1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hollerbach aachia ngazi Hamburg SV

Sekione Kitojo
12 Machi 2018

Baada ya  wiki  saba  madarakani  kocha  wa  Hamburg SV Bernd Hollerbach aachia  ngazi, safari ya kigogo hicho cha soka nchini  Ujerumani kuelekea daraja la pili nyeupee ..

https://p.dw.com/p/2uBuR
Fußballtrainer Hamburg Bernd Hollerbach
Bernd Hollerbach kocha wa zamani wa Hamburger SVPicha: picture-alliance/dpa/M. Christians

 

Ni timu  ambayo  haijashuka daraja  tangu  Bundesliga  kuanzishwa  mwaka  1963. Imekwisha  kuwa  bingwa  wa  ligi ya  taifa  Bundesliga mara  6, kombe  la shirikisho DFB Pokal mara 3,  kombe  la washindi  barani  Ulaya, hivi  sasa  Europa League mara  1 na  Kombe  la  Ulaya , hivi  sasa  Champions League mara 1. Timu  hii  ni  Hamburger SV  ambayo  kwa  jina  la  utani inaitwa  Dino, ama  Dinosaurus, wanyama  waliokuwa wakiishi  katika  dunia  miaka  milioni  kadhaa  iliyopita ambao  sasa  hawako  tena.

Deutschland 1. Bundesliga Javi Martinez (FC Bayern München)
Javi Martinez wa Bayern Munich akimpita mchezaji wa Hamburg SV Walace (anayeanguka chini)Picha: Imago/Sven Simon

Hiyo  ndio historia  fupi ya  Hamburg SV ambayo  ni  ya mafanikio  makubwa  katika  soka  la  Ujerumani, timu ambayo  aliichezea pia  mchezaji  maafuru  wa  Ujerumani Kaiza Franz Beckenbauear  na  mchezaji  maarufu  wa Uingereza  Kevin Keegan. Lakini  hivi  sasa  imo katika hatari  ya  kushuka  daraja  la  pili na  kumekuwa  na mtafaruku  mkubwa  katika  timu  hiyo.

Misimu minne iliypopita  Hamburg SV imebadilisha  makocha  zaidi  ya kumi na  hakuna  hata  mmoja  aliyeonesha  kuiletea  uhai timu  hiyo licha ya kuiokoa  tu  dhidi  ya  kushuka  daraja. Lakini  msimu  huu  hali  inaonekana  kuwa  ngumu  zaidi kwani Kocha  Bernd Hollerbach aliyeteuliwa  kuiokoa  timu hiyo  naye  kibarua  kimeota  majani.

Fußball Bundesliga Hamburger SV, Trainer Bernd Hollerbach
Kocha Bernd Hollerbach aliyepewa jukumu la kuiokoa timu ya Hamburg kutoshuka daraja ameachia ngaziPicha: Imago/Ulmer

Leo  Jumatatu(12.03.2018)  kocha  wa vijana  wa  umri  chini  ya  miaka  21  wa  klabu  hiyo Christian Titz  anatarajiwa  kutajwa  rasmi  kuwa  kocha  wa timu  ya  kwanza.

Hatua ya kumuondoa  Hollerbach  imekuja  baada  ya kichapo  cha  mabo 6-0 dhidi  ya  mabingwa  watarajiwa FC Bayern. Mchezaji  wa  Hamburg SV Sven Schipplock anasema:

"Hapa kwa  kweli ni  suala  la  kupambana  tu, kama  kuna uwezekano wa  kushikilia matokeo ya 0-0 na  nafasi chache zinazopatikana , kuzitumia. Lakini  tulisambaratika baada  ya  dakika  chache. Sifahamu , kichwani tunafikiria nini. Kwasababu  hakuna  anayeelewa, na  mimi  pia sifahamu."

Alipoulizwa mchezaji  wa  Bayern Munich Arjen Robben iwapo hawakuwahurumia wenzao wa  Hamburg alisema:

Bundesliga - Bayern München gegen Hamburger SV
Arjen Robben wa Bayern MunichPicha: picture-alliance/dpa/S. Hoppe

"Nini  maana  ya  kuhurumia ? Nafikiri , wao  pia hawakuhitaji  kuhurumiwa. Hii  ni  kandanda. Huo  ndio ukweli, ambapo  wanajikuta hivi  sasa. Lakini  sifikiri, kwamba  tuliingia  katika  mchezo  huo  tukiwahurumia. Tunacheza  mchezo  wetu, tunashinda, tunahitaji kufunga mabao, tunahitaji  kujisikia raha."

Bayern huenda ikatawazwa mabingwa mchezo wa 27

Bayern  ambayo  inaongoza Bundesliga  kwa  pointi  66  na timu  inayoifuatia Schalke 04  ikiwa  na  pointi 46 huenda ikatawazwa  mabingwa  katika  mchezo  wa  27 ujao wakati itakapopambana  dhidi  ya  RB Leipzig.

Schalke 04  wameng'ang'ania  katika  nafasi  ya  pili  ya msimamo wa  ligi baada  ya  kuishinda Mainz 05  kwa  bao 1-0  siku  ya  Ijumaa. Lakini  Borussia  Dortmund  ilipata changamoto  kubwa  kuweza  kunyakua  pointi  zote  tatu jana  Jumapili  baada  ya  kufanyakazi  ya  ziada  kuishinda Eintracht Frankfurt  kwa  mabao 3-2 katika  mchezo  ambao timu  zote ziliingia  uwanjani  zikiwa  na  pointi 42, zikiwania kushika nafasi  ya  tatu. Alikuwa Michy Batschuayi aliyeazimwa  kutoka  Chelsea  aliyeipatia  ushindi Dortmund baada  ya  kufunga  bao  la  ushindi  katika  dakika  ya  94 ya nyongeza. Nahodha  wa  Dortmund Marcel Schmelzer:

Bundesliga Borussia Dortmund  Eintracht Frankfurt
Michy Batshuayi mshambuliaji wa Borussia Dortmund akishangiria baoPicha: Getty Images /Bongarts/L. Baron

"Tumepoteza  nafasi  nyingi  katika  michezo  yetu , kama vile  dhidi  ya  Augsburg. Dhidi  ya  Leipzig  tulicheza  vizuri na timu  ambayo ni washindani wa moja  kwa  moja. Leo pia Frankfurt  wametupa changamoto  kubwa, ilikuwa muhimu , kwamba  katika  mchezo  huu  wa  pointi  6 tumeweza  kupambana na kupata  pointi 3 muhimu. Ni duru  ngumu  kabisa ya mwisho.

Leo hii timu inayokamata  mkia  katika  Bundesliga FC Kolon  inatapia  maisha  yake kwa  kupambana  na  Werder Bremen. FC Kolon ina  pointi 17 ikifuatiwa na  Hamburg SV yenye  pointi 18 na  Kolon  ikishinda  leo jioni itajiweka katika  nafasi  nzuri  ya  kujinasua  kutoka  katika  hatari  ya kushuka  daraka , ikiwa  imesalia  michezo  7  kabla  ya Bundesliga  kukunja  janvi.

 

Mwandishi: Sekione  Kitojo / dpae / rtre / afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman