1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatuhitaji kuwa na Salah Kikosini - Gernot Rohr

11 Juni 2018

Mchezo mzuri wa Nigeria umewafanya mashabik waanze kufikiria kuhusu ushindi wa Kombe la Dunia. Kocha Mkuu wa Nigeria Gernot Rohr alizungumza na DW.

https://p.dw.com/p/2zJFl
Gernot Rohr
Picha: picture-alliance/ZUMA Press/K. Galvin

 

DW: Nigeria ilikuwa na kazi rahisi katika mechi za kuwania kufuzu na walishinda mechi ya kirafiki dhidi ya mabingwa mara mbili wa dunia Argentina baada ya kuwa chini 0-2. Je, tutaiona Nigeria ile ile yenye nguvu kwenye Kombe la Dunia?

Gernot Rohr: Iwapo unaweza kushinda katika mechi ya kirafiki, unaanza kuamini kwamba unaweza kufanya hivyo tena katika mashindano. Kwa hiyo tuna imani ingawa hatuna mori na tunamwambia kila mtu Nigeria: Msisahau kwamba sisi ndio timu changa zaidi katika mashindano haya.

 

Hali ikoje Nigeria kwa sasa?

Kila mmoja ana furaha. Tulipofuzu mwezi Oktoba Zambia, kulikuwa na sherehe kubwa kote nchini. Furaha ilikuwa kubwa mno kiasi cha kwamba hatukuweza kuondoka uwanjani kwa masaa machache, kwasababu watu walikuwa wanataka kusherehekea na sisi. Ilikuwa vizuri kuona hali kama ile.

 

Je hisia hizi kuu ni motisha au mzigo mbele ya kombe la dunia?

Kawaida kuna shinikizo kila kwa wakati kwa wachezaji wanaocheza England, Ujerumani au nchi zengine za Ulaya. Bila shaka ni shinikizo kubwa zaidi kuichezea Nigeria kwasababu kuna watu milioni 200 wanaokutaka ushinde. Lakini nafikiri tulionyesha katika mechi za kuwania kufuzu kwamba tunaweza kuhimili shinikizo katika mechi muhimu. Kwa sasa tunacheza dhidi ya Croatia (katika mechi yetu ya kwanza) na wao, kama timu inayotarajiwa kufanya vyema, ndio watakaokuwa na shinikizo. Sisi ndio timu ndogo.

 

Ulisema kwamba "Super Eagles" wanahitaji nidhamu ili wafuzu kutoka kwenye hatua ya makundi. Je, hili ndilo lengo lako?

Mfumo wa mchezo wa soka wa Afrika ni kutumia nafasi vyema na kujilinda lakini wakati mwengine unapaswa kusahau kuhusu nidhamu na kujipanga katika safu ya ulinzi. Mimi ni Mjerumani na Mfaransa, kwa hiyo nafikiri hiyo nidhamu ni sehemu ya jinsi ninavyofikiria na naweza kujaribu kuwafunza, hasa wale wachezaji wadogo: Kufanya kila kitu kwa wakati na kutolala kuchelewa, kwa mfano. Mambo madogo. Tuna bahati kwamba timu nzima imekuwa Ulaya kwa hiyo tayari wana elimu kuhusu jinsi ya kujilinda katika mipira ya frikiki na kona. Wamejifunza pia kuhusiana na nidhamu ya kimbinu na pia kuchezea timu badala ya kujichezea wao wenyewe.

 

Kocha wa zamani wa Cameroon, Togo na Ivory Coast Otto Pfister, aliiambia DW kwamba damu ya Super Eagles iko moto sana na hawawezi kufika mbali katika kombe la dunia.

