1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali za Kongo, Afrika ya Kati zatawala magazeti

4 Januari 2013

Magazeti ya Ujerumani yamechambua zaidi mustakbali wa mazungumzo kati ya waasi wa Seleka na serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati sawa na yale ya waasi wa M23 na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/17Dit
Ramani ya maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa Seleka katika jamhuri ya Afrika kati

Zazeti la Frankfurter Allgemeine linasema Rais Francois Bozizé amebanwa katika wakati ambapo Ufaransa ya Rais Francois Hollande inafuata siasa ya kutoingilia mambo ya ndani ya makoloni yake ya zamani barani Afrika. Kwa maneno mengine Ufaransa, linasema Frankfurter Allgemeine, haifikirii kuingilia kati ili kumuokoa Rais Bozizé na utawala wake.

Gazeti hilo la mjini Frankfurt limezungumzia hotuba ya mwaka mpya ya rais wa Jamhuri ya Afrika Kati, akiwasihi watu "wamuachie akamilishe miaka mitatu iliyosalia" ya muhula wake.

Waasi wa Seleka lakini hawataki kusikia chochote. Ingawa wako tayari kushiriki katika mazungumzo ya amani ya Libreville, lakini wanasema kwa sharti kama yatapelekea Bozizé kung'atuka madarakani.

"Bozizé ameahidi mengi na hakuna alichokifanya," amesema msemaji wa waasi wa Seleka.

Ingawa Ufaransa imezidisha idadi ya wanajeshi wake katika Jamhuri ya Afrika kati, lengo lakini sio kumsaidia rais Bozizé, bali kuwalinda raia wa Ufaransa na Ulaya ikihitajika. Marekani imeufunga ubalozi wake mjini Bangui.

Vyombo vya habari nchini Ufaransa, linaandika Frankfurter Allgemeine, vinahofia hali katika Jamhuri ya Afrika kati isije ikageuka kama ile ya Mali na kuwapatia upenu wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislamu.

Eti yaliyotokea miaka kumi yanarudiwa

Gazeti la Die Tageszeitung limezungumzia pia hali namna ilivyo katika Jamhuri ya Afrika kati. "Vikosi vya Kabila vinasaidia mjini Bangui" ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya gazeti hilo la mjini Berlin

Katika wakati ambapo waasi wa Seleka hawako mbali na mji mkuu Bangui, Rais Bozizé amejipatia uungaji mkono wa wanajeshi kutoka kikosi maalumu cha rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila, linaandika gazeti la Die Tageszeitung linalowanukuu waasi wa Seleka wakisema wanajeshi hao wanafikia 300.

Msemaji wa serikali ya Kongo amethibitisha ripoti hizo, lakini amesema wanajeshi hao watatumikia kikosi cha kulinda amani cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Nchi za Afrika ya Kati.

Uamuzi wa kuingilia kati wanajeshi wa Rais Kabila kumsaidia Rais Bozizé, unazusha hisia nyeti, linaandika Die Tageszeitung linalokumbusha yaliyotokea miaka 10 iliyopita, pale wanajeshi wa Kongo walipopelekwa kwa mara ya kwanza mjini Bangui kumsaidia rais wa wakati ule, Ange Félix Patassé, dhidi ya waasi waliokuwa wakiongozwa na rais wa sasa, Francois Bozizé.

Kiongozi wa zamani wa waasi aliyekuja baadaye kuwa makamo wa rais, Jean-Pierre Bemba, ndiye aliyewatuma wanajeshi hao wakati ule. Gazeti hilo linakumbusha kwamba sasa Jean-Pierre Bemba anashtakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mjini The Hague kwa uhalifu wa vita uliofanywa na wapiganaji wake mjini Bangui.

Ndio kusema mwaka 2002 Bemba amemsaidia Patassé mjini Bangui, na mwaka 2012 Kabila anamsaidia Bozizé, limemaliza kuandika Die Tagezeitung lililowanukuu wakaazi wa Kinshasa wakichambua ripoti ya kutumwa wanajeshi wa Kongo mjini Bangui.

Hatima ya mazungumzo ya amani ya Kampala

Lilikuwa gazeti hilo hilo la mjini Berlin, Die Tageszeitzung, lililozungumzia kuhusu mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na waasi wa M23 mjini Kampala.

"Umoja wa Mataifa unakorofisha utaratibu wa amani" ndicho kichwa cha maneno cha ripoti ya gazeti hilo inayozungumzia kuhusu marufuku ya kusafiri waliowekewa waasi wa M23 na Umoja wa mataifa mjini New York.

Mbali na marufuku ya kusafiri, vikwazo vya Umoja wa Mataifa kwa M23 vinazungumzia pia juu ya kuzuiliwa shughuli zote za fedha pamoja na M23.

Die Tageszeitung linajiuliza kuhusu hatima ya mazungumzo ya amani ya mjini Kampala.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/All Presse
Mhariri: Josephat Charo