1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wavulana waliokolewa Nigeria wakutana na famila zao

18 Desemba 2020

Wavulana waliotekwa nyara tangu majuzi kaskazini magharibi mwa Nigeria wamerudishwa nyumbani leo Ijumaa, kitendawili ambacho hakijateguliwa ni hatima ya wasichana waliotekwa miaka sita iliyopita.

https://p.dw.com/p/3mvnw
Afrika Nigeria Schulkinder freigelassen
Picha: Yusuf Ibrahim Jargaba/DW

Picha kwenye televisheni zinaowaonesha vijana hao wa kiume wakiwa na mavazi yaliyojaa vumbi, huku nyuso zao zikionesha uchovu lakini wakitabasamu wakati wakishuka kwenye mabasi katika mji wa Katsina na kuelekea katika jengo la serikali.

Mvulana mmoja ambaye uso wake ulikuwa umetapakaa matope yaliyokauka, alitabasamu alipoulizwa na mwanahabari mmoja anajihisi vipi kufika Katsina, na kusema: "nimefurahi sana, kulikuwa na baridi", akimaanisha sehemu walipokuwa. soma zaidi Wavulana wa shule waliotekwa Nigeria waachiwa

Mvulana mwengine, ambaye hakutaja jina lake, alisema watekaji waliwacharaza kwa fimbo mara kwa mara, na walijitambulisha kwao kama wanamgambo wa kundi la Boko Haram, ingawa alishuku walikuwa majambazi tu wenye silaha.

Nigeria befreite Schüler in Katsina
Wavulana waliokombolewa na vikosi vya usalama NigeriaPicha: Afolabi Sotunde/Reuters

Walicharazwa

Akihadithia yaliyowasibu, mvulana huyo alisema, "Tuliteseka sana. Walitupa chakula mara moja kwa siku na maji mara mbili kwa siku, na watekaji walitaka niseme ni Boko Haram yakiri kuwateka nyara mamia ya wanafunzi na magenge ya Abu Shekau ndio waliohusika na utekaji."

"Walituficha mahali pamoja wakati walipotuteka nyara mwanzoni, lakini walipoona ndege ya kijeshi, walibadilisha eneo na kutuficha mahali pengine. Walitupatia chakula lakini kilikuwa kidogo sana." alisema mmoja wa vijana hao.

Mmoja wa wazazi wa watoto waliookolewa, alikiambia kituo cha televisheni cha Arise nchini Nigeria kwamba wamefurahi na wanashukuru sana kwamba watoto wao wako salama. Baba huyo ana wavulana wawili miongoni mwa waliokuwa wametekwa.

Nigeria Kankara | Angriff auf Schule | Entführte Schulkinder
Jamaa wa mmoja wa wavulana waliotekwa kaskazini magharibi mwa NigeriaPicha: Afolabi Sotunde/REUTERS

Furaha imewajaa wazazi

Hafsat Fantua, mama wa Hamza Naziru kijana mwenye umri wa miaka 16, amesema hakuamini taarifa za kuokolewa kwa wavulana hao hadi pale jirani yake alipomtaarifu ni kweli. Katika mahojiano kupitia njia ya simu, mama huyo amesema kutokana na furaha alichanganyikiwa na kutoka nje bila ya kujua anapokwenda lakini kisha alirudi ndani na kusali.

Aminu Bello Masari, Gavana wa jimbo la Katsina amesema, "Kwa wanafunzi, hii inapaswa kuwa sehemu ya historia yao, na sehemu ya safari yao hadi utu uzima. Nina hakika hii itakuwa ya kina. Muliteswa ... kimwili, kiakili na kisaikolojia, lakini nawahikisha kuwa tumeteseka zaidi na wazazi wenu pia wameteseka zaidi."  Soma zaidi Lifahamu kundi la Boko Haram

Hata hivyo, kinachosalia kuwa kitendawili kwa sasa ni jinsi watoto hao walivyoweza kuokolewa kwa haraka sana inapolinganishwa na mamia ya wasichana waliotekwa tangu Aprili 2014. Boko Haram iliwateka nyara wasichana 270 kutoka shule ya bweni ya serikali mjini Chibok jimbo la kaskazini mashariki la Borno. Miaka sita baadaye ni chini ya nusu ya wasichana hao waliopatikana au kuachiliwa, huku wengine ikiarifiwa kuwa waliolewa na wapiganaji hao na wengine hawajulikani walipo hadi kufikia sasa.

 

AP/RTRE