1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hollande: Ugaidi bado ni tishio kwa Ufaransa

14 Juni 2016

Rais wa Ufaransa, Francois Hollande amesema shambulizi la mauaji ya askari polisi na mpenzi wake ni kitendo cha kigaidi na ameonya kuwa Ufaransa bado inakabiliwa na kitisho kikubwa cha mashambulizi ya kigaidi.

https://p.dw.com/p/1J6Dq
Rais Francois Hollande
Rais Francois HollandePicha: picture-alliance/dpa/C. Petit Tesson

Hollande ameitoa kauli hiyo leo wakati akizungumza katika mkutano wa dharura alioitisha kati yake na maafisa waandamizi, baada ya shambulizi hilo lililotokea katika kitongoji cha Magnanville na ambalo linadaiwa kufanywa na mtu ambaye amekula kiapo cha utii kwa kundi lenye itikadi kali la Dola la Kiislamu-IS.

Rais Hollande amesema polisi huyo mwenye umri wa miaka 42 pamoja na mpenzi wake, walishambuliwa katika nyumba yao kaskazini-magharibi mwa Paris usiku wa kuamkia leo na kwamba bila kutilia shaka, hicho ni kitendo cha kigaidi. Amesema sio tu Ufaransa inayokabiliwa na kitisho cha ugaidi, bali ulimwengu wote.

''Lazima tushirikiane kwa pamoja. Mapambano dhidi ya ugaidi hayalihusu tu taifa moja au nchi maalum, bali jumuiya ya kimataifa. Mapambano dhidi ya ugaidi ni lazima yaambatane na kuchukuliwa hatua za kimataifa, kubadilishana taarifa na kuwafuatilia watu binafsi ambao wameorodheshwa kama watu wenye itikadi kali,'' amesema Hollande.

Magari ya polisi yakifanya doria kwenye eneo la tukio
Magari ya polisi yakifanya doria kwenye eneo la tukioPicha: Reuters/Reuters TV

Katika mkutano huo wa dharura, Hollande amesisitiza kuwa Ufaransa ambayo kwa sasa ndiyo mwenyeji wa michuano ya Kombe la mataifa ya Ulaya-Euro 2016, bado inakabiliwa na kitisho kikubwa sana cha ugaidi.

Mshambuliaji atambuliwa

Duru karibu na uchunguzi zimemtambua mshambuliaji huyo ambaye naye aliuawa katika operesheni ya polisi kuwa ni Larossi Abbala mwenye umri wa miaka 25. Mshambuliaji huyo aliwahi kuhukumiwa mwaka 2013 kutokana na kushirikiana na kundi la jihadi lenye mafungamano na Pakistan.

Mshambuliaji huyo pia alikuwa sehemu ya uchunguzi wa hivi karibuni wa mtandao unaowasajili wapiganaji wa jihadi wanaopambana nchini Syria. Wakati wa mazungumzo yaliyoshindikana kati ya mtu huyo na polisi ambayo yalimalizika kwa mapambano kwa polisi kuivamia nyumba hiyo, mshambuliaji huyo alikiri kufanya shambulizi hilo kwa niaba ya kundi la IS.

Hata hivyo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Pierre-Henry Brandet, amesema mtoto wa wapenzi hao waliouawa, amekutwa bila majeraha yoyote ndani ya nyumba hiyo, ingawa alikuwa katika mshtuko.

Eneo yalipotokea mauaji hayo
Eneo yalipotokea mauaji hayoPicha: Getty Images/AFP/M. Alexandre

Hilo ni shambulizi la kwanza la mauaji kuikumba Ufaransa, tangu yalipotokea mashambulizi ya kupangwa kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Paris, yaliyofanywa na kundi la IS, mwezi Novemba, 2015 ambapo watu 130 waliuawa.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Bernard Cazeneuve amesema zaidi ya watu 100 ambao wanaonekana kama ni tishio kwa usalama, wamekamatwa nchini Ufaransa tangu kuanza kwa mwaka huu, zikiwemo katika wiki za hivi karibuni.

Ufaransa kama ilivyo nchi nyingine za Ulaya, imeshuhudia mfululizo wa visa vya kuchomwa kisu, vinavyowalenga polisi au wanajeshi ambavyo vinafanywa na Waislamu wenye itikadi kali.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP,AP,DPA
Mhariri: Iddi Ssessanga