1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hertha yatoka sare na Dortmund

Bruce Amani
15 Oktoba 2016

Hertha Berlin ilitoka sare ya 1-1 ugenini na Borussia Dortmund na kubakia katika nafasi ya pili katika Bundesliga nyuma ya viongozi Bayern Munich

https://p.dw.com/p/2RGC7
Bundesliga - Borussia Dortmund v Hertha BSC
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Meissner

Wageni walikuwa kifua mbele kupitia bao safi la kisigino la, Valentin Stocker, katika dakika ya 51 kabla ya, Pierre-Emerick Aubameyang, ambaye mapema alipoteza penalti, kusawazisha katika dakika ya 80.

Chipukizi wa Dortmund, Emre Mor, alikula kadi nyekundu kwa kulipiza kisasi na kisha, Stocker, pia akatimuliwa uwanjani katika dakika ya mwisho. Bao la kuwasiza la Dortmund liliwapa rekodi ya klabu kucheza mechi 25 mfululizo bila kushindwa katika ligi, lakini wanasalia katika nafasi ya tatu katika orodha ya timu pointi moja nyuma ya Hertha.

Vijana hao wa mji mkuu, wako nyuma ya viongozi Bayern kwa pengo la pointi mbili, ambao wanaweza kuimarisha uongozi wao watakapocheza ugenini leo dhidi ya Eintracht Frankfurt.

Kocha wa Dortmund, Thomas Tuchel, alilazimika kufanya mabadiliko matano kutokana na majeruhi. Mikel Merino, alianza mchezo kwa mara ya kwanza katika safu ya ulinzi wakati Mario Goetze, Emre Mor, Felix Passlack na Marcel Schmelzer walirejea uwanjani. Gonzalo Castro, Raphael Guerreiro, Lukasz Piszczek na Sokratis walikuwa nje. Ousmane Dembele alikuwa kwenye benchi tu.

Kiungo wa Dortmund Sebastian Rode amesema "hatujawahi kucheza pamoja hivyo. Tunafahamu kuwa sote tunaweza kuimarika."

Dortmund waliutawala mchezo katika kipindi kizima cha kwanza, lakini bila kuwa na nafasi zozote za wazi za kufunga bao la Hertha.

"Ulikuwa mchezo mzuri kwa mashabiki,” kocha wa Hertha, Pal Dardai, aliiambia televisheni ya Sky. "Huo ulikuwa mpira wa mwanamme, mapambano makali, nnapenda hivyo”. Aliongeza kocha huyo ambaye wakati mmoja alikuwa kiungo mpambanaji.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Yusra Buwayhid