1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hotuba ya Trump yaanika mpasuko wa kisiasa Marekani

Daniel Gakuba
5 Februari 2020

Rais Trump kususia mkono wa Spika Pelosi na Pelosi kumjibu kwa kuichana hotuba yake ni baadhi tu ya vitimbi vilivyodhihirisha mgawanyiko mkali wa kisiasa nchini Marekani, wakati Trump alipotoa hotuba kuhusu hali ya nchi.

https://p.dw.com/p/3XHcQ
USA, Washington: Trump hält State of the Union Rede im Capitol
Spika wa Baraza la Wawakilishi Marekani Nancy Pelosi akiichana vipande vipande hotuba ya Rais Donald TrumpPicha: Getty Images/AFP/M. Ngan

Tofauti na ilivyozoeleka kuwa hotuba ya rais wa Marekani kuhusu hali ya nchi ni muda wa maridhiano kisiasa, mazingira katika kikao cha Congress kilichowaleta pamoja wajumbe wa baraza la wawakilishi na maseneta yaliakisi mpasuko mkali wa kisiasa muda wote wa saa moja na dakika 18 wa hotuba ya Trump.

Zoezi zima lilianza vibaya pale Rais Trump alipokataa kuupokea mkono alionyooshewa na spika wa baraza la wawakilishi Bi Nancy Pelosi na kuuacha ukining'inia hewani. Na lilimalizika kwa hatua ya Pelosi kumjibu Trump mtindo wa jino kwa jino, alipochana vipande vipande nakala ya hotuba ya Trump aliyokuwa amekabidhiwa, mara tu Trump alipomaliza kuzungumza.

Wasaa wa kujitapa na kujigamba

Rais Trump ametumia sehemu kubwa ya hotuba yake kwa majigambo, ya namna alivyofanikiwa kuukarabati uchumi wa Marekani, na hadhi ya nchi hiyo, ambavyo amedai vilikuwa vimewekwa rehani na watangulizi wake.

USA, Washington: Trump hält State of the Union Rede im Capitol
Rais wa Marekani Donald Trump akitoa hotuba ya hali ya nchi mbele ya CongressPicha: Getty Images/AFP/M. Ngan

''Miaka ya uozo wa kiuchumi imekwisha. Siku za Marekani kuhujumiwa kiuchumi na kukejliwa na mataifa mengine tumeziacha nyuma. Tumeipa pia kisogo mienendo ya kuvunja ahadi, na kutafuta visingizio vya kumomonyoka kwa uchumi, nguvu na fahari ya Marekani.'' Amesema Trump na kuongeza kuwa kwa miaka mitatu tu, ''tumevunjilia mbali mitazamo ya kwamba Marekani inadidimia.''

Masuala mengine aliyoyamulika Trump katika hotuba yake, ni mikubaliano ya kibiashara kati ya China, na mengine ya eneo huria la kibiashara katika nchi za Amerika Kaskazini, akisema hayo ni mafanikio makubwa ambayo yatarejesha maelefu ya viwanda nchini Marekani.

Amezungumzia pia sera za kupunguza kodi na kumaliza kuhusika kwa majeshi ya Marekani katika mizozo ya Mashariki ya Kati, kama ushahidi wa kutimiza ahadi alizozitoa kwa wapiga kura.

Ufa mpana kati ya Warepublican na Wademocrat

Hotuba yake ilishangiliwa mara kwa mara na wabunge wa chama chake cha Republican waliosimama kumpigia makofi, huku wademocrat wakibakia katika viti vyao, baadhi wakizomea, na wengine hata kutoka nje.

Pete Buttigieg - Präsidentschaftskanditat der Demokraten
Pete Buttigieg, mshindi wa uchaguzi wa mchujo upande wa Wademocrat katika jimbo la IowaPicha: Reuters/B. McDermid

Trump ambaye baadaye leo anatarajiwa kuondolewa hatia katika kesi anamoshtakiwa na wademocrat kwa tuhuma za matumizi mabaya ya wadhfa wake, hata mara moja hakuitaja kesi hiyo katika hotuba yake.

Wakati huo huo, matokeo ya uchaguzi wa kwanza wa mchujo katika chama cha democratic uliofanyika katika jimbo la Iowa yametangazwa, baada ya kucheleweshwa kutokana na hitilafu za kiufundi. Baada ya kuhesabiwa asilimia 62 ya kura, Meya wa zamani Pete Buttigieg amekuja katika nafasi ya kwanza, akifuatiwa na maseneta Bernie Sanders na Elizabbeth Warren, huku makamu wa rais wa zamani Joe Biden aliyepigiwa upatu kuongoza katika mbio za kukiwakilisha chama chake katika uchaguzi wa rais ujao, akitupwa mbali katika nafasi ya nne.

 

afpe, dpae, ape