1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatimaye Sudan wakubaliana

Lilian Mtono
5 Julai 2019

Viongozi wa vuguvugu linalounga mkono demokrasia nchini Sudan limekaribisha makubaliano yaliyofikiwa mapema hii leo ya kuundwa kwa serikali ya pamoja na baraza la mpito la kijeshi.

https://p.dw.com/p/3Les7
Sudan Karthoum | Demonstranten feiern nach einigung von Generälen und Protestführern
Picha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Wamesema ni ushindi wa mapinduzi waliyoyaanzisha, unaofufua pia matumaini ya kumalizika kwa mvutano wa miezi mitatu na baraza hilo, na kusababisha machafuko mabaya. 

Kwenye taarifa yao mapema hii leo waliyoichapisha kwenye ukurasa wa Facebook wa Jumuiya ya Wataalamu nchini humo, wamesema leo, mapinduzi yao yameshinda na ushindi wao unang'ara.

Kulingana na taarifa ya jumuiya hiyo, pande hizo mbili zimekubaliana kuunda baraza tawala la pamoja kuongoza nchi hiyo katika kipindi cha mpito cha miaka mitatu na miezi mitatu. Alipozungumza baada ya makubaliano hayo, kiongozi wa kundi la Forces of Declarartion of Freedom and Change, FDFC Omer al-Digair alisema "Makubaliano haya yanafungua njia ya kuunda utawala wa mpito utakaziba ombwe la kisiasa, uchumi na hata maisha ya kawaida. Suala litakalopewa kipaumbele na serikali hii ni kurejesha amani na uhuru, na uwazi katika uchunguzi wa wahusika wa mauaji ya mashahidi ili wawajibishwe"  

Sudan Khartoum | Sudans Stellvertretender Leiter des Militärrats - Mohamed Hamdan Dagalo
Makamu wa rais wa baraza la kijeshi la Sudan Mohamed Hamdan DagaloPicha: Getty Images/AFP/E. Hamid

Lakini pia, makamu wa rais wa baraza hilo la kijeshi Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo alisema, "Mkataba huu utakuwa mkamilifu, na hakutakuwa na uonevu dhidi ya mwingine lakini pia utatambua mahitaji ya watu wa Sudan pamoja na mapinduzi yao."

Hata hivyo baadhi ya viongozi wa upinzani hawaridhishwi sana na makubaliano.

Baraza hilo la kijeshi la Sudan litahusisha raia watano wanaowawakilisha vuguvugu la waandamanaji pamoja na wawakilishi watano wa kijeshi. Nafasi ya 11 itakwenda kwa raia atakayechaguliwa na pande zote.

Wanajeshi wataliongoza baraza hilo kwa miezi 21 ya mwanzo na baadae kushikiliwa na raia, hii ikiwa ni kulingana na makubaliano hayo. Taarifa ya jumuiya hiyo imesema pande hizo pia zimekubaliana kuanzisha uchunguzi huru wa pamoja wa kitaifa wa mauaji ya waandamanaji tangu rais Omar al-Bashir alipoondolewa mamlakani, Aprili 11.

Hata hivyo kiongozi mwingine wa FDFC Tarek Abdel Meguid ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, pamoja na hatua iliyofikiwa, lakini hajaridhishwa sana na makubaliano hayo, kwa kuwa hoja ya serikali ya kuundwa kwa serikali ya pamoja ilikwishakataliwa. Kwa mtizamo wake anaona  yamefikiwa mahsusi kwa ajili ya kuzuia umwagikaji mwingine wa damu.

Amesema, wanakutana mchana huu kujadili uwezekano wa kusitisha mpango wa maandamano ya kuadhimsha si ya 40 tangu vifo vya waandamanaji na kufuatiwa na kuanzishwa kwa mgomo wa nchi nzima, Julai 14.