Herrmann:Mazungumzo ya Umoja wa Ulaya na Uturuki yakome | Uchaguzi wa Ujerumani 2017 | DW | 05.09.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Ujerumani Yaamua

Herrmann:Mazungumzo ya Umoja wa Ulaya na Uturuki yakome

Joachim Herrmann, mgombea ukansela wa Ujerumani wa chama cha Christian Social Union, CSU, ameukosoa msimamo wa kibaguzi wa chama cha Mbadala kwa Ujerumani, AfD, katika mahojiano maalumu na DW.

Kwa kuzingatia hali ya wasiwasi na mivutano iliyoshuhudiwa hivi karibuni kati ya Ujerumani na Uturuki, waziri wa mambo ya ndani ya jimbo la Bavaria, Joachim Herrmann, wa chama cha CSU anataka sera ya wazi kumhusu rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan. "Sisi katika chama cha CSU bila shaka tunaunga mkono kukomeshwa kwa mazungumzo kuhusu Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya," alimwambia Mhariri Mkuu wa DW, Ines Pohl, na muongazaji matangazo, Jaafar Abdul-Karim.

Akiwa wakili, Hermann pia anasema serikali ya Ujerumani inatakiwa kutetea malipo ya Umoja wa Ulaya kwa Uturuki yakome. "Kutokana na mkwamo wa sasa na serikali ya Uturuki, hakuna sababu kwa Umoja wa Ulaya kutuma mabilioni ya euro kwa serikali ya Uturuki mwaka baada ya mwingine kuhusiana na azma ya kutaka kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya katika siku za usoni." Wakati huo huo, alisema Ujerumani lazima iendelee kuwasiliana na Uturuki, wakati wowote Erdogan atakapokuwa si rais tena wa Uturuki. Mkataba kuhusu wakimbizi kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki unatakiwa uendelee kutekelezwa, alisema.

'Mipaka ya wazi hainipendezi'

Mgombea huyo ukansela wa chama cha CSU alirudia tena wito wake kutaka wakimbizi wapya hadi 200,000 kwa mwaka waruhusiwe kuingia Ujerumani kama kikomo. Aliikosoa sera ya kansela Merkel ya milango wazi ya miaka miwili iliyopita, akidokeza kwamba hakuwa na shauku kuhusu kuikubali sera hiyo lakini katika miezi iliyofuata jimbo la Bavaria hususan, lilikuwa limefanya mengi kuwasajili na kuwajumuisha wakimbizi katika jamii.

Herrmann pia alitetea kusitishwa kwa haki za familia kuunganishwa tena kwa wakimbizi wengi. "Kulikuwa na wakati ambapo watu walijaribu kwanza kuhakikisha familia zao zinakwenda katika maeneo salama kabla kuhakikisha wao wenyewe wako salama. Lakini sasa ni vijana wanaojihakikishia usalama wao wenyewe na baadaye kujaribu kutafuta mbinu kuwawezesha wake zao na watoto wao wajiunge nao. Ndipo swali linajitokeza, na hili pia ni suala nyeti kwa Ofisi ya Shirikisho inayoshughulikia Uhamiaji na Wakimbizi, ni nani ambaye kimsingi anakabiliwa na kitisho?"

Deutschland wählt DW Interview mit Joachim Herrmann (DW/R. Oberhammer)

Joachim Herrmann, kulia, akihojiwa na Mhariri Mkuu wa DW, Ines Pohl, katikati na Jaafar Abdul Karim

Serikali ya Ujerumani kwa kiwango cha wastani ilizibana sheria za kuzijumuisha familia za wakimbizi mnamo mwezi Machi mwaka 2016. Tangu wakati huo kuzijumuisha familia za wakimbizi kumesitishwa kwa wale wanaokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe, lakini si kwa watu binafsi wanaoteswa. Herrmann aliiambia DW anataka kuona hilo likiendelea.

'Chama cha AfD ni cha ubaguzi'

Herrmann alichukua msimamo wa wazi kabisa dhidi ya chama cha Mbadala kwa Ujerumani cha siasa za mrengo wa kulia, AfD. "Hatuhusiki kabisa na ubaguzi wa chama cha AfD," alisema. "Chama cha AfD hakina uwezo wowote kuhusiana na usalama wa ndani. Wanazungumza sana lakini kwangu mimi kuzungumza tu hakuna umuhimu."

Kwa mujibu wa matokeo ya tafiti za maoni za hivi karibuni, chama cha AfD kimejikingia takriban asilimia 10 ya uungwaji mkono. Kiunzi cha kuwa na viti katika bunge la Ujerumani, Bundestag, ni asilimia 5.

Kujiunga na Merkel katika kisiwa cha jangwani

Kuna uwezekano Herrmann akawa waziri mpya wa masuala ya ndani wa serikali ya shirikisho, kuchukua nafasi itakayoachwa na waziri wa sasa, Thomas de Maiziere, wa chama cha Christian Democratic Union, CDU. Hata hivyo Herrmann, ambaye anashikilia wadhifa huo katika jimbo la Bavaria, anajiweka kando na tetesi hizo. "Sitobashiri kuhusu nyadhifa za baraza la mawaziri," alisema.

Mwenyekiti wa chama cha Christian Social Union, CSU, ambaye pia ni waziri mkuu wa jimbo la Bavaria, Horst Seehofer, inasemekana anataka Herrmann awe waziri wa mambo ya ndani wa serikali kuu mjini Berlin kama njia ya kuitia kishindo sera ya Merkel kuhusu wakimbizi, ambayo chama cha CSU kwa ujumla kwa muda mrefu kimeiona kuwa na mapungufu na kuikosoa.

Licha ya Herrmann kuwa na uhusiano mzuri na kansela Merkel, kwa haraka alimchagua kansela huyo kati ya wagombea wengine wa ukansela wa vyama mbalimbali, kama mtu pekee anayeweza kukwama naye katika kisiwa cha jangwani. Alimueleza, Merkel, Mkuu wa chama cha CDU kama "mwanamke mwerevu."

Mwandishi:Thurau, Jens (DW Berlin)

Tafsiri: Josephat Charo

Mhariri:Iddi Ssessanga

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com