1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajihadi wa kijerumani watapokonywa Uraia

11 Agosti 2016

Waziri wa mambo ya ndani wa serikali kuu ya Ujerumani,Thomas de Maiziére amefungua mjadala kuhusu kupokonywa uraia wa Ujerumani wanajihadi wanaomiliki uraia wa nchi mbili.

https://p.dw.com/p/1Jggd
Waziri wa Mambo ya ndani Thomas de MaizièrePicha: picture-alliance/dpa/W.Kumm

Akijiibu kitisho kinachotokana na kuongezeka mashambulio ya kigaidi, waziri wa mambo ya ndani wa serikali kuu ya Ujerumani Thomas de Maizière anataka kuwapokonya uraia wa Ujerumani wapiganaji wa itikadi kali wanaomiliki uraia wa nchi mbili :"Nnapendekeza,wajerumani wanaojiunga na wanamgambo wa kigaidi, wanaoshiriki katika mapigano nchi za nje, wanapokuwa na uraia wa nchi ya pili,na hapo tu ndipo inapowezekana, wapokonywe uraia wa Ujerumani."

Amesema waziri de Mazière katika mkutano na waandishi habari mjini Berlin. Jumla ya wanajihadi 820 wameondoka Ujerumani kwenda Syria na Iraq kwa mujibu wa ripoti ya idara ya upelelezi ya Ujerumani iliyochapishwa mwezi wa Mai mwaka huu.

Karibu thuluthi moja kati yao wamesharejea nchini Ujerumani na karibu 140 wameuwawa huku wengine 420 wakiwa bado wanakutikana nchini Syria na Iraq.

Hatua hizo zinabidi ziidhinishwe kabla ya uchaguzi mkuu 2017

Waziri wa mambo ya ndani amekiri atakuwa na kazi ngumu kuwatanabahisha washirika wa chama chake cha kihafidhina serikalini-wana Social Democrat walikubali pendekezo hilo.

Deutschland München nach dem Amoklauf Trauernde
Watu wanaomboleza baada ya mashambulio ya MunichPicha: DW/D. Regev

Hata hivyo anaamini lengo hilo pamoja na hatua nyengine za usalama zitaweza kuidhinishwa kabla ya uchaguzi mkuu msimu wa mapukutiko mwaka 2017.

Mpango wa kuwapokonya wahalifu uraia ulipendekezwa pia Ufaransa baada ya mashambulio ya Novemba 13 mwaka jana-ulishindwa lakini kutokana na mivutano ya kisiasa.

Miongoni mwa hatua zilizopendekezwa na de Maiziere leo hii ni pamoja na kubuniwa chombo kitakachoharakisha mhalifu mwenye asili ya kigeni kurejeshwa katika nchi alikotokea:"Tunataka siku za mbele kuwa na uwezo wa kutumia chombo kinachorahisisha kuwarejesha walikotokea wahalifu wa kigeni na watu wengine wanaotishia kuhatarisha usalama wa jamii."

Idadi ya polisi itazidishwa

Na mwishoe waziri huyo wa mambo ya ndani Thomas de Maizière amesema haungi mkono mpango wa kupigwa marufuku Burka kama ilivyopendekezwa na baadhi ya wanachama wa kihafidhina.

Deutschland Polizeifahrzeuge in München
Polisi wapiga doria mjini MunichPicha: picture alliance/dpa/F. Hörhager

Wakati huo huo,de Maiziere ameshauri izidishwe idadi ya polisi mnamo miaka inayokuja, pamoja na kuwekezwa zaidi katika teknolojia ya mawasiliano ya kimambo leo dhidi ya ugaidi na uhalifu wa mtandaoni.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Caro Robi