1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hongereni DW

17 Januari 2013

Ninaishika kalamu, shairi kulitongoa Kuyaghani ya muhimu, kuhusu yetu idhaa Radio yetu timamu, habari yatangazia Idhaa ya Kiswahili, Redio Ujerumani

https://p.dw.com/p/17LaW
Wettbewerb zum 50-jährigem Jubiläum. Musa Jafari Banji Dar Art Youth (Day) P.O. Box 79505 Dar es Salam, Tanzania 0716088888
50 Jahre Kisuaheli Redaktion WettbewerbPicha: DW

Imetimia hamsini, miaka ya kuzaliwa
Sauti Ujerumani, Kiswahili kuenziwa
Lugha hii ya thamani, ni fahari kutumiwa
Idhaa ya Kiswahili, Redio Ujerumani

Mambo yanayotokea, vipindi kutwelimisha
Makala za kuvutia, nzuri kufikirisha
Kila pembe za dunia, matukio kutupasha
Idhaa ya Kiswahili, Redio Ujerumani

Vipindi bora murua, matangazo maridhawa
Katu hamkubania, kwa uwazi mwasifiwa
Akili 'litufungua, maarifa yengaziwa
Idhaa ya Kiswahili, Redio Ujerumani

Haki mnaihubiri, bila woga wala haya
Ya kweli mwayabaini, uongo kuuzomeya
Mwayaanika dhahiri, mazuri nayo mabaya
Idhaa ya Kiswahili, Redio Ujerumani

Uhuru demokrasi, mumekuwa watetezi
Kaumu kadamnasi, sauti ya ukombozi
Arabuni na Urusi, mnapinga uonezi
Idhaa ya Kiswahili, Redio Ujerumani

Makala za mazingira, tamaduni, jinsia
Mijadala ya kung’ara, kwayo fora mnatia
Uchambuzi wenye dira, vinara mumebobea
Idhaa ya Kiswahili, Redio Ujerumani

Michezo, siasa na dini, kiu yetu mwaizima
Sanaa na burudani, kwa ladha ya kuzizima
Nyimbo tamu sikioni, na midundo ya magoma
Idhaa ya Kiswahili, Redio Ujerumani

Tunafaidi makala, za afya na malezi
Kazi yenu ni muwala, kwa marefu na ujazi
Inameta kwa jamala, tafakari tunduizi
Idhaa ya Kiswahili, Redio Ujerumani

Ulaya na Afrika, napo kote Bara Hindi
Karibini Amerika, vinasikika vipindi
Kwa muda na uhakika, vimepikwa kwa ufundi
Idhaa ya Kiswahili, Redio Ujerumani

Hongera nazimimina, Redio Ujerumani
Matangazo ya kufana, ubora uso kifani
Yenu ni kubwa dhamana, nawapa taji la shani
Idhaa ya Kiswahili, Redio Ujerumani.

Nawapa taji la shani, hamsini kutimiza
Na Mungu awaauni, dira msijepoteza
Mbakie kileleni, Kiswahili kueneza
Idhaa ya Kiswahili, Redio Ujerumani.

Tanbihi: Shairi hili limeandikwa na Emmanuel Marwa (Msemakweli-Mbiu ya Ushairi) wa Mufindi Iringa, Tanzania na picha imechorwa na Musa Jafari Banji wa Dar es Salaam, Tanzania, kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 ya DW.

Mhariri: Mohammed Khelef