile Masipa amesema kuna shaka , iwapo mwanamke alipiga ukelele usiku wakati Oscar Pistorius alipompiga risasi mpenzi wake Reeva Steenkamp mwaka jana kwasababu kuna utata wa mgongano wa maelezo katika ushahidi uliotolewa na mashahidi.

Taifa dhidi ya Pistorius

Taifa , ambalo linataka Pistorius ahukumiwe kwa kosa la kuuwa kwa kukusudia , limedai kwamba Steenkamp alipiga ukelele katika kipindi cha ugonvi mkubwa na mwanariadha huyo anayekimbia mbio za walemavu kabla ya kupiga kwa risasi kwa kukusudia kupitia mlango ambao ulikuwa umefungwa wa chooni.

Pistorius amejitetea kwa kusema alimpiga risasi Steenkamp kwa bahati mbaya akiamini ni mtu aliyekuwa ameingia katika nyumba yake kwa nia ya kufanya uhalifu.

Hapo kabla hata hivyo jaji Masipa amesema kuwa madai ya upande wa mashitaka kwamba kulikuwa na hali ya kuchafuliwa ushahidi katika eneo la tukio , hayana maana.

Oscar Pistorius Verteidiger Barry Roux 8. August
Wakili wa Pistorius Barry RouxPicha: Reuters

Hata hivyo ametia shaka kuhusu uaminifu wa ushahidi kutoka kwa majirani ambao wamesema walisikia milio ya bunduki ikichanganyika na ukelele.

"Kuna uwezekano mkubwa Pistorius akahukumiwa kwa mauaji lakini sio ya kukusudia," amesema James Grant, profesa wa sheria kuhusu uhalifu katika chuo kikuu cha Witwatersrand , mjini Johannesburg, ambaye anadhani kwamba mahakama itamhukumu Puistorius kwa uzembe.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Yusuf Saumu