1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hillary Clinton aanzisha vuguvugu jipya

Yusra Buwayhid
17 Mei 2017

Hillary Clinton amezindua vuguvugu jipya "Onward Together" linalomaanisha Twasonga Mbele Pamoja kuyasaidia makundi yanayohamasisha masuala ya siasa na yanayopinga uongozi wa Trump.

https://p.dw.com/p/2d4cH
USA Hillary Clinton in Capitol Hill
Picha: picture-alliance/newscom/K. Dietsch

Kushindwa kwa Clinton katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa Marekani uliopita, inasemekana kumemlazimisha ajitathmini tena ili kuitambua nafasi yake katika uwanja wa kisiasa unaobadilika.

Tangazo hilo limethibitisha kurudi kwa Clinton katika uwanja wa siasa kufuatia kushindwa kwake katika uchaguzi uliopita na chama cha Republican cha Rais Donald Trump mwezi November 2016.

"Katika miezi michache iliyopita, nimekuwa nikitafakari, nikitumia muda wangu kuwa karibu na familia yangu, na ndio, nilikuwa nikitembea msituni, " mgombea wa zamani wa chama cha Democrati Clinton ameandika katika mfululizo wa Tweets wakati akitangaza habari yake hiyo.

"Sasa hivi kuliko wakati mwengine wowote, naamini ushirikiano wa raia ni muhimu kwa demokrasia yetu. Nimehamasishwa sana na kila mtu aliyejitokeza kusaidia katika maandalizi na kutoa uongozi," alisema Clinton.

"Mwaka huu haukuwa vile nilivyotarajia, lakini bado najua ni kitu gani ninachokipigania: Marekani yenye moyo mwema, na inayoshirikisha kila mtu. Tunaendelea mbele" aliongeza.

Mwamvuli wa makundi yote

Screenshot onwardtogether | Hillary Clinton
Tovuti ya vuguvugu la Hillary Clinton "Onward Together"

Clinton ametaja makundi matano ambayo vuguvugu lake litayasaidia, ikiwa ni pamoja na kundi la Indivisible, ambalo lengo lake kuu ni "kumpinga Trump," shirika lenye misimamo mikali linaloitwa Color of Change pamoja na programu inayoongoza ya mafunzo ya wanawake wa chama cha Democrat, Emerge America.

Run for Something, kundi linalowasaidia vijana kugombea nafasi za kisiasa, na Swing Left, kampeni inayowasaidia Wademocrat kurejesha ushindi katika Baraza la Wawakilishi katika uchaguzi wa katikati ya muhula 2018, pia yatapata msaada kutoka kwa vuguvugu la Clinton la Onward Together.

"Wakati mwingine, tutatoa msaada wa kifedha wa moja kwa moja kwa mashirika haya," ameandika Clinton katika barua pepe kwa wafuasi wake hapo Jumatatu, kulingana na vyombo kadhaa vya habari vya Marekani.

"Kwa wengine, tutawasaidia kwa kukuza kazi zao and kufanya kila tuwezalo kuwasaidia kuendelea kukuza idadi ya wafuasi wao na kukuza uwezo wao wa kuwafikia watu zaidi." Kufuatia tangazo hilo, shirika la Run for Something limeandika Jumatatu kwamba wanashukuru sana "kuwa na Hillary Clinton katika timu yao."

Kitabu cha kushindwa

Washington Senat Aussage FBI Director James Comey
Aliyekuwa Mkurugenzi wa FBI, James ComeyPicha: Reuters/K. Lamarque

Clinton kwa sasa pia anaandika kitabu kuhusu kushindwa kwake, ambacho kinatarajiwa kuuzwa katika maduka ya vitabu baadaye mwaka huu.

Pia ameonekana katika hafla kadhaa za umma tokea kushindwa kwake, na mapema mwezi huu alisema kuwa angekuwa rais isisngekuwa kwa mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), James Comey, ambaye muda mfupi kabla ya uchaguzi alitangaza kuwa shirika lake linafungua upya uchunguzi dhidi yake unaohusu utumiaji wake wa anuani binafsi ya barua pepe kwa mawasiliano ya kikazi.

Trump wiki iliyopita alimfuta kazi Comey, ambaye kwa wakati huo alikuwa akiongoza uchunguzi mwingine wa madai ya kuwepo uhusiano kati ya timu ya kampeni ya rais Trump na Urusi.

Mashirika ya upelelezi ya Marekani yamesema kwamba Urusi ilidukua barua pepe za msimamizi wa kampeni ya Clinton John Podesta na kuzivujisha katika jitihada zao za kushawishi uchaguzi wa Marekani.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afp/dpa/DW

Mhariri: Iddi ssessanga