HRW: M23 walitumika kupambana na waandamanaji DRC | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.12.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

HRW: M23 walitumika kupambana na waandamanaji DRC

Ripoti ya Human Rights Watch imeeleza kuwa, Maofisa wa juu wa Usalama nchini  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo waliwatumia waasi wa kundi la M23  ili kuwazuia waandamanaji waliokuwa wakimpinga Rais Joseph Kabila

Kongo Unruhen in Kinshasa (Reuters/N'Kengo)

Waandamanaji wakichoma tairi katika mji Mkuu wa Kinshasa, Congo,wakati wa maandamano, mnamo Januari 2015.

 Ripoti hiyo yenye kurasa 69  inaeleza kuwa waasi hao zaidi ya 200 walitumika kuzuia maandamano ya kumpinga Rais Kabila.  Tangu wakati huo, Kabila, ameendelea kuimarisha nguvu zake, huku akiuchelewesha uchaguzi.

Ripoti hiyo, ilipewa  jina la  Mpango maalum: Utumiaji wa waasi wa M23 katika kuzima maandamano nchini Congo.

 Ripoti hiyo inaeleza kuwa maofisa usalama wa Congo kwa kushirikiana  na wapiganaji wa M23 kutoka Uganda na Rwanda, waliua karibu watu 62 na kukamata mamia wakati wa maandamano hayo ya kuipinga serikali katika kipindi cha Desemba 19 hadi Desemba 22. 

Ni katika kipindi ambacho Kabila aligoma kuondoka madarakani kama katiba ya nchi hiyo inavyomtaka Rais  kuongoza kwa mihula miwili tu.

 Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wapiganaji wa M23 walilinda mitaa ya miji mikuu ya Congo, wakifyatua risasi au kukamata waandamanaji  au yeyote aliyeonekana kuwa tishio kwa Rais.

Matokeo ya ripoti hiyo, yalijikita katika mahojiano  waliofanyiwa watu 120 , yakiwahusisha waathirika wa unyanyasaji, familia zao, mashahidi, wanaharakati wa ndani pamoja na maofisa usalama tisa wa Congo.

Akizungumzia matokeo ya utafiti  huo,  Mkurugenzi wa Taasisi hiyo kwa  upande wa Afrika ya Kati, Ida Sawyer alikuwa na haya ya kusema kuwa kama waasis wanaweza kutumika kuzuia waandamanaji basi wanaweza kufanya chochote kile ili kubaki madarakani.

Human Rights Watch Logo

Nembo ya Shirika la Kutetea Haki za Binadamu, Human Right Watch.

 Utafiti wawahoji wapiganaji 21 wa M23

Wengine waliohojiwa katika utafiti huo ni pamoja na maofisa wa serikali, Umoja wa Mataifa, wanadiplomasia na wapiganaji 21 wa M23.

Human Right Watch ilifanya utafiti huo, katika maeneo ya Kinshasa, Goma, Lubumbashi . Kadhalika na upande wa Uganda, Rwanda, Brussels. Utafiti huo ulifanyika katika kipindi cha Desemba 2016 hadi Novemba 2017.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa, kati ya Oktoba na mwanzoni mwa Desemba, 2016, wakati kukiwa na shinikizo kubwa la Kabila kuondoka madarakani,  maofisa wa juu wa usalama wa  Congo, waliwatumia wapiganaji hao wa M23 kutoka katika kambi za jeshi na za wakimbizi, zilizoko nchini  Uganda na Rwanda.

Baada ya kupelekwa Congo, M23 walihamishiwa katika mji mkuu wa Kinshasa, Goma na Lubumbashi. Wanausalama waliwapa sare mpya na silaha na kisha wakajiingiza  miongoni mwa polisi, jeshi, na Walinzi wa nchi. Kadhalika ripoti hiyo inaeleza kuwa,  maofisa wa jeshi wa Congo,  wengi wao wakiwa waliosaidiwa na waasi wa Rwanda, walitumika kuwaangalia, kuwalipa na kuwapa chakula na malazi kundi hilo la M23.

 Ili kumlinda Rais Kabila  na  kuwazuia waandamanaji, wapiganaji wa M23 walipewa amri maalum ya kutumia silaha za moto mara moja, dhidi ya  wananchi waliodhubutu kufanya  chokochoko.

Maofisa wa Congo, waliwarudisha wapiganaji wa M23 nchini Uganda na Rwanda, mwishoni mwa Desemba  2016 na  mwanzoni wa Januari mwaka huu.

 Wengi wao walirudishwa kati ya Mei na Julai na kupelekwa maeneo ya Kisangani,  Kaskazini, Mashariki mwa Congo wakidaiwa kujiandaa kwa ajili ya operesheni maalum  ili kuwajibika pindi kitakapotokea kikwazo chochote katika utawala wa Kabila.

Novemba 5 mara baaada ya Balozi wa Umoja wa Mataifa, Nikki Haley kuitembelea Congo na kumtaka Kabila kuitisha uchaguzi mpya mwishoni mwa 2018, Tume ya Uchaguzi nchini humo, ilichapisha kalenda mpya ya uchaguzi na kutangaza  tarehe ya uchaguzi kuwa Desemba 23, 2018.  Lakini kipindi hicho ni cha zaidi ya miaka miwili baada ya muda wake wa kukaa madarakani kumalizika.

 Mwandishi: Florence Majani(https://www.hrw.org/news/2017/12/04/interview-how-dr-congos-president-hired-rebel-fighters-crush-protests, AFP)

Mhariri: Saumu Yusuf

 

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com