Hamas yadai kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na Israel | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hamas yadai kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na Israel

Kundi la Hamas linaloudhibiti Ukanda wa Gaza limesema limefikia makubaliano ya kusitisha mapigano na Israel kufuatia mapigano makali kati ya makundi ya pande zote mbili tangu vita vya mwaka 2014 vya Hamas na Israel.

Khalil al-Hayah, Naibu Mkuu wa Hamas mjini Gaza, amesema wamekubaliana kurejelea makubaliano ya zamani yaliyofikiwa ya kusimamisha mapigano. Katika taarifa yake al Hayah amesema watajitolea kusimamia makubaliano hayo ili mradi tu Israel nayo iwe na nia ya kuyaheshimu makubaliano hayo.

Kulingana na afisa mmoja kutoka Palestina upatanisho kutoka Misri ndio umesababisha uwepo wa makubaliano ya kusitisha mapigano, ambayo hayakwenda mbali na kuimarishah hali ya utulivu kwa pande zote mbili. Aidha Msemaji wa Hamas  Hammad Al-Reqeb,  amesema hawatakubali kushambuliwa na wako tayari kujibu iwapo hilo litafanyika

Gaza - PK von Hamas-Chef Ismail Haniyeh wegen Jerusalem-Status (Reuters/M. Salem)

Kiongozi wa kundi la Hamas Ismail Haniyeh

Huku hayo yakiarifiwa hii leo waziri wa elimu wa Israel Naftali Bennett, ambaye pia ni mwanachama wa Baraza la Mawaziri wa Usalama, amekanusha suala hilo akisema hakuna aina yoyote ya makubaliano kati yao na Hamas. Ameongeza kuwa hali leo ni shwari lakini itategemea ni kitu gani Hamas watakachofanya, amesema kundi hilo likivuruga hali kuwa mbaya hata wao pia wako tayari kujibu.

Awali msemaji wa jeshi la Israel, Jonathan Conricus alisema wanamgambo wa Palestina walirusha makombora na maroketi 100 nchini Israel usiku kucha huku jeshi la Israel likijibu kwa kuripua maeneo kadhaa ya kijeshi katika eneo la pwani lililozingirwa. Majibizano hayo makali yamekuja baada ya zaidi ya wapalestina 100 kuuwawa na wanajeshi wa Israel katika vurugu wakati wa maandamano wiki kadhaa zilizopita. 

Marekani yalaani mashambulizi ya maroketi kutoka Gaza

Jana jioni Marekani iliitisha mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili juu ya mashambulizi ya maroketi kutoka Gaza. Umoja wa Ulaya nao umelaani shambulizi lililofanywa na Palestina. "Mashambulizi dhidi ya raia hayatakubalika kabisa katika hali yoyote ile," alisema msemaji wa Umoja huo Maja Kocijancic.

Gaza ambayo ni makaazi kwa mamilioni ya Wapalestina inakabiliwa na uhaba mkubwa wa msaada wa kiutu kukiwa na upungufu wa umeme na maji huku kiwango cha watu wasio na ajira kikizidi asilimia 40.

USA Washington Donald Trump auf dem Weg nach Nashville (picture-alliance/MediaPunch/CNP/C. Kleponis)

Rais wa Marekani Donald Trump

Hali hiyo imesababishwa na miaka 11 ya mzingiro wa wanajeshi wa Israel. Israel ilianzisha mzingiro huo baada ya Hamas kuidhibiti Gaza mwaka 2007 ikisema ni muhimu ili kulizuwia kundi la Hamas kuishambulia Israel. Hata hivyo wapalestina wamekuwa wakiandamana katika maeneo ya mpakani hivi karibuni wakitaka kusitishwa kwa mzingiro huo na kukubaliwa kurejea Israel walikolazimishwa kutoroka.

Israel ilijibu maandamano hayo kwa mitutu ya bunduki wakiishutumu Hamas kujaribu kuvuka mipaka na kuwashambulia raia wake.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com