1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hollande amchagua Waziri Mkuu mpya

1 Aprili 2014

Orodha kamili ya mawaziri katika serikali mpya ya Ufaransa inatarajiwa kutangazwa leo baada ya Rais Francois Hollande kufanya uamuzi wa kumteua Waziri wa Mambo ya Ndani Manuel Valls kuwa Waziri Mkuu.

https://p.dw.com/p/1BZSv
Frankreich Innenminister Manuel Valls wird neuer Ministerpräsident
Picha: ERIC FEFERBERG/AFP/Getty Images

Hii ni baada ya chama chake cha Kisoshalisti kushindwa vibaya katika uchaguzi wa mitaa ulioandaliwa Jumapili iliyopita. Manuel Valls mwenye umri wa miaka 51, anachukua nafasi ya Jean-Marc Ayraut ambaye alijiuzulu wadhifa wake baada ya matokeo mabaya ya chama cha Kisoshalisti. Serikali hiyo mpya haitawajumuisha mawaziri wawili wa chama cha Kijani ambao walikuwa sehemu ya utawala unaoondoka.

Chama cha Kijani kimesema “kinasubiri thibitisho” la mwelekeo wa serikali ya Valls kabla ya kuamua kuhusu ushirikiano zaidi. Hollande jana alithibitisha kujiuzulu kwa Ayrault na kuteuliwa Valls kupitia hotuba iliyorushwa kwenye televisheni, siku moja baada ya Wasoshalisti kushindwa na chama cha siasa za mrengo wa kulia katika zaidi ya miji 150 kwenye uchaguzi wa mitaa.

Katika hotuba yake rais aliwaambia raia wa Ufaransa, na hapa namnukuu, ''katika uchaguzi, mlielezea kutofurahishwa kwenu na kukasirishwa kwenu. Nimesikia ujumbe wenu ambao ni wa wazi.” Mwisho wa kumnukuu. Rais huyo amekiri kuwa wapiga kura wamepoteza subira kutokana na kodi za juu na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira.

Jean-Marc Ayrault ambaye amejiuzulu wadhifa wake kama waziri mkuu wa Ufaransa
Jean-Marc Ayrault ambaye amejiuzulu wadhifa wake kama waziri mkuu wa UfaransaPicha: Reuters

Hollande alisema Valls atatwikwa jukumu la kutekeleza mpango wa sera zinazounga mkono biashara, unaofahamika kama Mkataba wa Uwajibikaji. Lakini rais huyo amesema hilo litawekwa katika uwiano na “mkataba mpya wa mshikamano” ambao utajumuisha hatua za kuimarisha matumizi kwa ajili ya elimu na afya, na kupunguza mapato na kodi za mishahara, ili mradi tu waweze kufadhiliwa na makato kutoka kwingine.

Orodha kamili ya baraza jipya la mawaziri inatarajiwa kutangazwa leo huku kukisubiriwa kuona kama Hollande atamrejesha serikalini mama wa watoto wake wanne, Segolene Royal. Royal alikuwa mgombea wa urais wa Wasoshalisti katika mwaka wa 2007 lakini kujumuishwa kwake katika baraza la kwanza la mawaziri wa Hollande, kulizuiwa kwa sababu ya uhasama kutoka kwa Valerie Trierweiler, aliyekuwa mpenzi wa rais huyo kwa wakati huo.

Kikwazo hicho sasa kimeondolewa baada ya Hollande kutengana na Trierweiler, na Royal anadokezwa kurudi tena kwenye siasa kwa kupewa wizara kuu ya elimu, michezo na vijana. Valls, mzaliwa wa Barcelona, ni mwanasiasa ambaye amekuwa mwanachama maarufu sana katika serikali inayoongozwa na Wasoshalisti, na baada ya kuhudumu kama meneja wa mawasiliano katika kampeni ya Hollande mnamo mwaka wa 2012, amekuwa mtu wa karibu kwa rais huyo.

Mwandishi. Bruce Amani/AFP
Mhariri: Gakuba Daniel