1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hoppe awapa matumaini Schalke kupata ushindi wa kwanza

Bruce Amani
11 Januari 2021

Habari kubwa hata hivyo ambayo wengi walisubiri kuona iliihusu Schalke 04 ambayo ilikuwa katika mkondo wa kuvunja rekodi mbaya kabisa ya kutoshinda katika mechi 31 mfululizo kwenye Bundesliga.

https://p.dw.com/p/3nn5R
Deutschland Bundesliga FC Schalke 04 v TSG Hoffenheim | 3. Tor Matthew Hoppe
Picha: Ina Fassbender/REUTERS

Habari kubwa hata hivyo ambayo wengi walisubiri kuona iliihusu Schalke 04 ambayo ilikuwa katika mkondo wa kuvunja rekodi mbaya kabisa ya kutoshinda katika mechi 31 mfululizo kwenye Bundesliga. Rekodi ambayo wanaoishikilia ni Tasmania Berlin, walioiweka miaka 54 iliyopita. Na walikuwa wanaiombea Schalke ipate ushindi ili rekodi yao isiharibiwe.

Maombi hayo yalijibiwa hasa na kinda mmoja wa Kimarekani kwa jina Mathew Hoppe ambaye alifunga hat trick na kuipa Schalke ushindi mnono wa 4 – 0 dhidi ya Hoffenheim. Ukiwa ushindi wa kwanza wa Schalke katika mechi 30. Ushindi wao wa mwisho kwenye ligi ulikuwa Januari 17, 2019.

Deutschland Bundesliga FC Schalke 04 v TSG Hoffenheim | Kolasinac
Kolasinac alitanguliza dua kabla ya mechiPicha: Tim Rehbein/RHR-FOTO/imago images

Tasmania ilicheza mechi 31 mfululizo bila ushindi katika msimu wa 1965-66. Kocha wa Schalke Christian Gross, ambaye aliitwa kuja kuokoa jahazi kutoka maisha ya kustaafu alielezea furaha yake. "Bila shaka tumefurahishwa na matokeo haya na pointi hizi tatu. Ninafahamu kuwa tulilazimika kumtegemea pakubwa kipa wetu hodari, Ralf Fährmann, hasa katika kipindi cha kwanza. Timu ilijiamini Zaidi baada ya kuwa kifua mbele 1 – 0. Lakini nafahamu tuna kazi nyingi ya kufanya. Hilo ni moja. Kwa upande mwingine, nataka kusisitiza tena kuwa timu ilifanya kila kitu, na bahati ilikuwa upande wetu leo."

Na kwa nini Tasmania wanajivunia rekodi hiyo mbaya? Mwenyekiti wa klabu hiyo ya Berlin Almir Numic aliiambia redio ya mjini humo kuwa bila rekodi hiyo, hakuna mtu Ujerumani au Ulaya ambaye angeweza kuizungumzia Tasmania Berlin.

Katika matokeo mengine, Bayer Leverkusen ililazimisha sare ya 1 – 1 na Werder Bremen, wakati Union Berlin zikitoka sare na Wolfsburg 2 – 2 katika mechi ya kusisimua kabisa ambayo tulikutangazia moja kwa moja hapa DW Kiswahili

afp/reuters/ap/dpa