Hollande asisitiza viongozi waheshimu katiba | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.07.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Hollande asisitiza viongozi waheshimu katiba

Hollande yuko nchini Angola,kituo cha pili cha ziara yake katika nchi tatu barani Afrika . Nchi hizo zikiwa ni pamoja na Benin na kubwa linaloulizwa na wachambuzi ni nini hasa madhumuni ya ziara hiyo ?

Hollande in Benin

Rais Francois Hollande na mwenyeji wake Thomas Boni Yayi wa Beni mjini Cotonou Alhamisi.

Rais Francois Hollande alianzia ziara yake nchini Benin ambapo Alhamisi akizungumza katika mji mkuu wa Benin Cotonou alikuwa na ujumbe kwa viongozi wenye kungan´gania madaraka barani Afrika akisema lazima waheshimu katiba au wawe tayari kukabiliana na vuguvugu la umma. Hollande akaipongeza Benin kwa hilo, wakati ambao Rais wake Thomas Boni Yayi ametangaza kwamba hatogombea mhula wa tatu. Hollande alisema Benin ni mfano wa demokrasia na yuko nchini humo kuonyesha kwamba nchi hiyo inatoa mfano kwa wengine.

Akazungumzia yaliomfika Rais wa zamani wa Burkina Faso Blaise Campaore na akizungumza hayo, ikiwa ni siku moja baada ya watu 6 kuuwawa nchini Burundi katika machafuko mpya, kufuatia uamuzi wa rais Pierre Nkurunziza kugombea mhula wa tatu akihakikisha uchaguzi unafanyika kama ilivyopangwa. Viongozi katika nchi nyengine mbili barani humo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na rwanda nao wana azma hiyo hiyo. Ziara ya mwisho ya Rais wa Ufaransa nchini Benin ilifanywa na Francois Mitterand 1983. Hii leo Rais huyo wa Ufaransa anaelekea Angola na ataondoka baadae usiku kuelekea Cameroun kituo cha mwisho cha ziara hiyo.

Angola Präsident Jose Eduardo dos Santos

Rais Jose Eduardo dos Santos wa Angola

Akiwa Angola ambako rais Jose Eduardo dos Santos anatawala tokea 1979, rais Hollande atafungua kongamano la kiuchumi mchana huu kati ya Ufaransa na Angola ambapo pia mikataba kadhaa yenye kugharimu karibu dola bilioni moja itatiwa saini. kampuni ya mafuta ya Ufaransa Total ambayo 10 asili mia ya biashara yake duniani ni mafuta inayochimba Angola, itasaini mikataba miwili inayohusiana na nishati ya jua. kiongozi huyo wa Ufaransa alilisisitiza hilo Alhamisi usiku, katika mazungumzo na jamii ya wafaransa wanaoishi Angola mara baada ya kuwasili mjini Luanda, aliposema Ufaransa na Angola sasa zinakusudia kuimarisha uhusiano wao.

Uhusiano huo uliingia dosari katika ngazi ya kidiplomasia baada ya Ufaransa kuhusika katika kashfa ya mauzo ya silaha kwa Angola kinyume cha sheria 1994-iliojulikana kama Angolagate, kabla ya hali kuboreshwa kufuatia ziara ya mtangulizi wake Nicolas Sarkozy mjini Luanda 2008. Tokea vimalizike vita vya wenyewe kwa wenyewe 2002, Angola nchi ya pili kubwa kwa uchimbaji mafuta barani Afrika imekumbwa na matatizo kutokana na kushika kwa bei ya mafuta tangu mwisho wa 2014.

Nchini Cameroun ,suala kuu litakalozingatiwa mazungumzo yake ya rais Paul Biya ni hali ya usalama katika nchi hiyom inayotiwa msukosuko na kundi la wapiganaji wa itikadi kali kutoka Nigeria la Boko Haram. Cameroun inashirikiana na nchi nyengine za kanda hiyo ya Afrika magharibi- Chad, Niger na Nigeria yenyewe katika vita dhidi ya waasi hao, baada ya kusambaza harakati zao hadi ardhi ya nchi hizo jirani. Kwa jumla ziara ya rais Hollande katika nchi hizo tatu za kiafrika ni mchanganyiko wa masuilahi ya kisiasa na kiuchumi ya Ufaransa.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, afp, dw

Mhariri:Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com