1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatima ya wajerumani 2 watekwanyara

20 Julai 2007

wajerumani 2 waliotekwanyara juzi jumatano nchini Afghanistan bado hakuna taarifa juu yao au ni akina nani waliowanyakua.Wataliban wamekanusha kuhusika.

https://p.dw.com/p/CHAm

Hatima ya wajerumani 2 waliotekwanyara nchini Afghanistan bado haijulikani.Kwa muujibu wa taarifa za wizara ya nje ya Ujerumani, mawasiliano yameanzishwa na ubalozi wa Ujerumani mjini Kabul pamoja na idara zinazohusika za nchi hiyo.Wajerumani hao wanaotumikia kampuni moja katika mkoa wa Wardak, walinyakuliwa adhuhuri ya jumatano.

Duka kubwa liitwalo “Chelsea Supermarket” liko katika kitovu cha mji mkuu Kabul na ni miongoni mwa maduka ya zamani kabisa yaliopo mjini humo.

Tangu miaka 7 sasa, wanunuzi hujipatia hapo mahitaji yao na kama zamani , leo pia wengi wao ni raia wa kigeni.

Taarifa za kutekwanyara kwa wajerumani hao 2 zilipokewa dukani kwa masikitiko na wasi wasi.Mwenyeduka mmoja aitwae Ali asema:

“Nimevunjika moyo,nina huzuni na nimeingiwa na wasi wasi.Kwani, jambo kama hilo likitokea, ukoo huingiwa na hofu na wasi wasi juu ya maisha yao.Isitoshe, visa kama hivi vina arthari zake katika hali ya usalama na uchumi nchini Afghanistan.”

Serikali mjini Kabul na pia Berlin, zinaendelea kukaa kimya.Taarifa chache zilizoibuka ni za kutatanisha.Madai ya watekanyara hayajulikani tena siku 2 tangu kuzuka mkasa huo.Pia hakujajitokeza ama kikundi cha wahalifu au chenye siasa kali kujitwika dhamana ya kitendo hicho.

Wakati Gavana wa mkoa jirani wa Ghasni amewanyoshea kidole watalibani,wao wamekanusha kuhusika .Mabingwa wa usalama wanadhani, hii yamkini ni kazi ya majambazi wanaotapia fedha.

Raia wote wa kigeni waliotekwanyara mwishoe, wakiachwa huru bila kudhuriwa .Mabingwa hao hawalinganishi hali nchini Afghanistan kuwa sawa na Iraq.

Nic Lee, mkurugenzi wa shirika la usalama wa mashirika ya misaada mjini Kabul asema:

“Nchini Afghanistan, utekajinyara haukufikia kiwango cha Irak.Nchini Irak na kwengineko,utekajinyara unafanyika tangu mijini hata mikoani pamoja na miji mikuu.Hali kama hiyo haipo hapa.Wanaonyakuliwa hasa ni wale watu wale wanaotembelea sehemu za kando kabisa na zisizolindwa barabara.

Mimi sioni hapa kampuni la majambazi watekaonyara katika kila pembe ya nchi hii.”

Wahandisi hao 2 wa kijerumani pamoja na wafanyikazi wenzao 5 wa kiafghani, juzi jumatano walikuwapo mkoani Wardak,kiasi cha km 100,kusini-magharibi mwa mji mkuu Kabul walipovamiwa na kunyakuliwa na watu wasiojulikana.Yadhihirika walikuwa katika njia-panda baina ya mji mkuu Kabul na Kandahar.

Gari la polisi lililokuwa likiwalinda katika msafara wao ,lilivuka salama na hakuna polisi aliedhurika.

Haijulikani lakini iwapo, polisi hao walipokonywa silaha na watekanyara na kuambiwa wende zao au walikabidhi binafsi silaha zao na kusalim amri na kutimka mbio.

Kwa desturi,majimbo ya Wardak na Ghasni lakini hasa njia-panda kati ya Kabul na Kandahar, ni ya hatari.Sababu ni kusheheni sehemu hizo kwa wapiganaji wa Taliban na magengi ya majambazi.

Kijana muuza-duka Ali, kwa fahari kabisa aonesha picha za zamani za duka la wazee wake -enzi ya miaka ya 1940- 1950.Anasema hata nyakati za vita vya kienyeji wakati wa utawala wa watalibani biashara ikiendelea.

Lakini, anaongeza, kwa jicho la kuzidihivi sasa matumizi ya nguvu na vya utekajinyara mfano wa kunyakuliwa wajerumani hao 2,ameingiwa sasa na hofu na wasi wasi hasa kwa wanunuzi wake –raia wa kigeni.