Damu moto inamaanisha nini? Tuna wachezaji wanaokuja kwetu kutoka nchi tofauti. Kutoka Uturuki, Italia, kutoka Uhispania, kutoka Uingereza, kutoka Ujerumani na kutoka Nigeria, kwa hiyo wanaleta njia tofauti za kufikiria. Hatuna cha kupoteza. Iwapo hatutafuzu kutoka kwenye hatua ya makundi, si kwasababu damu yetu ni moto mno, bali ni kwasababu timu zengine zinacheza mpira bora kutushinda. Kwangu mimi haina maana kusingizia sababu zengine.

 

Umesema hakuna wachezaji nyota katika kikosi cha Super Eagles'. Utafanya nini kuwa na Mohammed Salah wa Nigeria?

Nafikiri ni vizuri sana kwa Misri kuwa na mchezaji kama huyo, kama vile tu Argentina walivyo na Messi na Croatia walivyo na Modric. Lakini badala yake, sisi tuna ushirikiano mzuri baina yetu. Ushirikiano mzuri ndilo jambo muhimu na wala sio uzuri wa mchezaji mmoja hata ikiwa huyo mchezaji ni mzuri vipi. Hili ni jambo muhimu sana kuliko Mohammed Salah mmoja.

Fussball African Cup 2017 - Nigeria - Nationaltrainer Gernot Rohr
Kocha wa Super Eagles Gernot RohrPicha: Getty Images/AFP/P. U. Ekpei

 

 

Zaidi ya asilimia 90 ya wachezaji wako wanacheza mpira nje ya Nigeria. Kuna ugumu gani wa kuleta ushirikiano mzuri katika timu?

Sihitaji kuuleta huo ushirikiano mzuri. Tayari tunao huo ushirikiano kwasababu kila mmoja ana furaha kuja na kuichezea Nigeria na kuziwakilisha rangi za kijani na nyeupe, Na uwanjani hatuna wasiwasi. Kwa kawaida hakuna muda mwingi kwa hiyo hua natumia mbinu rahisi ambazo wachezaji wote wanaweza kuzielewa kutoka kwenye vilabu vyao.

 

Je unaona kuna mustakabali wa timu ya taifa ya Nigeria iliyo na wachezaji wanaocheza soka ya klabu Nigeria?

Tayari tuna wachezaji wawili au watatu kutoka vilabu vya Nigeria katika timu ya taifa. Na timu yetu ya CHAN, ambayo ilikuwa imejuisha wachezaji wa nyumbani, ilifika fainali Morocco.

Kwa upande mwengine, vilabu nchini Nigeria si vizuri zaidi kutoa timu nzima ya wachezaji wanaoweza kushindana na wale waliopewa mafunzo Ulaya.

 

Hilo litabadilika?

Kwa hili vilabu vinahitaji miundo mbinu bora. Hawana viwanja vizuri na hawana shule za mafunzo ya soka. Kwa sasa, timu ya taifa inaweza kucheza Uyo na Port Harcourt pekee - Hatuwezi hata kucheza Abuja kwasababu hakuna uwanja mzuri. Tunahitaji maendeleo.

 

Je, ni wakati wa timu ya Afrika kushinda kombe la dunia?

Nataraji kwamba timu ya taifa siku moja itashinda kombe la dunia. Timu zote kila mahali zinajitahidi kushinda. Nigeria tunataka kujipangya vyema ili tusiyafanye yale makosa ya zamani. Kwa mfano tulifikia maelewano na maafisa wa soka wa Nigeria kuhusu malipo ya wachezaji ili tusiwe na mazungumzo ya dakika za mwisho yatakayoathiri mechi. Kwa sasa tunaweza kuweka fahamu katika mechi.

Tunataka kushinda bila shaka, ila tusiposhinda kwa kuwa timu nyengine ni bora, hilo halitakuwa janga. Wacha tujaribu kustawi. Tuna timu ya wachezaji wenye umri mdogo kabisa katika shindano hili na tutajifunza. Kwa lolote litakalotokea, litakuwa kombe zuri la dunia.

 

Mwandishi: Philip Barth

Tafsiri: Jacob Safari

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman