Homa ya nguruwe yazagaa | Magazetini | DW | 30.04.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Homa ya nguruwe yazagaa

Homa ya nguruwe,ukosefu wa usalama nchini Afghanistan ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo Alkhamisi.Basi tukianza na gazeti la NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG linasema:

"Virusi vya homa ya nguruwe sasa vimeathiri zaidi ya nchi ishirini kwa hivyo shinikizo ni kubwa kwa viongozi na madaktari kuhakikisha kuwa kutakuwepo dawa za kutosha iwapo ugonjwa huo utazidi kuenea.Kwa maneno mengine kinachohitajiwa ni kinga na sio kiwewe."

Gazeti la SÄCHSISCHE ZEITUNG likiendelea na mada hiyo hiyo linasema:

"Hali ya wasi wasi imezagaa kwani kila kukicha,kesi mpya za homa ya nguruwe zinaripotiwa sehemu mbali mbali za dunia.Lakini kuna habari nzuri pia kwani dawa za kuzuia virusi hivyo kuzaliana zinafanya kazi na hivyo husaidia kupunguza kasi ya ugonjwa huo kuenea. Lakini hiyo haimaanishi kuwa hatari imetoweka. Vile vile kila mmoja anapaswa kuzidisha hatua za usafi kama vile kukosha mikono.Na utaratibu huo usisahauliwe hata kitisho cha homa ya nguruwe kitakapotoweka. Mara nyingi uwezekano kwa hatari mpya kuchomoza hupuuzwa."

Tukigeukia mada nyingine,gazeti la WESTDEUTSCHE ZEITUNG linaeleza :

"Katika miezi ya hivi karibuni hali ya usalama kaskazini mwa Afghanistan - eneo linalosemekana kuwa na utulivu wa aina fulani-imezidi kusababisha mabishano. Kila siku,hali ya hatari inazidi kuwa kubwa kwa wanajeshi wa Kijerumani kaskazini mwa Afghanistan kwani Marekani inaimarisha vikosi vyake ukingoni mwa mji mkuu Kabul na hivyo wanamgambo wa Kitaliban hawana budi ila kukimbilia maeneo ya kaskazini."

Kwa maoni ya WESTDEUTSCHE ZEITUNG:

"Bado kuna kazi kubwa ya kutekelezwa kabla ya jumuiya ya kimataifa kuweza kuwashinda kijeshi wanamgambo wa Taliban. Na huo ni ukweli usiopaswa kufichwa na wanasiasa wa Ujerumani hata wakati huu wa kujitayarisha kwa kampeni za uchaguzi ujao.Wakati huo huo, serikali iendelee kupigia debe mradi wake wa kusaidia kuijenga upya Afghanistan.Kwani hayo ni matumaini pekee ya umma katika nchi iliyoteketezwa kwa vita."

Tunamalizia kwa uhariri wa gazeti la BADISCHE NEUESTE NACHRICHTEN linalosema:

"Umoja wa Ulaya haumudu tena kuwapokea wanachama wepya bila ya kuhatarisha mshikamano na kujitenganisha na umma.Mkataba wa Lisbon uliokataliwa na Ireland ni mageuzi haba kwa Umoja wa Ulaya kuweza kuwa na uzito na uwezo wa kupitisha maamuzi katika ulimwengu wa utandawazi.Licha ya mkataba huo,Umoja wa Ulaya unabidi kujiwekea mipaka."

Mwandishi: P.Martin

Mhariri: Abdul-Rahman

 • Tarehe 30.04.2009
 • Mwandishi Prema Martin
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Hh1L
 • Tarehe 30.04.2009
 • Mwandishi Prema Martin
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Hh1L