1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Hatuogopi tena": Kiongozi wa upinzani Belarus ahimiza Umoja

Sekione Kitojo
23 Agosti 2020

Kiongozi wa upinzani nchini Belarus Svetlana Tikhanovskaya amewataka  waandamanaji  wanaodai demokrasia kuendelea na juhudi hizo, akisema  rais Alexander Lukashenko hana "chaguo" ila kuzungumza na upinzani.

https://p.dw.com/p/3hMoW
Belarus Minsk | Proteste gegen Präsident Lukaschenko
Picha: Getty Images/AFP/S. Gapon

Katika  mahojiano  na  shirika  la  habari  la  AFP, Tikhanovskaya pia  amesema   watu wa Belarus  wameondoa  hofu yao  na kuiita hatua ya Lukashenko  ya kuongeza  usalama katika  mipaka  kuwa ni  juhudi tu za kutaka "kuondoa mtazamo katika matatizo yetu ya ndani".

Belarus | Proteste gegen Präsident Lukaschenko
Watu wakishiriki maandamano kupinga matokeo ya uchaguzi BelarusPicha: AFP/S. Gapon

"Najisikia fahari sana na Wabelarusi hivi sasa kwasababu  baada ya  miaka  26 ya hofu wako tayari  kulinda  haki zao," alisema  mjini Vilnius , ambako alikimbilia baada  ya  uchaguzi  hapo Agosti  9 ambao anadai kupata  ushindi.

"Nawataka  kuendelea, sio kuacha, kwasababu  ni muhimu  sana hivi  sasa  kuendelea  kuwa  na  umoja  katika  mapambano  kwa ajili ya  haki," alisema, akizungumza  katika  mkesha  wa  maandamano makubwa  yanayotarajiwa  nchini  Belarus siku  ya  Jumapili.

Wapinzani  wa  kiongozi  huyo  aliyekuwapo madarakani kwa  muda mrefu  zaidi  barani  Ulaya  wametayarisha  migomo na maandamano  makubwa  katika  taifa  hilo  la zamani  wa  Umoja  wa Kisovieti  katika  historia  ya  hivi  karibuni kupinga  kuchaguliwa kwake  tena  na  wanadai kuwa  ajiuzulu.

Lithauen Vilnius | Sviatlana Tsikhanouskaya
Kiongozi wa upinzani Belarus Svetlana TikhanovskayaPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Kulbis

Hatuwaogopi

"Wanapaswa kuelewa kuwa  sisi  sio vuguvugu  la  maandamano. Sisi ni  watu wa Belarus na tuko wengi  na  hatutakaa kando. Hatuwaogopi  tena;" Tikhanovskaya aliliambia  shirika  la  habari  la AFP.

Mwalimu huyo wa zamani wa  somo  la  Kiingereza na mwanagenzi katika  siasa , mwenye umri wa miaka 37 , Tikhanovskaya  alijiunga tu  katika  jukwaa  la  kisiasa   wiki  kadhaa  kabla  ya  uchaguzi baada  ya  mume  wake ambaye  huandika taarifa katika  blog alipozuiwa  kujiandikisha  kuwa  mgombea  wa  rais.

Hakutoa  maelezo juu  ya  kwanini  aliondoka  Belarus baada  ya uchaguzi lakini  alisema  alifanya hivyo kwa  ajili  ya  watoto wake na waungaji  wake  mkono wanasema  alikabiliwa  na  shinikizo  kubwa kutoka  kwa  maafisa  wa  Belarus. Ametoa  wito  wa  uchaguzi mpya  na  kusema  hana  mpango wa  kugombea  katika  uchaguzi wowote  hapo  baadaye.

Minsk | Auftritt Lukaschenko Unabhängigkeitsplatz
Alexander Lukashenko rais wa BelarusPicha: Imago Images/ITAR-TASS/V. Sharifulin

Tikhanovskaya  pia  ameteua  baraza  la  uratibu ambalo  anataka kujadili "makabidhiano ya amani  ya  madaraka" lakini chombo  hicho cha  upinzani kinachunguzwa nchini  Belarus  kuwa  ni  jaribio lisilo halali kisheria  kumuondoa  madarakani  rais Lukashenko.

Alipoulizwa  kitu  ambacho  kinaweza  kumsukuma Lukashenko kufanya  majadiliano  na  upinzani , alisema: "Nafikiri hana chaguo." Lakini  alisema  kwamba  majadiliano  yanapaswa  kuanza haraka iwezekanavyo "ili  kutoruhusu mzozo  huu  kuwa  mkubwa zaidi".