1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hofu ya utekwaji wa wasichana wa Chibok yarejea Nigeria

21 Februari 2018

Zaidi ya wasichana 90 wa shule wanahofiwa kupotea baada ya watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram kuvamia shule katika kijiji kimoja kaskazini mashariki mwa jimbo la Yobe huko Nigeria.

https://p.dw.com/p/2t65Y
Abubakar Shekau
Picha: picture alliance/AP Photo

Iwapo kupotea kwao kutathibitishwa huo ndio utakuwa utekaji nyara mkubwa zaidi uliofanywa na Boko Haram tangu mwaka 2014 ambapo wasichana 270 wa shule kutoka mji wa Chibok walipotekwa nyara.

Tukio hilo lililofanyika Jumatatu hofu ya kujirejelea kwa lile tukio la utekwaji nyara wa wasichana wa Chibok imeibuka na Jumatano wazazi 50 walikusanyika katika shule hiyo kutaka taarifa zaidi kuhusiana na watoto wao.

Watu wawili ambao wana ufahamu mzuri wa utekaji huo waliliambia shirika la habari la Reuters kwamba usimamizi wa shule hiyo ulipokuwa unafanya uchunguzi wa kawaida wa idadi ya wanafunzi waliopo walipata kwamba wasichana 91 hawakuwepo.

Shule hiyo imefungwa kwa sasa

Shirika la habari la Reuters halikuweza kuthibitisha iwapo boko haram ndio waliohusika katika tukio hilo la utekaji hapo juzi. Polisi ya Nigeria na wizara ya elimu ya jimbo hilo imekanusha madai ya utekaji nyara wowote ule ila wazazi na mashuhuda wengine wamesema baadhi ya wasichana hawajulikani walipo.

Tschad Boko Haram greift Ngouboua an
Uharibifu unaofanywa na Boko Haram katika vijiji kaskazini mwa NigeriaPicha: Reuters/M. Nako

Waziri wa elimu wa jimbo la Yobe Mohammed Lamin amesema shule hiyo imefungwa.

Waliozungumza na Reuters walitoa taarifa hiyo ingawa hawakutaka kujitambulisha kwasababu walionywa na maafisa wa usalama wa Nigeria na maafisa wa serikali wasifichue kupotea kwa wasichana hao.

Duru zinaarifu ya kwamba wanamgambo hao waliwasili katika kijiji hicho wakiwa kwenye malori wengine wakiwa wamejihami kwa bunduki huku wakiwa wamevalia magwanda ya kijeshi. Walianza kufyatua risasi na kuwapelekea walimu na wanafunzi kukimbilia maisha yao.

Waliotekwa nyara Chibok wengine walitoroka

Serikali ya Nigeria inadaiwa kuanza harakati za kuwatafuta wasichana hao wasiojulikana waliko.

Zaidi ya watu 20,000 wameuwawa na zaidi ya milioni mbili wamelazimika kuyakimbia makaazi yao kaskazini mashariki mwa nchi hiyo iliyo na idadi kubwa ya watu barani Afrika tangu Boko Haram lilipoanza uvamizi wake mwaka 2009.

Nigeria 21 Chibok-Mädchen
Baadhi ya wasichana waliotekwa nyara Chibok mwaka 2014Picha: Picture-Alliance/Sunday Aghaeze/Nigeria State House via AP

Kati ya wasichana 270 waliotekwa nyara katika shule huko Chibok Aprili mwaka 2014 karibu 60 walitoroka baadae na baadhi wameachiwa baada ya maelewano baina ya serikali na kundi hilo la kigaidi.

Mwezi uliopita magaidi hao walitoa ukanda wa vidio ulioonesha baadhi ya hao wasichana wa Chibok ambao bado wamezuiliwa wakisema hawataki kurejea nyumbani.

Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/AFPE

Mhariri: Yusuf Saumu