Heiko Maas asema Ujerumani ina wajibu mkubwa kimataifa | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.01.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Heiko Maas asema Ujerumani ina wajibu mkubwa kimataifa

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani amekutana na mwenzake wa Urusi mjini Moscow kwa mazungumzo yaliyolenga moja kwa moja juu ya bomba la gesi, mizozo ya Ukraine na Syria, na mkataba wa atomiki wa enzi za Kisovieti.

Maas amemweleza waziri mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov kwamba Ujerumni "itakuwa na wajibu mkubwa kimataifa mbele yake ", akimaanisha taifa hilo litakapoketi katika kiti kisicho cha kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa miaka miwili ijayo. Urusi ni moja ya wanachama watano wa kudumu kwenye baraza hilo.

Marekani ambayo ni mwanachama mwingine wa kudumu inaituhumu Urusi kwa kukiuka mkataba wa nyukilia wa masafa ya kati INF, uliokuwepo tangu enzi za Kisovieti. Waziri Lavrov wa Urusi ameyaelezea madai ya Marekani kama sababu ya kujiondoa katika mkataba huo. Lavrov amesema Urusi iko tyari kuendelea na majadiliano na Marekani ili kuokoa mkataba huo.

"Licha ya kushindwa, kwa sababu ya tarehe ya mwisho na msimamo wa Marekani, majadiliano yaliyofanyika kati ya wataalamu wa Urusi na Marekani huko Geneva tarehe 15 Januari, bado tuko tayari kuendelea na mazungumzo ya kitaaluma, tukiwa na tariifa zote kujaribu kuokoa mkataba huu muhimu, ambao unatoa kiwango kikubwa cha utulivu," alisema Lavrov.

Russland Sergej Lawrow & Heiko Maas in Moskau (picture-alliance/dpa/K. Nietfeld)

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov

Marekani imeipatia Urusi muda wa hadi Februari mwanzoni ili iweze kuharibu hifadhi hiyo. Urusi awali ilishutumu madai hayo, ikisema makombora yake hayajaribiwa ndani ya masafa ya kilometa 500 hadi 5,500. Mwezi uliopita ilitangaza kwamba imefanya jaribio la kombora la kwenye ardhi kutoka kituo kimoja kusini mwa milima ya Ural na kulenga kilometa 6000 kaskazini mwa mkoa wa Kamchatka.

Mawaziri hao pia wamegusia hali katika mlango bahari wa Kerch. Mnamo Novemba 25, vikosi vya mpakani vya Urusi vilizikamata meli tatu za vikosi vya majini vya Ukraine katika eneo la mlango bahari wa Kerch.

"Urusi na Ukraine wanawajibika kuhakikisha kwamba tunasonga mbele na muundo wa usitishaji halisi wa mapigano. Hali katika Bahari ya Azov, kila kitu kilichotokea hapo, ilikuwa sababu ya wasiwasi. Hatutaki migogoro mipya huko. Sehemu huru ya kupita meli ni lazima itolewe. Mgogoro uliotokea mnamo Novemba haupaswi kutokea tena. Kwa kusudi hili, tunahitaji ufafanuzi katika siku zijazo. Kinachotokea sasa, meli ziko huru kupita, hicho kinapaswa kuwa msingi wa kudumu", alisema Maas.

Maas alitarajiwa kukutana na waziri mwenzake wa Ukraine Pavlo Klimkin mjini Kiev baadae Ijumaa  katika jitihada za kusaka suluhu katika mzozo wa nchi hiyo na waasi wa Kirusi karibu na mpaka na Ukraine.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpa/Afp

Mhariri: Saumu Yusuf

 

 

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com