1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jaji Bomani asema hali ya Zanzibar yatishia eneo zima

George Njogopa17 Desemba 2015

Mwanasheria mkuu wa zamani wa Tanzania, Jaji Mark Bomani, anasema hali ya kisiasa visiwani Zanzibar inatishia mustakabali wa eneo hilo na kama uchaguzi mpya utafanyika basi lazima usimamiwe na jopo maalumu la wataalamu.

https://p.dw.com/p/1HOyU
Picha: DW/M. Khelef
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mwanasheria huyo amesema kuwa kile kinachoendelea visiwani humo hakiashirii picha njema hivyo akashauri kuchukuliwa kwa hatua za kibusara kwa ajili ya kukwamua mzozo huo.
Ikiwa ni kauli yake ya kwanza tangu kufutwa kwa uchaguzi huo miezi miwili iliyopita, Jaji Bomani amesema kuwa iwapo hali hiyo itaachwa iendelee inaweza kusababisha madhara makubwa jambo ambalo linaweza kuirudisha nyuma Zanzibar.

Kauli hiyo imekuja huku kukiwa na ripoti kwamba viongozi wa pande zote CCM na CUF wamekuwa wakikutana mara kwa mara Ikulu ya Zanzibar katika kile kinachoelezwa kuwa ni jitihada za kujaribu kutanzua hali hiyo.

Tangu kuanza kwa vikao hivyo hakuna upande uliokuwa tayari kuelezea maendeleo yaliyofikiwa huku baadhi ya maofisa wa CUF wakiendelea kusisitiza haja ya kutolewa kwa matokeo ya uchaguzi huo ambao ulifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha.

Ama mwanasheria huyo ambaye amekuwa akitokeza mara kwa mara kutoa maoni yake pindi kunapojitokeza utata katika masuala ya kitaifa, amesema kuwa pande zote mbili yaani CCM na CUF bado haziaminiani hivyo iwapo hata kutarudiwa kwa uchaguzi huo hali itajirudia ile ile.

Kwa maana hiyo alitaka kuundwa kwa jopo maalumu la wataalamu wa mambo ikiwamo kutoka jumuiya ya kimataifa ili kushughulikia uchaguzi mwingine.

CCM Zanzibar yaendelea kung'ang'ania uchaguzi
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.Picha: DW/M. Khelef
Hayo yakiarifiwa, visiwani Zanzibar hali imeendelea kuwa ya taharuki kutokana na kutojuilikana hasa hatima ya mzozo huu. Hivi leo, mitandao ya kijamii ilizagaa taarifa za baadhi ya viongozi wa CCM kujitayarisha kuchukuwa hatua za kushinikiza kutangazwa kwa tarehe ya uchaguzi mpya, licha ya mazungumzo yanayoendelea.
Akizungumza na DW kwa njia ya simu akiwa mjini Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai, alisema pamoja na kuwa wanayaunga mkono mazungumzo yanayofanyika kuukwamua mkwamo wa kisiasa na kisheria uliopo "bado lazima sheria zifuatwe".
CCM inaunga mkono tamko la kufutwa kwa uchaguzi la hapo tarehe 28 Oktoba 2015 na inasisitiza kuwa lilitolewa kwa mujibu wa sheria za nchi, hoja inayopingwa vikali na wanasheria mbalimbali nchini Tanzania.
Kufutwa kwa uchaguzi huo ambao ni tukio la kihistoria kwa siasa za Tanzania kulikosolewa pia na wawakilishi kadhaa wa jumuiya za kimataifa ikiwamo zile zilizotuma waangalizi wake katika uchaguzi huo.

Marekani, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya na taasisi za kiraia ni baadhi ya wale walijitokeza na mapema kulaani hatua hiyo wakitaka matakwa ya wananchi wa Zanzibar yasikilizwe.

Uchaguzi wa Zanzibar mara zote umekuwa ukiibua masuala tete na wakati mwingine kuchafua hali ya kisiasa.

Majadiliano ya mwaka 2009 kati ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani Karume, na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kwa kiasi kikubwa yalifanikiwa kuzika hali ya uhasama na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa serikali ambayo kwa sasa iko majaribuni kutokana na mvutano huu unaoendelea.
Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Khelef