Holbrooke afanya mazungumzo na maafisa wakuu wa usalama Afghanistan | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.02.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Holbrooke afanya mazungumzo na maafisa wakuu wa usalama Afghanistan

Holbrooke asema juhudi zaidi zinahitajika kukabiliana na wanamgambo wa Taliban.

Mjumbe maalum wa Marekani Richard Holbrooke

Mjumbe maalum wa Marekani Richard Holbrooke


Mjumbe maalum wa Marekani Richard Holbrooke amekua na mazungumzo na maafisa wa ngazi ya juu wa usalama nchini Afghanistan,kujadili uongezaji juhudi za kukabiliana na uasi wa wanamgambo wa Taliban. Na kama anavyoripoti jane Nyingi mshauri huyo wa rais Barack Obama wa marekani amesema uongezeko la mashambulio na wanamgambo hao ni swala linalotia wasiwasi.


Ziara ya bw Holbrooke, inatokea siku moja tu baada ya wanamgambo wa Taliban kujipenyeza katika mji mkuu wa Afghanistan Kabul na kuwaua watu 26 kufuatia mashambulio matatu ya bomu katika majengo ya serikali.


Wachambuzi wanasema huenda wanamgambo wa Taliban walitumia mashambulio hayo kutoa ujumbe kwa Holbrooke kuwa kuwepo kwa karibu wanajeshi elfu 70 wa kimataifa nchini Afghanistan hakujasadia kwa vyoyote kurejesha kuwa ya kawaida nchini humo.


Taarifa kamili kuhusu ziara ya mjumbe huyo wa Marekani nchini Afghanistan na Pakistan haijatolewa lakini anatarajiwa kufanya mazungumzo pia na maafisa wa ngazi ya juu wa kimataifa nchini humo na rais Khamid Karzai ambaye uhusiano wake na Marekani unakabiliwa na matatizo.


Mwakilishi maalum mpya wa Uingereza nchini Afghanistan na Pakistan na balozi wa sasa wa Uingereza nchini Afghanistan Sir Sherad Cowper Coles pia wako mjini Kabul. Huku Holbrooke akiendelea na mazungumzo, maafisa wakuu wa Afghanistan ameripoti kuwa watoto watano wameauwa kufuatia makabiliano kati ya wanamgambo hao na majeshi kusini mwa nchi hiyo. Mwanajeshi mmoja pia aliuwawa katika kisa chengine tofauti. Hali hii imewatia wasiwasi raia raia wengi nchini humo. Mkaazi mmoja wa Kabul alisema


“Watoto wangu wanapokwenda shule nawaambia wajitahadhari na maeneo yenye shughuli nyingi na pia wasipite karibu na majengo ya serikali. Hali hii ni ya kutia wasiwasi”


Idadi ya raia wanaouawa kufuatia makabiliano kati ya wanagambo wa Taliban na majeshi ya kimataifa imeendelea kuongezeka. Ziara hiyo ya Holbrooke katika ukanda huo ilimpelekea Pakistan na anatarajiwa kusafiri hadi India, chini ya mpango wa serikali ya rais Obama kuangazia mapigano katika Asia Kusini.


Holbrooke ambaye anafahamika kwa kufanikisha kumalizwa kwa mapigano nchini Bosnia amekiri kuwa anakabiliwa na kibarua kigumu nchini Afghanistan kuliko hata Iraq.


Mashambulizi nchini Afghanistan yameongezeka tangu majeshi ya marekani kuingia nchini humo kukabiliana na wanamgambo wa Taliban mwaka 2001. Kwa mujibu wa ripoti ya umoja wa matiafa karibu watu elfu 5 wamefariki wakiwemo raia elfu mbili katika mapigano hayo mwaka jana.


Rais Obama anatarajiwa kuamua iwapo atume wanajeshi zaidi wa marekani nchini Afghanistan.Maafisa wa kijeshi wanasema huenda kati ya wanajeshi elfu 15 hadi 30 zaidi wakapelekwa kusini mwa Afghanistan,ambako uasi wa wanamgambo wa Taliban umeongezeka na wilaya kadhaa hazipo chini ya usimamizi wa serikali.


Holbrooke amesema anaitumia ziara hiyo kusikiliza na kuelewa mambo kabla ya kumfahamisha rais Obama na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Bibi Hillary Clinton kuzingatia hatua zinazopaswa kuchukuliwa.
 • Tarehe 13.02.2009
 • Mwandishi Jane Nyingi/ AFPE..Picha AFP
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Gtiz
 • Tarehe 13.02.2009
 • Mwandishi Jane Nyingi/ AFPE..Picha AFP
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Gtiz
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com