1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hasimu wa Netanyahu naye ashindwa kuunda serikali Israel

Sylvia Mwehozi
21 Novemba 2019

Israel imeingia katika mkwamo zaidi baada ya kiongozi wa chama cha pili Benny Gantz kushindwa kuunda serikali ya muungano, kufuatia uchaguzi wa Septemba na hivyo kupisha njia ya kufanyika uchaguzi mwingine wa tatu. 

https://p.dw.com/p/3TRXY
Arabische Liste empfiehlt Gantz als Israels Premier | Benny Gantz
Picha: Reuters/A. Cohen

Kiongozi wa chama cha Bluu na Nyeupe yani Blue and White party Benny Gantz, amerejesha jukumu lake la kuunda serikali na kuibua uwezekano wa kufanyika uchaguzi wa tatu ndani ya mwaka huu. Kiongozi huyo alikuwa na muda wa siku 28 wa kuunda serikali baada ya waziri mkuu na kiongozi wa chama cha Likud Benjamin Netanyahu naye kushindwa kuiunda serikali.

Rais wa Israel Reuvin Rivlin anatarajiwa kuliarifu na kukabidhi mamlaka kwa bunge mchana huu, hatua itakayofungua milango kwa bunge kutafuta mbunge yeyote katika bunge la Knesset lenye viti 120, kujaribu kutafuta uungwaji mkono ili kuunda serikali, ikiwa ni mara ya kwanza kwa taifa hilo la Israel.

Mbunge yeyote akiwemo Gantz na Netanyahu watakuwa na siku 21, angalau kutafuta uungwaji mkono wa wabunge 61 na kisha kujaribu kuunda serikali ya muungano. Mbunge atakayepata uungwaji mkono kama huo atapewa muda wa siku 14 wa kuunda serikali.

Ikiwa itashindikana kutaitishwa uchaguzi mpya ambao huenda ukafanyika mwezi machi. Gantz amemshukuru rais Rivlin kwa kumuunga mkono na kusema kwamba ataendelea na juhudi za kuunda serikali kwa ajili ya watu wa Israel.

Israel Präsident Reuven Rivlin mit Benny Gantz
Rais wa israel Reuven Rivlin(kulia) na kiongozi wa chama cha Bluu na Nyeupe Benny GantzPicha: Reuter/R. Zvulun

"Hizi ni siku 21 za mwisho ambapo demokrasia ya Israel itakuwa katika mtihani mkubwa. Hata wakati huu nitajitokeza na kutumia rasilimali zote ili mazungumzo yafanyike haraka na kutoa taswira ya matokeo ya uchaguzi na kuunda serikali itakayoiondoa Israel katika mkwamo uliosababishwa na watu walioweka viunzi," alisema Gantz. 

Netanyahuameelezea utayari wake wa kurejea katika majadiliano ya kuunda serikali baada ya jaribio la Gantz kushindwa. Uamuzi wa kiongozi huyo wa chama cha Bluu na Nyeupe ulikuja saa chache baada ya muda wa mwisho aliopatiwa kumalizika usiku wa Jumatano.

Mwanasiasa Avigdor Lieberman ambaye anaonekana kuwa na umuhimu na kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia cha Yisrael Beiteinu, siku ya Jumatano alikataa kuwaunga mkono Netanyahu na Gantz kuwa mawaziri wakuu, akiongeza kwamba wote wawili ni wa kushutumiwa kwa kushindwa kuunda serikali. Tangazo lake lilikuwa ni ishara nyingine ya Israel kuelekea katika uchaguzi. Lieberman ana jumla ya viti nane bungeni na hivyo kushikilia uzani wa madaraka baina ya Gantz na Netanyahu.