Hatima ya mahabusi 2 wa kijerumani nchini Irak | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hatima ya mahabusi 2 wa kijerumani nchini Irak

Muda wa onyo la pili la wateka nyara umeshapita tangu jana usiku

Rais wa shirikisho Horst Köhler akiwasihi wateka nyara kwa njia ya televisheni

Rais wa shirikisho Horst Köhler akiwasihi wateka nyara kwa njia ya televisheni

Muda wa pili wa onyo la watu waliowateka nyara raia wawili wa kijerumani nchini Irak,umemalizika jana usiku.Wateka nyara wanaitaka serikali kuu ya Ujerumani iwarejeshe nyumbani wanajeshi wake toka Afghanistan.

Wateka nyara wametishia,kuwauwa mahabusi hao 2 wanaowashikilia tangu mapema mwezi February- mama mtu mwenye umri wa miaka 61 na mwanawe wa kiume mwenye umri wa miaka 20 ikiwa madai yao hayatatekelezwa.

Hadi dakika hii tulio nayo hakuna habari zozote zinazojulikana kuhusu kisa hicho cha utekaji nyara.

Jana,muda mfupi kabla ya muda uliowekwa kumalizika, serikali kuu ya Ujerumani ilisisitiza kwa mara nyengine tena masharti ya wateka nyara hayatekelezeki.”Ujerumani haitokubali kutiuwa vishindo katika kadhia hiyo” alisema waaziri wa dola katika wizara ya mambo ya nchi za njje Gernot Erler.

Ameongeza kusema tunanukuu:” wanachana wa kamati maalum wanaoshughulikia mzozo huo wanafanya kazi mtindo mmoja ili kupata ufumbuzi wa maana kwa mahabusi hao ambao hatima yao inaisumbua sana serikali kuu.”Mwisho wa kumnukuu waziri wa dola katika wizara ya mambo ya nchi za nje Gernot Erler.

Wanachama wa kamati hiyo maalum inayoshughulikia suala la mahabusi hao 2 wa kijerumani nchini Irak wanakutana tena jioni hii mjini Berlin.”Hatujakata tama,tunataraji na kuamini wako salama”-amesema kwa upande wake msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje Martin Jäger hii leo mjini Berlin.Amesisitiza kamati ya mizozo itafanya kila liwezekanalo ili familia hiyo irejee salama nchini Ujerumani.

Miito kadhaa ya nasaha imekua ikitolewa na wanasiasa mashuhuri wa Ujerumani kuwaomba wateka nyara wasiwadhuru mashabusi hao.Kati kati ya mwezi uliopita rais wa shirikisho Horst Köhler aliwaomba wateka nyara na kusema:“Nakuombeni,waachieni huru haraka bibi Krause na mwanawe.Damu nyingi ya wasiokua na hatia imemwagika nchini Irak.Acheni kumwaga damu.Waachieni mahabusi warejee katika familia zao.Hakuna lengo lolote la kisiasa linaloweza kuhalalisha utekaji nyara au kuuliwa watu wasiokua na hatia.“

Mwito kama huo ulitolewa pia na mwenyekiti wa baraza la kiislam la Ujerumani Islamrat,Ali Kizilkaya aliyesema "kuwateka nyara watu wasiokua na hatia si ubinaadam na wala si uislam."

Bibi huyo na mwanawe walitekwa nyara February sita iliyopita walipokua wakitoka nyumbani kwao nje ya mji mkuu wa irak-Baghdad.Onyo lao la kwanza muda wake ulimalizika March 21 iliyopita na la pili muda wake umemalizika jana usiku.Madai yao ni yale yale wanaitaka Ujerumani iwarejeshe nyumbani wanajeshi wake toka Afghanistan.

 • Tarehe 13.04.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHGI
 • Tarehe 13.04.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHGI
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com