Hotuba ya Steinmeier kuadhimisha siku ya Muungano Magazetini | Magazetini | DW | 04.10.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Hotuba ya Steinmeier kuadhimisha siku ya Muungano Magazetini

Hotuba ya rais wa shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Frank-Walter Steinmeier kuadhimisha siku ya muungano na kitisho cha kupoteza umuhimu wake chama cha Social Democratic-SPD ni miongoni mwa mada magazetini.

Tunaanzia Mainz zilikofanyika sherehe rasmi za miaka 27 ya Muungano. Kauli mbiu ya sherehe za mwaka huu ni "Sote kwa pamoja ni Ujerumani."Gazeti la "Allgemeine Zeitung" linaichambua hotuba ya rais wa shirikisho Steinemeier na kuandika:"Kwa mara ya kwanza rais wa shirikisho amezungumzia kile ambacho kwa miaka kadhaa tumekuwa tukijidanganya. Kwamba hadhi katika maisha haimaanishi pekee hifadhi ya jamii na pensheni kubwa kubwa. Ushindi wa wafuasi wa siasa kali za kizalendo katika uchaguzi mkuu uliopita, umedhihirisha wazi kabisa kwamba sehemu kubwa ya wajerumani wa Mashariki hawajisikii vizuri katika Ujerumani ya uwazi na ya kiliberali."

Wanasiasa wawajibike

Gazeti la "Ludwigsburger Kreiszeitung" linaichambua miaka 27 ya muungano na  kuandika: "Steinmeier alipochaguliwa kuwa rais wa shirikisho Februari iliyopita, hakuwa pengine akitambua changamoto za wadhifa wake. Sasa anaziona. Miaka 27 imekamilika tangu Ujerumani ilipoungana upya, muda huo umesaidia kuponya majaraha ya kale lakini kuta nyengine zimechomoza, kama Steinmeier alivyosema. Ushahidi ni kuwakilishwa chama cha AfD katika bunge la shirikisho. Kinachohitajika sasa ni kujibu kwa kufuata siasa ambayo masuala yote yatazingatiwa. Amegusia ndipo kabisa rais wa shirikisho na huo pia ni wito kwa wanasiasa mjini Berlin. Kwasababu wao ndio chanzo cha vurugu na watu kukata tamaa."

 Hatima ya chama cha SPD

 Uchaguzi mkuu uliopita umezusha zilzala ya kisiasa humu nchini. Sio tu kwamba chama cha siasa kali za mrengo wa kulia "Chaguo Mbadala kwa Ujerumani"-AfD kinawakilishwa kwa mara ya kwanza katika bunge la shirikisho, bali pia kwa sababu chama kikongwe cha kisiasa humu nchini, chama cha Social Democrat kimepata pigo kubwa kuwahi kushuhudiwa tangu vilipomalizika vita vikuu vya pili vya dunia. Gazeti la "Märkische Oderzeitung" linachambua mzozo uliozuka ndani ya chama hicho na kuandika: "Martin Schulz hajakosea anaposema, miaka inayokuja kipa umbele kitakuwa kupigania mustakbali wa siasa za ujamaa wa kidemokrasia nchini Ujerumani. SPD kiko taabani na yanayokisibu chama cha kisoshialisti cha Ufaransa ni onyo nacho pia kisije kikatoweka mapema kuliko wengi wanavyofikiria. Sifa za zamani kama chama cha wananchi hazisaidii kitu: Atakaeweza kukiokoa chama hicho ni wanachama wake tu; na hasa vijana, wanachama wepya na wanawake. Na wote hao wanapaza sauti kudai marekebisho.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com